JAMII: BIBI AUAWA KIKATILI KWA KUKATWA SHOKA KICHWANI HUKO SHINYANGA (Tunaomba Radhi kwa picha)

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/jamii-bibi-auawa-kikatili-kwa-kukatwa.html
Bibi mmoja Mkazi wa mtaa wa Nyahanga,
wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Rebeka Sengasenga (82), ameuawa kwa
kukatwa na Shoka kichwani kwa kile kinachohisiwa kuwa ni imani za
Kishirikina.
Kwa mujibu wa majirani, tukio hilo
limetokea jana asubuhi katika Mtaa wa Nyahanga, wilayani humo, ambapo
Marehemu Rebeka alienda nyumbani kwa mtoto wake Bundala Sengasenga
alikokuwa ameitwa na mke wa Bundala kusaidia kuanika Dengu.
Imeelezwa kuwa Merehemu Rebeka ambaye
alikuwa akiishi kwa mwanae mkubwa Stanley Sengasenga katika mtaa huo
alifika kwa Bundala baada ya kuitwa na Magreth Richard ambaye ni mke wa
Bundala kwa ajili ya shughuli hiyo.
Katika
maelezo yake Magreth amesema Mama mkwe wake Marehemu Rebeka alifikia
sebuleni, na kwamba wakati yeye yuko nje, alimwona mtu ambaye hakuweza
kumfahamu akitoka sebuleni hapo na kukimbia ndipo alipoangalia na
kumkuta Rebeka ameuawa.
Taarifa za awali zimedai, kabla ya
tukio hilo Magreth ambaye kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi
mjini Kahama kwa mahojiano alienda nyumba ya jirani kuazima Shoka,
ambalo baadaye limekutwa kwenye shimo la maji taka nyumbani hapo.
Shoka
hilo limepatikana baada ya mbinu za kiupelelezi za Jeshi la Polisi
kuagiza gari la maji taka kuyavuta maji hayo baada ya majirani kudai
hawajaona mtu aliyekimbia na shoka muda huo katika mwelekeo ambao
Magreth ameelekeza.
Jeshi
la Polisi wilaya ya Kahama limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kwamba Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
katika hospitali ya Wilaya ya Kahama, huku upelelezi ukiendelea.