Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo Pinda
ameshauri Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Mwalimu Julius Nyerere,
maarufu kama Sabasaba, yasimamishwe angalau kwa mwaka mmoja kwa ajili ya
kurekebisha miundombinu ndani ya uwanja huo ili iendane na viwango
vinavyostahili.
Pinda alisema hayo jana alipotembelea maonyesho
hayo ya kila mwaka yanayoendelea kwenye uwanja huo kukagua mabanda
mbalimbali ya kampuni zinazotangaza biashara na taasisi binafsi na
serikali zinazotoa huduma mbalimbali.
“Nimemshauri Waziri wa Viwanda na Biashara kuwa
viwanja hivi vinahitaji marekebisho. Ongezeko la washiriki wa kimataifa
ambao nimeambiwa zimefikia kampuni 500 kutoka nchi 33, inadhihirisha
umuhimu na kukua kwa maonyesho yenyewe ambayo sasa nchi mbalimbali
zinayazingatia,” alisema Pinda.
“Ikibidi tupoteze fursa ya mwaka mmoja ili
tuboreshe viwanja hivi tulivyorithi na kuendelea kuvitumia kwa muda
mrefu vikiwa na miundombinu ileile. Yatupasa kuboresha kila kitu kwa
viwango vya kimataifa. Ukihudhuria maonyesho mengine ya kimataifa katika
nchi nyingine unaona tofauti ya ubora wa viwanja vyao ukilinganisha na
hivi vyetu… njia ni ndogo na hazijapangwa vizuri.”
Mbali na barabara za ndani ya uwanja huo kuwa
ndogo, mpangilio mbovu wa mabanda ya maonyesho, umeme kukatika mara kwa
mara, uchache wa maliwato na kutokuwapo kwa alama za kuongoza magari
yanapoingia hadi kutoka, vimekuwa ni vitu vinavyolalamikiwa sana na
washiriki wa maonyesho hayo makubwa kwenye ukanda wa mashariki ya
Afrika.
Waziri Mkuu alitembelea mabanda kadhaa na kujionea
shughuli zinazofanywa ambapo alivutiwa na ubora unaoonekana katika
bidhaa nyingi za kilimo na kupendekeza umakini kidogo uongezwe katika
ufungaji wa bidhaa hizo.
“Mnajua kuwa napenda sana asali. Kuna maendeleo
makubwa sana nimeyaona kutoka kwa wakulima waliopo kwenye banda la
asali… wamejitahidi kuongeza ubora na wanatia moyo kwa kuwa kila mmoja
anaweza akaliona hilo miongoni mwa bidhaa zilizopo,” alisema Waziri Mkuu
na kueleza kuwa changamoto aliyoiona katika vifungashio akiiomba
mamlaka husika kuwaongezea uwezo wafugaji wa nyuki.
Pinda aliitaka sekta binafsi kuisaidia Serikali
kuboresha huduma za kijamii hasa elimu ya juu baada ya juhudi za Kampuni
ya Global Education Link kumfahamisha wanavyoshughulika katika kupeleka
wanafunzi nje kufuata taratibu na sheria zilizopo ili wakanufaike na
kuja kulitumikia taifa baadaye.
“Juhudi za vijana kama hawa zinapaswa kupongezwa
na kuungwa mkono. Wazazi wengi wamekuwa wakipoteza fadha kusomesha
watoto wao nje na pale warejeapo wanakataliwa na bodi ya vyuo vikuu
lakini kwa namna hawa jamaa wanavyofanya kazi yao kwa uwazi na gharama
nafuu. Nashauri vijana wengi zaidi wajitokeze ili kupunguza urasimu
uliopo serikalini,” alisema Pinda.
“Hakuna taasisi ya serikali inayoweza kukuambia
kuwa wanatoa ufadhili kama hawa vijana. Sisi serikali zikiwepo nafasi
hizo ni mpaka mtu atafute taarifa, tena kwa shida ndipo azipate.”
Kwa jumla, Pinda alipongeza juhudi za Mamlaka ya
Maendeleo ya Biashara (TanTrade) kwa kuboresha na kuyatangaza maonyesho
hayo kimataifa kiasi cha kushawishi kampuni nyingi kutoka nchi tofauti
kuja kushiriki.
“Maonyesho kama haya yana nafasi nzuri ya
kuimarisha uchumi wa nchi kama kampuni ya ndani yatatumia ipasavyo fursa
waipatayo kujenga uhusiano mzuri na wenzao wa nje kwa kuwa itawasaidia
kujua mahitaji yaliyopo katika nchi mbalimbali waliko na washirika,”
alisema.