jaridahuru

Mitandao

KITAIFA: KISANGA CHA POLISI KUWAPIGA WAANDISHI WA HABARI CHAGEUKA MWIBA KWA JESHI LA POLISI NCHINI




WADAU wa Habari nchini wamelaani kitendo cha askari polisi kuwapiga waandishi wa habari waliokuwa kwenye majukumu yao na kuitaka serikali kuchukua hatua stahili.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeitaka serikali kulivunja na kuliunda upya Jeshi la Polisi kutokana na kukithiri kwa matukio ya kuwadhuru raia wasio na hatia, jambo linalochafua sifa ya Tanzania ulimwenguni.

Kauli ya TEF ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda, alipozungumza na waandishi wa habari kulaani kipigo cha polisi kwa waandishi wa habari waliokuwa kazini.

Waandishi waliopigwa ni Yusuf Badi wa magazeti ya serikali (TSN), Josephat Isango wa Free Media na Shamim Ausi kutoka Hoja, ambao walikuwa nje ya makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakimsubiri Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe aliyeitwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusu kauli ya kuitisha maandamano nchi nzima.
Kibanda, alisema kupigwa kwa waandishi hao ni mwendelezo wa uhalifu unaofanywa na askari wajinga ambao hawajifunzi na kwamba wanafanya uhalifu huo kwa makusudi.

“Katika mazingira haya tunataka jeshi la polisi livunjwe kisha liundwe upya, kwani hata chini ya mkuu wake mpya, IGP Ernest Mangu na Naibu wake ambaye pia ni mwanahabari mwenzetu, Abdulrahman Kaniki, bado polisi wanaendeleza ujinga ule ule wa kufanya kazi bila kuzingatia weledi na kuheshimu haki za binadamU katika kutekeleza wajibu wao.

“… TEF inaamini kwamba hiki kilichotokea juzi hakikuwa bahati mbaya hata kidogo, kilifanywa kwa makusudi kwa maana kwamba, polisi walikusudia kuwapiga na kuwajeruhi waandishi wa habari.

“Tunasema hivyo kwa sababu kuna ushahidi kwamba, waliopigwa walionesha vitambulisho vyao mapema, tunakumbuka kifo cha Daudi Mwangosi aliyeuawa mikononi mwa polisi, tena kwa kupigwa bomu… mauaji hayo yalifanyika mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa wakati huo, afande Michael Kamuhanda ambaye baada ya ‘kufanya kazi yake vizuri’ (kwa maono ya Jeshi la Polisi), alipandishwa cheo na kuhamishiwa makao makuu,” alisema Kibanda.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kiashiria kingine cha uadui wa polisi na vyombo vya habari ni kutoshiriki kwao katika mkutano wa vyombo vya habari na vile vya ulinzi na usalama pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliyewataka watendaji wa vyuombo hivyo kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alitaka serikali kuchunguza kwa kina matukio ya polisi kuwapiga wanahabari ili kujua hasira za polisi zinatokana na nini, huku akisisitiza kwamba, wanahabari watatumia kalamu zao na zana nyingine kulaani uhalifu huo dhidi yao.

Aidha, Kibanda alisema jukwaa litaandika barua rasmi kwa IGP Mangu, kutaka ufanyike uchunguzi maalumu na wahusika wachukuliwe hatua stahiki.

BARAZA LA HABARI
Pamoja na kulaani kitendo hicho, Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, alisema katika dunia ya leo vitendo vya kikatili vinafifisha uhuru wa habari, kuleta aibu na kushusha hadhi ya taifa na kumdhalilisha rais wa nchi machoni pa mataifa, kwa kuwa ni muumini wa makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi.

“MCT inaamini kuwa, kushambuliwa kwa waandishi wa habari haikuwa bahati mbaya, kwani huu ni mfululizo wa jeshi hilo kuwanyanyasa waandishi wanapokuwa kazini jambo linalolalamikiwa kwa muda mrefu sasa.

“Pamoja na polisi kujua umuhimu wa waandishi wa habari, tukio la jana ni la kikatili, limefanyika licha ya juhudi zao za kujitambulisha huku wengine wakiwa wamebeba vitendea kazi,” alisema Mukajanga.

