MAHAKAMA ya Afrika inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu, jana
imetoa hukumu katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher
Mtikila ambayo italazimisha kusitishwa kwa Bunge la Katiba ili kupisha
utekelezaji wa sehemu ya hukumu hiyo ambayo ni ya kikatiba.
Katika hukumu hiyo, mahakama imeitaka serikali kutekeleza kwa vitendo
hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Juni 14, mwaka jana katika kesi ya
kudai mgombea binafsi katika uchaguzi wa ngazi zote, iliyofunguliwa na
Mchungaji Mtikila dhidi ya serikali.
Akisoma hukumu hiyo, Rais wa majaji wa mahakama hiyo, Jaji Sophia
Akuffor mbele ya wawakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitaka
serikali ya Tanzania ndani ya miezi sita kwanza kutangaza katika gazeti
la serikali hukumu iliyompa ushindi Mchungaji Mtikila ya mgombea binafsi
na pia kutangaza hukumu hiyo katika wavuti ya serikali.
Jaji huyo aliitaka serikali kuwasilisha katika mahakama hiyo
utekelezaji wa hukumu hiyo na kubainisha kuwa imeweka katika mchakato
suala la mgombea binafsi ili kutekeleza hukumu hiyo.
Alisema pia katika matangazo hayo, hukumu hiyo iwe imetafsiriwa
katika lugha nyepesi ya Kiswahili na Kiingereza ili kuwawezesha wananchi
wote kuisoma vizuri.
Hukumu hiyo imeipa serikali miezi tisa iwe imewasilisha kwa maandishi
na vielelezo vya kuonyesha imetekelezaje hukumu hiyo ya jana na
vipengele vyake vyote vya hukumu.
Mbali ya kuishindilia serikali katika hukumu hiyo, Jaji Akuffor
alitupilia mbali madai ya Mchungaji Mtikila katika kesi yake ya msingi
namba 011 ya mwaka 2013 ya kutaka kulipwa fidia za gharama za kesi kwa
wanasheria wake, gharama za yeye kupewa manyanyaso na serikali akidai
haki hiyo kabla ya kufungua kesi hiyo ya kihistoria na pia gharama
alizotumia katika mchakato mzima wa kesi yake ya awali ya kudai mgombea
binafsi ambayo alishinda.
Katika msingi wa kesi hiyo ya madai, Mtikila alitaka kulipwa zaidi ya
sh bilioni 9 za gharama zote kwa kushinda kesi ya awali, madai ambayo
mahakama hiyo baada ya kuyapitia, ilikosa vielelezo vya kuyathibitisha.
Akitupilia mbali madai ya Mtikila kunyanyasika kibinadamu kwa kukosa
haki yake ya mgombea binafsi, Jaji Akuffor alifafanua kuwa kwa hukumu
iliyotolewa mwaka jana na kumpa ushindi, ilitosha kufidia machungu
aliyoyapata katika kuikosa haki hiyo.
Awali Mtikila alipinga mwananchi wa Tanzania, kulazimishwa kujiunga
na chama cha siasa ndipo apate sifa ya kuwa mgombea katika chaguzi
mbalimbali za kisiasa, ikiwemo urais, ubunge na udiwani.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya ushindi huo, Mchungaji Mtikila
alisema hukumu hiyo ni ushindi mkubwa kwa Watanganyika wote kwani
kuanzia sasa watakuwa na nafasi ya kumchagua mtu wanayemuona anawafaa
kuwaongoza bila kujali siasa za vyama.
Alisema kwa hukumu hiyo, ni wazi hakuna uwezekano wa kuendelea kwa
mchakato wa Bunge la Katiba hadi pale vipengele vya mgombea binafsi
vitakapowekwa katika rasimu ya katiba mpya:
“Baada ya hukumu hii…siku chache zijazo naleta tena maombi mapya ya
kufutilia mbali Bunge la Katiba kwa kuwa limekiuka katiba ya nchi kwa
wajumbe wake kuteuliwa na mtu mmoja kwa maslahi ya kikundi cha watu
wachache,” alisema Mtikila.
Alifafanua kuwa katika kesi hiyo ataitaka mahakama iilazimishe
serikali kuwaachia wananchi wajitengenezee katiba yao badala ya sasa
kutengenezewa katiba na watu wachache, tena wote wakiwa wanasiasa kwa
maslahi yao ya kisiasa:
“Jamani wote mnashuhudia jinsi wajumbe waliochaguliwa na mtu kuingia
katika Bunge hilo la katiba wengine wakiwa hawana sifa na ambao
tutawataja kwa majina wakati ukifika…ambao kazi yao katika Bunge lile ni
kuzomea watu tu,” alisema Mtikila.
Akinukuu baadhi ya maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Mtikila
alisema muasisi huyo katika mambo ya msingi ambayo aliona kwa wakati huo
bado Watanzania hawana uwelewa nayo wa kutosha, aliyaacha ili kutoa
muda kwa wananchi wake wajifunze kwanza.
Mawakili wa serikali waliokuwepo mahakamani hapo, walikataa
kuzungumzia hukumu hiyo kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa idara hiyo.
Chanzo: TanzaniaDaima