SIASA: NJAMA ZA KUWAUA SLAA NA MNYIKA ZAVUJA, MASELE ATAJWA KUPANGA NJAMA HIZO ILI WALIPULIWE KWENYE CHOPA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/08/siasa-njama-za-kuwaua-slaa-na-mnyika.html
HALI ya siasa nchini inazidi kuwa tete baada ya Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Stephen Masele, kuhusishwa katika njama za kutaka
kumuua Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho,
John Mnyika.
Mbali na kutajwa katika njama hizo ambazo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga
Mjini, Anarose Nyamubi anadaiwa kukataa zisitekelezwe katika wialaya
yake, Masele pia anahusishwa na kupanga kiasi cha fedha kilichotakiwa
kutolewa kwa madiwani wawili wa CHADEMA kama wangeweza kufanikisha
mkakati huo.
Tuhuma hizo nzito zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na diwani wa
Kata ya Ngokelo, Sebastian Peter kutoka mkoani Shinyanga wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CHADEMA.
Hata hivyo, wawili hao Masele na Nyamubi hawakuweza kupatikana kujibu
tuhuma hizo, na alipoulizwa msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera
Senso kama waliwahi kupokea malalamiko hayo, alisema hawana taarifa
yoyote na kwamba hao waliotoa taarifa hizo wanapaswa kuziwasilisha
polisi ili zifanyiwe kazi.
Peter maarufu kama Obama na diwani mwenzake wa kata ya Masekelo,
Zakaria Mfukwa, alisema kuwa awali walihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kwa ahadi ya kuboreshewa maisha ukiwa ni mkakati wa Waziri Masele.
Alifafanua kuwa mkakati huo wa kuwauwa viongozi hao wa CHADEMA
ulikuwa utekelezwe mapema Februari mwaka huu, wakati viongozi hao
walipofika mkoani Shinyanga kwa ajili ya kukusanya maoni ya wanancchi
juu ya muundo wa serikali.
Alisema mara baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto
Kabwe kusimamishwa uongozi wa chama hicho, walifuatwa na Habibu Mchange
na kuelezwa kuwa kuna mpango unaoweza kuwaondoa katika lindi la
umasikini ikiwa wataweza kuufanikisha.
“Baada ya maongezi ya aina mbali mbali na Mchange tulishindwa kupata
muafaka lakini tuliendelea kuwasiliana na aliporudi Shinyanga akatueleza
kuwa kuna mpango mzuri wa fedha na kwamba utasimamiwa na Waziri Masele
na kwamba tutapata sh. milioni 180 kila mmoja,”alisema.
Aliongeza kuwa alipigiwa simu na Masele na kisha kuelekezwa kazi ya
kufanya kuwa ni kutoa taarifa ya helikopta iliyombeba Dk. Slaa na Mnyika
ingetua eneo gani itakapofika Shinyanga Mjini na kwamba ni nani
wengine ambao wangekuwa katika msafara huo, huku wakielezwa kuwa jukumu
lao lingeishia katika kutoa taarifa na mikakati ya ulipuaji ingesimamiwa
na Masele.
Alisema katika mkakati huo, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mjini,
Anarose Nyamubi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
wilaya alikataa mpango huo kutekelezwa katika wilaya yake hali
iliyowafanya wao wajiulize kama wana sababu ya kuendelea na jambo hilo.
“Nilipofikiria Taifa na nikafikiria namna msiba wa Dk. Slaa na Mnyika
utakavyopokewa nikaona siwezi kutekeleza jambo hilo nilichoweza
kuwashauri ni kwamba waandae mabango ya kumzomea Dk. Slaa,”alisema
Peter.
Akizungumzia mikakati hiyo, Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu,
alisema siku zote wamekuwa wakiueleza umma juu ya njama zinazofanywa na
CCM kupitia kwa watu waliofukuzwa ndani ya CHADEMA kama Habibu Mchange
aliyetajwa kuwa nyuma ya uratibu wa mkakati huo kwa kushirikiana na CCM.
Alisema kitendo cha kutaka kulipua helikopta makosa yake yanaelekezwa
katika sheria ya kukabiliana na ugaidi na kwamba jeshi la polisi
linapaswa kuchukua hatua zinazostahili.
SOURCE: TANZANIA DAIMA