UJUMBE: MSANII WA MAIGIZO 'BONGO MOVIE' AANDIKA UJUMBE MZITO WA MAJONZI KWA KIFO CHA MZEE SMALL

Mzee Jongo, 'Kamanda' Mzee Pwagu, Mzee Hmisi Tjiri, Mzee Majengo, Mzee Mkombora, Mzee Halikuniki, Mama Haambiliki, Bibi Nyakomba, Bibi Hindu, Bi' Chau, Mzee Small, Tupa Tupa, Mzee 'King' Majuto, Mwalimu Kassimu El Siagi, Mzee Amry Bawji, Pembe na wengineo, ni wasanii walioitoa sanaa ya maigizo katika wakati mgumu sana.
Wakati uliokuwa na stesheni za runinga kama nne hivi na stesheni mbili za Radio. Wakati uliokosa mitandao ya kijamii, wakati uliokosa kuthamini sanaa kama bidhaa ifaayo kununuliwa ama ajira ya kuheshimika.
Licha ya yote hayo, ndugu hawa walikuwa madhubuti kufanya kile walichokuwa wakikipenda na kukiamini zaidi yaani sanaa yao.
Mapenzi na bidii yao katika sanaa ndiyo ilituvuta wengi tuliomo katika uga huu wa sanaa ya maigizo kwa lugha adhimu ya Kiswahili.
Hivyo, akiondoka mmoja wa manguli hawa ni sawasawa na jabali kupiga chini na kuacha tetemo kuu. Nakutakia makazi mema Small Ngamba pamoja na wenzako wote waliotangulia mbele ya haki. Mlitayarisha chungu lakini hamkufaidi ugali.
Hamkuwa wabinafsi. Mmeacha watoto na wajukuu zenu wakifaidi msingi imara mlioujenga. Ninyi ni mashujaa.
By: Rutakirwa Kasiga. (BonFide Films)