UTAFITI: MTANZANIA TOKA SUA AGUNDUA CHANJO YA NDUI YA KUKU

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/utafiti-mtanzania-toka-sua-agundua.html
Dar es Salaam. Tanzania imeingia katika vitabu vya kihistoria ya tiba baada ya Profesa Philemon Wambura kugundua chanjo ya ugonjwa wa ndui kwa kuku ambayo imetambuliwa kimataifa.
Chanjo hiyo iitwayo ‘Fowl Pox TPV-1 strain,’
iliyofanyiwa utafiti kwa miaka 10 na ya kwanza kugunduliwa duniani,
itaanza kutumika Afrika na dunia nzima hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano
na kampuni ya kimataifa inayotengeneza dawa na chanjo mbalimbali za
mifugo, MCI Sante Animale ya Morocco, Profesa Wambura alisema chanjo
hiyo ni ya kwanza kukubalika kutumika kuzuia ugonjwa wa ndui ya kuku na
ni rahisi kutumia ukilinganisha na chanjo nyingine zilizowahi kufanyiwa
majaribio.
“Ni fahari kwa Tanzania kuwa mgunduzi wa kwanza wa
chanjo hii duniani, ni chanjo yenye ubora wa hali ya juu na matumizi
yake yataongeza uzalishaji wa kuku na kuongeza kipato,” alisema Profesa
Wambura ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Tiba ya Wanyama wa Chuo cha Kilimo
Sokoine (SUA).
Profesa Wambura alisema tofauti na chanjo
nyingine, hiyo inaweza ikawekwa kwenye chakula au maji ya kunywa bila
kupata usumbufu wa kuwakamata mmoja mmoja na kuweka dawa machoni kama
ilivyozoeleka.
Alisema chanjo hiyo ina sifa kubwa ya kuvumilia
joto, jambo linaloifanya kuwa ni rafiki wa mazingira ya vijijini ambako
hakuna umeme na ina uwezo wa kutambua iwapo kuku ana virusi vya ugonjwa
wa ndui kwa kutumia damu ya kuku mwenyewe.
“Madhumuni yetu ni kuhakikisha chanjo hii
inapatikana kwa bei nafuu ili hata wananchi wa kawaida wanufaike. Ndiyo
maana itazalishwa kwa wingi ili iuzwe kwa bei nafuu,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia
(Costech), Dk Hassan Mshinda alisema ni fahari kubwa kuwa kazi ya
mtafiti wa Kitanzania imeonekana na mataifa ya nje, jambo ambalo linatoa
ari kwa watafiti wengine kufanya kazi zaidi.
Alisema mradi huo wa chanjo ya ndui ya kuku
uliogharimu Sh205 milioni ni wa kimataifa na chanjo hiyo itasambazwa
duniani kote kwa ushirikiano wa Costech na Kampuni ya MCI.
“Ni vizuri sasa tafiti za Kitanzania zinatumika
badala ya kuhifadhiwa kwenye makabrasha bila faida yoyote. Ni kazi ya
kujivunia hasa,” alisema
Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji wa Biashara wa
MCI, Dk Baptiste Dungu alisema kampuni yake imefanya kazi na Profesa
Wambura na kugundua kuwa utafiti wa chanjo yake una manufaa makubwa kwa
sababu ni wa kwanza duniani.