https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-zitto-aitolea-uvivu-serikali.html
Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema),
Zitto Kabwe amesema unafuu wa Kodi ya Mshahara (Paye), uliotangazwa na
Serikali kwamba umeshuka kutoka asilimia 13 hadi 12 ni mdogo
hautamsaidia mfanyakazi kubaki na fedha kwa ajili ya matumizi wala
kujiwekea akiba.
Katika mchango wake wa maandishi kwa Bajeti ya
Serikali jana, Zitto alisema ni dhahiri kuwa Paye ni chanzo kikubwa cha
mapato ya ndani ya Serikali lakini akapendekeza kipunguzwe zaidi.
Mbunge huyo alishauri kiwango cha chini cha
mshahara unaokatwa kodi kiwe Sh330,000 na kiwango cha chini cha kodi
kiwe asilimia tisa.
“Kiwango hiki cha kodi pia kinawezekana kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabovu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kwa mfano, kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi Mkuu
wa ndani wa Serikali mwaka 2013, mfumo wa kukagua utumishi wa umma
umegundua kuwa jumla ya wafanyakazi wa Serikali 6,500 walikuwa
wameajiriwa mara mbili kwa majina yaleyale, 2,700 mara tatu na kulikuwa
na watumishi 2,500 waliokuwa wanachukua mishahara miwili mpaka mitatu
kila mwezi.”
Alisema hatua ya kuondoa matumizi mabovu kutokana
na kulipa mishahara hewa pia inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kodi
kwa wafanyakazi nchini.
“Serikali hutumia wastani wa Sh360 bilioni kila
mwezi kulipa mishahara na kati ya hizo Sh10 bilioni zimekuwa zikilipwa
kwa watumishi hewa,” alisema Zitto.
Alisema nafuu ya kodi kwa wafanyakazi nchini
katika sekta zote na hasa wafanyakazi wa kima cha chini itachochea
matumizi binafsi ya bidhaa na huduma na hivyo kuchangamsha uchumi na
kuwezesha uwekaji wa akiba.
“Nashauri ukaguzi zaidi ufanyike katika utumishi wa umma ili kumaliza kabisa tatizo la wafanyakazi hewa.”
Aliipongeza Serikali kwa kuanzisha kodi ya zuio ya
ada kwa wakurugenzi wa kampuni na mashirika akisema itaongeza mapato ya
Serikali.