TEKNOLOJIA: TUME YA UCHAGUZI 'NEC' YAENDELEZA UTATA ZABUNI YA MASHINE ZA KUPIGIA KURA 'BVR'
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/teknolojia-tume-ya-uchaguzi-nec.html
TUME ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), imezidi kuibua utata
kuhusiana na gharama halisi za kupata mzabuni wa kuboresha daftari la
kudumu la kupigia kura kwa njia ya kielektroniki, (BVR), baada ya kudai
gharama zilizotajwa katika hukumu ya mamlaka ya ununuzi wa umma (PPAA),
si sahihi.
Hivi karibuni, PPAA iliweka katika tovuti yake uamuzi wa kesi namba
33/2013-14, kuihalalisha kampuni ya Ms Lithotec kuwa mzabuni halali
katika ukamilishaji wa vifaa vya kupigia kura kielektroniki na kuonyesha
gharama alizopewa mzabuni huyo ni dola 117,184,507.05 za Marekani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar esSalaam jana,
Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema, fedha halali walizokubaliana
na kampuni ya Lithotec kukamilisha mchakato wote ni dola 89,094,407.05
huku gharama za BVR peke yake ikiwa ni dola 71,032,500 za Marekani.
Mallaba alisema, kabla ya mkataba huo kusainiwa kati ya NEC na Ms
Lithotec, mmoja wa wazabuni MS/Morpho alilalamikia zabuni hiyo PPAA,
hali iliyowafanya wapeleke makubaliano ya awali katika mamlaka hiyo.
“Naomba ieleweke, gharama zinazotajwa sijui dola milioni 117 sisi
hatuzijui, sisi tuna gharama zetu halisi katika mkataba tofauti na
zinazoandikwa,” alisema Mallaba.
Kampuni ya MS Lithotec, imefanikiwa kupata zabuni hiyo baada ya
kuitishwa kwa mara ya pili kutokana na uamuzi wa PPAA kuitaka NEC ianze
mchakato huo upya, baada ya malalamiko ya wazabuni wengine.