SIASA: ONYO LA CHADEMA KWA WAGOMBEA WAKE LAMTIA KIWEWE FREEMAN MBOWE, ATAKA APELEKEWE FOMU
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/siasa-onyo-la-chadema-kwa-wagombea-wake.html
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema wagombea wa
nafasi za kitaifa hawaruhusiwi kukutana na wajumbe wapiga kura waliyoko
mikoani, kwani kwa kufanya hivyo kuna mianya ya rushwa na atakayebainika
ataondolewa kwenye kinyang’anyiro.
Chama hicho, pia kimesisitiza kuwa suala la kugombea ni hiari ya kila
mwanachama wala sio suala la uongozi wa ngazi yoyote ya chama, hivyo
kila mgombea atekeleze wajibu kwa kujaza fomu, kuzilipia na kuzifikisha
ofisini kwa utaratibu uliowekwa.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Uratibu wa Kanda wa CHADEMA, Benson Kigaila, wakati
akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar
es Salaam.
Kigaila, alitoa msisitizo huo kukazia kanuni za kampeni na rushwa za
chama hicho, huku akitoa taarifa kuwa zoezi la kuchukua fomu na
kurejesha kwa nafasi za kitaifa limeongezewa hadi Agosti 30 mwaka huu
badala ya Agosti 25 iliyokuwa imetangazwa awali.
“CHADEMA kuna kanuni za Uchaguzi na kanuni kuhusu namna ya kudhibiti
vitendo vya rushwa, na kwa mujibu wa kanuni hizo, wagombea hufanya
kampeni ukumbini siku ya Uchaguzi,” alisema.
Akieleza sababu za kuongeza muda huo, Kigaila alisema kuwa bado kuna
chaguzi mbalimbali zinafanyika ngazi za mikoa, hivyo sekretarieti ya
chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi, iliamua kuongeza ili
wagombea wengine watakaoshinda kwenye ngazi za mikoa, wapate pia fursa
ya kugombea nafasi mbalimbali za kitaifa.
Kuhusu taarifa za uchaguzi, alisema umekamilika ngazi za misingi,
mitaa, shehia kwa upande wa Zanzibar na matawi. Ngazi za kata majimbo na
wilaya, pia zimekamilika na hadi jana ilitarajiwa mikoa 25 itakuwa
imekamilisha na kubakiza saba tu itakayohitimisha kabla ya Agosti 30.
Katika hatua nyingine, zoezi la kumkabidhi Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama hicho fomu yake na kumshawishi agombee, halikufanyika kama
ilivyotarajiwa jana.
Mmoja wa watoa taarifa ambaye aliomba asitajwe gazetini, alisema
baada ya zoezi hilo kuungwa mkono na wazee wa Dar es Salaam na Pwani,
taarifa imepelekwa kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe, na sasa
anatafuta wakati muafaka wa kukutana na wazee hao waliyotoka Kigoma
kumletea fomu aweze kutetea kiti hicho.
Aidha, kuhusu tarehe ya uchaguzi mkuu, Kigaila alisema CHADEMA
haitabadilisha na itabaki Septemba 14 kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya CHADEMA, zinasema mkutano wa
ufunguzi wa uchaguzi huo utarushwa moja kwa moja na kituo cha runinga
kwa saa tatu na pia wakati wa kutangaza matokeo, pia matangazo
yatarushwa moja kwa moja.