jaridahuru

Mitandao

SIASA: JANUARY MAKAMBA ATANGAZA RASMI NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015, ASEMA NI MUDA WA VIJANA KUSHIKA DOLA


Licha ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwafungia kwa mwaka mmoja makada wake sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kugombea urais mwakani, mmoja wa makada hao,  Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amekiuka maagizo ya chama chake, kwa kutangaza kwamba ameshafanya maamuzi ya kuwania nafasi hiyo kwa asilimia 90.
Akizungumza katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London Uingereza juzi usiku, Makamba alisema tayari ameshachukua uamuzi huo, lakini kinachokisubiri kwa sasa ni ushauri wa mwisho kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na wakubwa wake.

Makamba amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa nakada wa CCM wanaotaka kuwania nafasi ya kusimamisha na CCM kupamabana na vyama vingine kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwakani.

Kiongozi huyo kutoka miongoni mwa makundi ya vijana wanaotaka kuwania urasi mwakani, hii ni mara yake ya  kwanza kutamka hadharani kuwa na nia ya kuwania urais, ingawa nyendo zake na kauli zake siku za nyuma zilikuwa
zikiashiria jambo hilo.

Nyendo hizo za Makamba na makada wengine watano waandamizi wa CCM wanadaiwa kufanya harakati za chini kwa chini kuwania urais kabla ya wakati, zilipelekea  Februari, mwaka huu, CCM kutoa onyo kali dhidi yao.

Makada wengine waliopewa onyo hilo na Kamati Kuu ya (CC) pamoja na Makamba, ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Mbali na kupewa onyo kali, makada hao pia walitakiwa kutojihusisha na kampeni au vitendo vyovyote  vinavyoashiria kampeni na watakuwa chini ya uangalizi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, baadhi ya wagombea hao wameendelea na kampeni za chini kwa chini ikiwamo kupigana vikumbo kwenye nyumba za ibada na kwa wananchi.

Akijibu swali la mtangazaji wa BBC Swahili, Salim Kikeke, anayeendesha kipindi cha Dira ya Dunia juzi aliyetaka kujua kama atawania urais mwakani, Makamba, alisema kwa asilimia 90 ameshafanya uamuzi wa kuwania nafasi hiyo na asilimia 10 iliyobaki anategemea uchaushi kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo viongozi wa dini na wakubwa zake.

“Wewe ni miongoni mwa vijana wanaotajwa kutaka kuwania urais uchaguzi mkuu ujao, nini maoni katika hili?” alihoji Kikeke.

Akijibu Makamba alisema: “Kuna masuala kadhaa ambayo lazima uyajibu mwenyewe ndani ya nafsi yako, nafasi yenyewe unaiweza? Pili una maarifa na fikra mpya za kuisogeza Tanzania na kuleta mabadiliko?

“Maswali hayo nimekuwa nikijiuliza na imefikia kipindi nimefanya uamuzi kuwa itakapofika wakati huo nitashiriki na hadi sasa kwa asilimia 90 nitajitokeza na asilimia 10 nategemea ushauri kutoka kwa makundi mbalimbali kama wazee, viongozi wa dini na wakubwa zangu,” alisema.

Pia, Kikeke alitaka kujua kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete anamaliza muda wake, je, Makamba anadhani atakuwa na sifa ya kuvaa viatu vyake?

Makamba alisema atakayekuwa na sifa ya kuvaa viatu vya Kikwete ni mwanachama wa CCM na ndani ya chama hicho kuna utaratibu wa namna ya kupata mgombea huyo na kwamba ipo hazina ya wananchama na viongozi ambao watakuwa na sifa.

Hata hivyo, alisema kila kipindi cha utawala kina changamoto zake na kwamba wakati wa utawala wa Rais Kikwete kuna changamoto za wakati huu ambazo anakabiliana nazo kuliongoza taifa na kwamba utawala ujao utakuwa na changamoto mpya zitakazohitaji nguvu na fikra za vijana kukabiliana nazo ili kwenda na matarajio ya wakati huo.

