jaridahuru

Mitandao

KITAIFA: SUMAYE AONYA KUHUSU UDINI, AWAASA WATANZANIA WASIRUHU MTENGAMANO WA KIDINI

 



WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amewaasa Watanzania wajiepushe na chuki za kidini zinazotokana na imani za watu kwa kuwa ni hatari kwa taifa.

Sumaye, alitoa kauli hiyo jana mkoani Arusha katika Mkutano Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kusimamia vema waumini wao ili nchi isije ikakumbwa na balaa la vurugu za kidini.

Sumaye alisema vita vyote havina macho, lakini vita vya kidini ni vibaya zaidi na huishia kuuana bila kuwa na mshindi, hivyo ni vema chokochoko za hapa na pale zenye sura ya imani zinazotokea, zikatatuliwa mara moja.

“Upendo na uzalendo vimepungua na kuathiri umoja wetu. Tukiwa wamoja hili halina nafasi kwa sababu hakuna dini inayofundisha chuki kwa binadamu mwenzako. Ni lazima tukubali kuwa nchini mwetu kila mtu ana uhuru wa kuabudu dini aitakayo ilimradi havunji sheria za nchi,” alisema.

Sumaye alisema chuki nyingine inayolikabili taifa ni tofauti kubwa ya kimapato baina ya makundi tofauti, hasa kati ya matajiri wachache na wenye madaraka kwa upande mmoja na masikini walio wengi kwa upande wa pili.

Alisema jambo hilo limesababishwa na mfumo mbaya wa uchumi na ubinafsi uliokithiri, usiojali binadamu wengine, hali ambayo ni ya hatari kwa amani na utulivu wa taifa lolote, kwa kuwa walio wengi hawatavumilia kuona wachache wakiishi katika anasa za kutisha wakati wao wengi hawamudu chakula, matibabu na maji.

Sumaye alisema kuwa umoja ni muhimu kwa amani na utulivu, kwani pasipokuwa na umoja maendeleo huwa duni sana, jambo linalosababisha mtu kukosa moyo wa uzalendo wa kuipenda nchi yake na watu wake.

Alibainisha kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia bara la Afrika kutokuwa na maendeleo ni kukosekana kwa umoja.

Sumaye alisema Tanzania ina matatizo makubwa ya maadili kuanzia vijana hadi wakubwa, ambayo yanahitaji viongozi wa kiroho washiriki kikamilifu kuyatatua badala ya kuwangoja wahusika kwenye nyumba za ibada wanakokwenda kuabudu.

“Katika taifa letu ninyi ndio chumvi na taa ya nuru alizozisema Bwana Yesu. Kama jamii ikiharibika maana yake chumvi na taa hazijafanya kazi zao vizuri, tushirikiane sisi sote,” alisema.

Sumaye aliongeza kuwa umoja ni muhimu kwa nchi, kwa kuwa nchi zilizoukosa zimejikuta zikiingia kwenye migawanyiko na uvunjivu wa amani ikiwemo kupigana wenyewe kwa wenyewe.

Related

Kitaifa 6752026698296510503

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item