KITAIFA: MMBONGO AKAMATWA NA PESA BANDIA ZENYE THAMANI YA TSH MIL 400, AKIRI KUZINUNUA ISEBANIA KENYA

https://jaridahuru.blogspot.com/2015/01/kitaifa-mmbongo-akamatwa-na-pesa-bandia.html
JESHI
la Polisi mkoani hapa linamshikilia mkazi wa Buzuruga jijini hapa,
Zakaria Matiku Werema (35) baada ya kukamatwa akiwa na fedha bandia za
Tanzania na za kigeni, ambazo kama zingekuwa halali zingekuwa na thamani
ya zaidi ya Sh milioni 400.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema jana kuwa mtuhumiwa
huyo alikamatwa Januari 2, mwaka huu, majira ya saa 8:00 alipokuwa
kwenye harakati za kutafuta wateja.(MM)
Alisema
mtuhumiwa huyo alikamatwa kwenye mtaa wa Rwegasore wilaya ya Nyamagana
jijini hapa akiwa na noti bandia za Sh elfu tano tano zenye thamani ya
Sh 11,955,000, ambazo alizificha ndani ya kasha dogo la kuhifadhia glasi
na kulivisha mfuko mweusi.
Alisema
mtuhumiwa baada ya kukamatwa, askari walikwenda naye nyumbani kwake
Buzuruga kwa ajili ya upekuzi, ambako walifanikiwa kumkuta na dola
bandia za Marekani 244,100 sawa na Sh 414, 970,000 za Tanzania na fedha
bandia za Tanzania Sh 12,000,000 ambazo alizificha kwenye kona chumbani
kwake.
“Mtuhumiwa
tulimkamata akiwa na fedha bandia Shilingi 23,955,000 na dola bandia za
Marekani 244,100, kama fedha hizo zote zingekuwa ni halali zingekuwa na
thamani ya Shilingi 438,925,000, endapo zingeingia kwenye mzunguko
zingesababisha madhara makubwa na ni wazi uchumi wa nchi yetu
ungeyumba,” alisema Kamanda huyo.
Aliongeza
kuwa walipomfanyia mahojiano, mtuhumiwa alikiri kununua fedha zote hizo
eneo la Isibania nchini Kenya Desemba 22, mwaka jana, kwa thamani ya Sh
milioni nane za Tanzania.
Alisema
mtuhumiwa aliingiza fedha hizo bandia nchini kwa ajili ya kuziuza na
kwamba alipanga kuuza Sh 300,000 halali kwa Sh 1,000,000 bandia na dola
moja alipanga kuiza kwa Sh 800 ya Tanzania.
Polisi
wanaendelea kumhoji ili kubaini na kuuvunja mtandao wote, unaojihusisha
na biashara hiyo haramu. Kamanda Mlowola alitoa rai kwa wafanyabiashara
wa jiji na mkoani hapa kuwa waangalifu wanapofanya miamala ya fedha za
kigeni na pia watilie shaka pale wanapouziwa fedha za kigeni kwa bei ya
chini.
HABARILEO