WAHAMAZA
Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza), kimepokea kwa masikitiko makubwa mwendelezo wa askari polisi kuingilia uhuru wa waandishi wa habari. Tukio la Septemba 18, 2014 la askari kuwasukuma na kuwapiga waandishi wa habari walipokuwa wanafuatilia tukio la kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe, na kuwazuia wandishi kufanya kazi zao halikubaliki.
Kwa mujibu wa Katibu wa Wahamaza, Salma Said, huu ni wakati wa kujenga uhusiano mzuri wa kufanya kazi kati ya polisi na wandishi wa habari hasa wakati fujo inapotokea.

“Tunaotoa wito kwa uongozi wa polisi nchini kutoa maelekezo ya mara kwa mara kwa askari wote kutoa ushirikiano muda wote kwa wandishi wanapofanya kazi yao. Askari yoyote anayetenda kinyume achukuliwe hatua za kisheria,” alisema Salma na kuongeza.

Wandishi wa habari siku zote wamekuwa wasikivu na kufuata sheria, lakini inasikitisha kuona askari polisi wanashindwa kutoa maelekezo kwa waandishi wa habari na badala yake kuwazuia kufanya kazi.

OJADACT
Mwenyekiti Chama cha Waandishi wa Habari za Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT), Edwin Soko, amelitaka jeshi hilo kuomba radhi kwa waandishi wa habari ndani ya siku saba, vinginevyo watasusia kuandika habari zao.

Soko, alisema hayo mjini Mwanza jana alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa UTPC Nyanza na kusema jeshi hilo limewadhalilisha waandishi waliyokuwa wakitimiza wajibu wao.
Alitaka pia iundwe tume ya kuchunguza uhusiano wa polisi na wanahabari, hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 sanjari na kumtaka waziri mwenye dhamana kuwajibika kwa kushindwa kulisimamia vema jeshi hilo.

CHADEMA
CHADEMA, wamelaani kitendo cha viongozi wa Jeshi la Polisi kuongoza katika kupigwa waandishi wa habari kama mbwa koko.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari, Tumain Makene, alisema chama hicho hakiamini kama kitendo kile kinaweza kutokea mbele ya viongozi wa wizara hiyo huku wakikaa kimya.

Alisema wanalaani tukio hilo, kwa sababu linaonekana ni la kupangwa ili kuwanyamazisha waandishi wa habari katika juhudi zao za kutoa taarifa za uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba unaondelea kwenye Bunge maalum la Katiba mjini Dodoma.

Alisema mazingira ya kupigwa wandishi wale linafanana na lile la kupigwa bomu lililosababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Chanel Ten, Daud Mwangosi, miaka miwili iliyopita.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mtwara, Kassim Bingwe, alisema kitendo cha kupigwa na kuwajeruhiwa kwa waandishi waliokuwa katika majukumu yao ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kinatakiwa kikemewe.

“Lazima wahusika wachukuliwe hatua kali… waandishi walikuwa wanatekeleza majukumu yao ilikuwaje polisi wawazuie wasifanye kazi zao? alihoji Bingwe.

BULAYA CCM
Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya (CCM), naye amelaani kitendo cha polisi kuwashushia kipigo waandishi wa habari waliyokuwa kwenye majukumu yao.

Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Bulaya alisema; “Waandishi wamejitambulisha lakini bado polisi wamewanyanyasa badala ya kuwalinda, kimeniuma kwa kuwa nami ni mwanahabari… hii kazi ya ubunge inaweza kuisha lakini fani yangu ya habari nitakuwa nayo na ninaweza kurejea,” alisema.

WATETEZI HAKI ZA BINADAMU
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD-Coalition), na waandishi wa habari, wamelaani kitendo cha polisi kuwapiga waandishi wa habari na kuwanyima haki ya kutimiza wajibu wao.
Mratibu wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa, alisema inasikitisha ikizingatiwa kwamba ilikuwa siku moja baada ya vyombo vya haki kukutanishwa na wadau wa habari kisha kukubaliana namna ya kufanya kazi katika mazingira rafiki, likiwemo jeshi hilo uliondaliwa na Baraza la Habari nchini (MCT).

“Kwa kitendo hicho sasa polisi anaonekana sio mtu wa kukimbiliwa tena… inajenga uhasama kati ya raia na wao,” alisema Mratibu huyo.

Naye Mratibu wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu chapta ya Tanzania (SAhRINGON), Martina Kabisama, alitoa wito kwa jeshi hilo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria badala ya kuwapiga raia.

Mwandishi wa kituo cha ITV, Alkadi Belesi aliwataka waandishi waseme imetosha kwa kuwa serikali inaonekana kushindwa kuwaadhibu askari wake waovu.

Chanzo:FreeMedia

Related

Kitaifa 6427143946645177830

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item