SIASA: WANYE NIA UCHAGUZI UJAO WAONGEZEKA, MWANDISHI WA HABARI GAZETI LA MWANANCHI NAE ATANGAZA NIA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-wanye-nia-uchaguzi-ujao.html
MWANDISHI wa Habari Dismas Lyassa ametangaza nia ya kuwania urais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) utakaofanyika Agosti 4 na 5 mwaka huu.
Lyassa anatangaza uamuzi huo baada ya nafasi hiyo kuachwa wazi na aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Omari Ayoub aliyeondolewa ghalfa baada ya kukosa sifa kabla ya muda wake kuisha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Lyassa alitaja viapumbele vyake kuwa ni kupigania na kulinda haki za wafanyakazi.
Aliahidi kuondoa matatizo sugu kwa wafanyakazi ikiwemo ujira duni usioendana na hali ngumu ya maisha.
Kwa mujibu wa Lyassa, atahakikisha wazawa wanapewa fursa ya kufanya kazi nchini, ikiwemo kuomba sifa za elimu za wageni ili kubaini viwango vyao vya elimu iwapo hakuna Watanzania wenye sifa za kufanya kazi hiyo.
Aliahidi pia kulifufua gazeti la Mfanyakazi ndani ya siku 90 ili liwe sauti ya wafanyakazi bila kujali iwapo Tucta itakuwa na fedha au la kwa kuwa anao marafiki wenye uwezo watampatia fedha.
“Pia kama mwandishi wa habari nitahakikisha nafufua chama cha waandishi na kukifanya kiwe na nguvu kutokana na ukweli kwamba kati ya wafanyakazi wanaoonewa na kukosa pa kukimbilia ni waandishi,” alisema Lyassa.