“Kizazi kipya (vijana) ndiyo wenye sifa ya kuchukua nafasi hiyo kwa kuwa kila kipindi kina mahitaji na changamoto zake, kwa kuwa miaka kumi ijayo itakuwa na changamoto na mahita mahususi, naamini aina ya uongozi unaohitajika baada ya Kikwete ni kizazi kipya ili kukabiliana na changamoto  ya karne ya 21,” alisema.

Mbunge huyo wa Bumbuli (CCM) kwa muda mrefu amekuwa akishawishi umri wa kugombea urais upunguzwe ili vijana nao wapate nafasi ya kuwania nafasi hiyo.

Makamba, kwa sasa ana umri wa miaka 40 kwani alizaliwa Januari 28, 1974.

Novemba mwaka jana, Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, alisema anatafakari kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2015 kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.

Kumekuwa na ‘utitiri’ wa wanachama wa CCM wanaojitokeza hadharani na kutangaza nia ya kuwania nafasi ya urais wa 2015.

NEC ya CCM ilishapiga marufuku wanachama wa chama hicho kutangaza nia ya kuutaka urais kwa maelezaoi kuwa, kufanya hivyo ni sawa na kufanya kampeni kabla ya wakati.

KATIBA MPYA
Makamba, pia alizungumzia mchakato wa kutengenza Katiba Mpya, ambao kwasasa umekwama katika Bunge la Maalum la Katiba baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia bunge hilo.

Alisema hadi sasa mchakato huo unaonekana kushindwa kufikia maridhiano na wanasiasa wameshindwa kuwapatia Watanzania Katiba wanayoitarajia.

Hata hivyo alishauri kwamba, kama mwafaka utashindwa kupatikana katika Bunge hilo kutokana na mivutano ya wanasiasa, mchakato huo usimamishwe na uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa kutumia Katiba ya sasa ya mwaka 1977.

“Kitakachohitajika kufanywa ni ni marekebisho tu kwenye katiba ya sasa hasa kwenye baadhi ya vifungu vitakavyowezesha uchaguzi huo kuwa huru na wa haki kama vile Tume ya Uchaguzi, nafasi ya mgombea binafsi na fursa ya kuhoji matokeo ya urais mahakamani.

“Vipengele vinavyolalamikiwa zaidi ni tume huru ya uchaguzi na mgombea huru, hivyo inapaswa kufanyiwa marekebisho hayo na kuendelea kutumika wakati maandalizi ya mchakato mwingine wa Katiba mpya yakiendelea,” alisema.

Alisema baada ya uchaguzi mchato huo urudishwe kwa wananchi kupitia kura ya maoni na kwamba wananchi wataulizwa maswali mawili la kama wanauhitaji Muungano na kama wanauhitaji uwe wa aina gani.

Alisema kura ya maoni ndiyo itakayokata mzizi wa fitina kwani baada ya hapo Bunge Maalum litaitishwa tena na kazi yake itakuwa ni kujadili yale tu yaliyoamuliwa na wananchi kupitia kura hiyo.


“Mapendekezo kama yalivyo sasa yakipitishwa basi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza isiwepo kama ilivyosasa, baadhi yetu tunaamini hili ni jambo kubwa na la msingi lingepelekwa kwa wananchi kwanza.”

“Kutokana na ukweli kuwa sisi wanasiasa tumekaribia kushindwa jinsi namna ya kukubaliana jinsi ya kuendelea mbele, tuwaulize wananchi kwenye kura ya maoni maswali mawili, Je kuwepo kwa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, la pili aina gani ya Muungano uwepo na wananchi watakapoamua  Bunge hilo lirudi na kuendelea kutengeneza Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.”

Makamba alikuwa Londoni kuhudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano juu ya namna mpya, maarifa mapya na teknolojia mpya za kuendesha mitandao ulioandaliwa na kampuni ya Macktech na Total Telecom ili kusaidia nchi katika sekta ya mawasiliano.

Imeandikwa na Abdallah Bawazir, Salome Kitomari na Sanula Athanas

Related

Siasa 7429906511342383509

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item