BUNGENI: UTORO WA WABUNGE KATIKA BUNGE LA WAAKILISHI ZANZIBAR WAKWAMISHA BAJETI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-utoro-wa-wabunge-katika-bunge.html
Zanzibar. Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) limekwama kukaa kama kamati ya matumizi na vikao kwa mara ya tano tangu kuanza kujadili bajeti za mwaka wa fedha 2014/15 Mei 14 mwaka huu kutokana na tatizo la wajumbe kuwa watoro wa kuhudhuria vikao.
Hali hiyo imekuwa ikimlazimu Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Naibu Spika Ali Abdallah Ali na
Mwenyekiti wa Baraza hilo Mgeni Hassan Juma kushindwa kuitisha Kamati ya
Matumizi kutokana na kutotimia akidi ya asilimia 50 ya wajumbe 40 kati
ya wajumbe 82.
Tukio la aina hiyo lililotokea mwishoni mwa wiki
baada ya Naibu Spika Ali Abdallah Ali kujikuta akiahirisha Baraza hilo
kutokana na uchache wa wajumbe wakati wakijadili bajeti ya Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati iliyowasilishwa na Waziri Ramadhan
Abdallah Shaaban.
Naibu Spika alisema pamoja na Waziri kukamilisha
mjadala wa bajeti yake, Kamati ya Matumizi haitaweza kuendelea kukaa na
kupitisha vifungu kutokana na akidi ya wajumbe kutofikia asilimia 50.
‘Kutokana na akidi ya wajumbe kutokamilika, Baraza
halitaweza kukaa kama kamati na kupitisha vifungu, nalazimika
kuahirisha kikao hiki,” alisema Naibu Spika.
Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Nassor Salim Ali
alisimama na kutaka mwongozo akitaka kujua sababu ya wajumbe kutotimia
ili wananchi waweze kufahamu mahali waliko wawakilishi wao hasa kwa
kuzingatia kuwa tatizo hilo limekuwa likijitokeza kila mara.
Naibu Spika alisema tatizo hilo limekuwa likitokea
kutokana na sababu mbalimbali na kuwataka wajumbe kuhakikisha
wanahudhuria kwa wakati mwafaka ili kazi iliyokuwa imelala iweze
kufanyika kwa wakati sahihi na mwafaka.
Mkasa huo ulitanguliwa na ule wa Baraza kushindwa
kukaa kama kamati wakati ikijadiliwa Bajeti ya Wizara ya Viwanda,
Biashara na Masoko kutokana na idadi ya wajumbe kuwa wachache ambapo
kamati ya matumizi ilishindwa kukaa na kupitisha vifungu vya matumizi
chini ya Mwenyekiti wa Baraza hilo Mgeni Hassan Juma mbali na matukio
mawili yaliyotokea ya akidi kutotimia huku Spika wa Baraza hilo akikalia
kiti.
Hali ya mahudhurio iliendelea kuwa mbaya zaidi
baada ya wajumbe wengi wa CUF kuhudhuria Mkutano Mkuu wa chama chao
uliokuwa ukifanyika jijini Dar es Salaam.
Wakati wajumbe wa CUF wakitingwa na vikao vya
mkutano mkuu, wale wa CCM wamekuwa wakihudhuria vikao vya Bunge huko
Dodoma kutokana na kuwa na kofia mbili kwa wakati mmoja kutokana na kuwa
wawakilishi na wabunge wa kuteuliwa.
Aidha, Spika Pandu Ameir Kificho tayari
amekwishakemea mara mbili tabia ya utoro na kuwataka wajumbe kutambua
dhamana waliyonayo kwa taifa na umuhimu wao wa kuhudhuria vikao kama
wawakilishi wa wananchi.
Wawakilishi hulipwa posho ya kikao kimoja kwa siku Sh150,000 mbali na mshahara wa Sh4.5 milioni kwa mwezi.
CHANZO: MWANANCHI