SIASA: WASOMI WADAI AHADI ZA JK 2010 ZAICHIMBIA KABURI CCM 2015, WADAI CCM YA SASA IKO KWENYE MACHELA

https://jaridahuru.blogspot.com/2015/01/siasa-wasomi-wadai-ahadi-za-jk-2010.html
Dar es Salaam. Ahadi zilizotolewa na Rais
Jakaya Kikwete kwa wananchi katika mikutano mbalimbali nchini wakati wa
kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, huenda zikawa mwiba kwa CCM katika
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, kutokana na nyingi
kutokutekelezwa au kuwa katika hatua za mwanzo.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Taifa, kwa nyakati tofauti alitoa ahadi kusaidia kuwakwamua wananchi
kutoka kwenye dimbwi la umaskini, maradhi na kuboresha upatikanaji wa
elimu nchini. Ahadi hizo zilitarajiwa kukamilika kabla hajatoka
madarakani.
Ikiwa imebaki takriban miezi 10 ya uongozi wa
kipindi cha pili cha awamu ya nne kufikia ukomo, muda unakwenda haraka
na utekelezaji wa ahadi hizo unasuasua jambo linalotia shaka iwapo kila
ahadi itatekelezwa kwa wakati.
Kushindwa kutekeleza ahadi hizo ambazo zimo katika
kitabu cha ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete wakati wa kampeni za urais 2010, kilichondaliwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, kunaiweka Serikali ya CCM katika wakati mgumu hasa pale
itakaporudi kwa wananchi kutoa ahadi nyingine kwenye kampeni za uchaguzi
mkuu ujao.
Nape
Alipoulizwa kuhusu ahadi hizo, Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Rais Kikwete ametekeleza ahadi
zaidi ya inavyoahidi ilani ya CCM.
“Ukitaka kumtendea haki Rais Kikwete katika
utekelezaji wa ahadi zake, lazima uangalie kitabu chote cha ahadi harafu
upate ushahidi wa viongozi wawakilishi au kuzunguka kwenye maeneo
zilizokotolewa ahadi hizo,” alisema na kuongeza;
“Kwa ufupi tu, Rais huyu amefanikiwa kutekeleza ahadi nyingi ambazo ziko kwenye ilani na zile alizotoa papo kwa papo.”
Hata hivyo Nape alimwahidi mwandishi wa gazeti
hili kutoa ufafanuzi wa ahadi zilizotekelezwa na Rais kwa kipindi chote
alichokaa madarakani wiki ijayo.
Turuka
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens
Turuka alisema ofisi yake kwa sasa iko kwenye uchambuzi na uandaaji wa
kitabu kitakachoeleza utekelezaji wake.
Turuka alisema kazi hiyo itakamilika kwa miezi miwili kuanzia
sasa.“Yapo mengi sana aliyoyafanya rais, lakini tutaweka wazi wala siyo
siri, kazi zote alizofanya zinaonekana ila kwa sasa itakuwa vigumu
kubainisha kiwango cha ahadi alizotekeleza,” alisema Turuka.
Rais Kikwete alipokuwa wilayani Bunda, Mkoa wa
Mara aliahidi kutokomeza ugonjwa malaria ifikapo mwaka 2015, lakini
mpaka sasa ugonjwa huo umebaki kuwa tishio na ukipoteza maisha ya
Watanzania wengi kila mwaka.
Rais Mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania
(MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa kwa mujibu wa malengo ya
Milenia, Tanzania imepunguza vifo vitokanavyo na malaria licha ya
kuendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa.
Alisema kwa hali ilivyo hivi sasa nchini, ambapo
dawa hazipatikani kwa kiwango kinachotakiwa ni vigumu kufanikiwa
kutokomeza ugonjwa huo kwa asilimia 100 mwaka huu.
“Kama tukipata Rais mzuri ambaye ataweka nguvu
kwenye sekta ya afya, malaria inaweza kuondoka kwa asilimia 100 baada ya
miaka 15,” alisema Dk Saidia.
Akiwa wilayani Nzega mkoani Tabora, Rais Kikwete
aliahidi kuwa Serikali yake ingejenga reli mpya kutoka Dar es Salaam
mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijakamilika
ingawa tayari ameshakutana na Kampuni ya China Railway Group Limited
inayotarajiwa kutekeleza mradi huo.
Pia, akiwa Tanga Mjini, Rais Kikwete aliahidi
kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa jiji la viwanda. Ahadi hiyo mpaka sasa
haijakamilika ingawa tayari maeneo kwa ajili ya wawekezaji
yamekwishatengwa.
Akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora, Rais Kikwete
aliahidi kuwa wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji kutoka Ziwa
Victoria. Ahadi hiyo mpaka sasa haijakamilika japokuwa akijibu swali
bungeni, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge alisema mwaka 2013/14
Serikali ilitenga Sh450 milioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu
wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni.
Ahadi nyingine za Rais Kikwete ni pamoja na
kumaliza migogoro ya ardhi nchini, wakulima kuacha kutumia jembe la
mkono na kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba iliyozama Mei 21, 1996.
Pia, kiongozi huyo wa nchi aliahidi kuimarisha
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kwa miaka
mitatu, kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali na
kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi
maalumu chenye vifaa vya kupambana na wahalifu.
Katika orodha ya ahadi hizo, pia Rais Kikwete
aliahidi kumaliza tatizo la walimu nchini. Hata hivyo, bado walimu
wameendelea kuinyooshea kidole Serikali wakilalamikia kushindwa
kuwapandisha madaraja, malimbikizo ya madeni na mishahara midogo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiah Oluoch alisema licha ya kuwa Rais Kikwete amefanya mambo
mengi tangu alipoingia madarakani, ataiacha nchi ikiwa njiapanda
kielimu.
Alisema Rais Kikwete aliahidi kutatua tatizo la kupandishwa
madaraja walimu, lakini mpaka mwisho wa mwaka huu kutakuwa na walimu
120,000 wanaostahili kupandishwa madaraja.
Akifafanua alisema: “Mwaka jana walimu 40,000
hawakupandishwa madaraja, mwaka huu wengine 40,000 walitakiwa
kupandishwa na Julai, 2015 wengine tena watahitaji kupandishwa
madaraja.”
Oluoch alieleza kuwa Rais Kikwete aliwaahidi
walimu kuwa angewaanzishia tume yao, lakini mpaka sasa hakuna hata
muswada uliotayarishwa.
Pia, alisema Oktoba 5, 2010 huko Songea mkoani
Ruvuma, Rais Kikwete aliwaahidi walimu kuwa angeunda Bodi ya Taaluma ya
Walimu, lakini jambo hilo bado halijatekelezwa.
“Hili tunaliona kama ni deni, Rais asiondoke Ikulu bila kutekeleza ahadi hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Serikali ya awamu ya nne inaiacha
nchi njiapanda kielimu, elimu haikupaswa kusimamiwa na Tamisemi
inatakiwa isimamiwe na Wizara ya elimu.”
Vilevile, Rais Kikwete aliahidi kuwajengea nyumba
waathirika wa mafuriko ya Kilosa, kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa na
kujenga Bandari Kasanga.
Ahadi zingine ni kufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe wa
Kiwira, kuzuia hatari ya Kisiwa cha Pangani kuzama, kumaliza tatizo la
maji katika Wilaya ya Same, kusambaza walimu 16,000 katika shule za
sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu na kununua vyandarua viwili
kwa kila kaya.
Rais Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la ukosefu
wa umeme mkoani Arusha, kukopesha wavuvi zana za kilimo, kuwapatia maji
wakazi wa Wilaya ya Longido, kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni
mwa Hifadhi ya Taifa ya Seregenti na kusambaza maji nchi nzima.
Kuhakikisha Jimbo la Isimani linapata maji ya
uhakika, kuweka lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya
Ruaha na Serikali kujenga upya Bandari ya Mbambabay.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel
Ruhuza alisema Rais Kikwete anaweza kutekeleza ahadi zake kwa asilimia
zaidi ya 70 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Lazima tuwe wakweli huyu Rais amefanya mengi
sana, yaani ukiangalia kuna ahadi nyingi kafanya japokuwa hawezi
kumaliza zote kwa muda uliobakia,” alisema Ruhuza.
Hata hivyo, aliongeza kuwa baadhi ya ahadi ambazo
hazijatekelezwa mpaka sasa ni pamoja na ujenzi wa barabara za
Kigoma-Nyakanazi(km330),
Lulenge-Mulungarama(km100),Karagwe-Ngara(km150).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la
Watendaji wakuu wa Makampuni nchini(CEOs Roundtable-Tanzania),Ali
Mufuruki alisema ahadi alizotekeleza n8i nyingi japokuwa hataweza
kumalizia zilizobakia.
“Lakini labda nikupatie mfano, unaweza kuahidi
watoto wako zawadi na ukawanunulia wote, inatokea wengine wanakosa kwa
hivyo sioni kama ni tatizo hilo,” alisema Mufuruki.
~MWANANCHI
~MWANANCHI