MATUKIO: WANANCHI WAVUNJA MOCHUARI KUTAKA KUONA MAITI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/matukio-wananchi-wavunja-mochuari.html
Muleba. Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya baadhi ya wanakijiji wa Bukono, Kata ya Muleba, mkoani Kagera ambao walivunja mlango wa chumba cha kuhifadhi maiti Kituo cha Afya Kaigara, wakitaka kuchukua maiti ya mtoto aliyefariki dunia mkoani Arusha alikokuwa akifanya kazi za ndani.
Mtoto huyo Asela Triphone (16) alikuwa akifanya kazi za ndani kwa mwanamke mmoja aliyemchukua kutoka kwa wazazi wake.
Wanakijiji hao walichukua hatua hiyo, wakidai
mwili uliokuwa kwenye jeneza ulikuwa umenyofolewa baadhi ya viungo vya
mwili; sehemu za siri, mkono na mguu ikidaiwa kuwa vilichukuliwa kwa
ajili ya imani za kishirikina.
Inadaiwa kuwa baada ya kufika Arusha, Asela
alianza kufanya kazi za ndani na alifariki dunia katika mazingira ya
kutatanisha na mwili wake ulirejeshwa juzi kwa wazazi wake.
Akisimulia tukio hilo, mama wa marehemu, Georgina
Triphone alisema aliombwa mtoto wake kwenda kufanya kazi za ndani
Januari mwaka jana na kwamba, alikuwa akipata mawasiliano ya simu kutoka
kwa mwajiri wake.
“Tangu Alhamisi (Juni 12, mwaka huu), nimekuwa
nikipokea simu tofautitofauti kuhusu binti yangu kupitia kwa mwajiri
wake kuwa, atakuja karibuni kusalimia,” alisema na kuongeza: “Ijumaa
(Juni 13 mwaka huu), nilipigiwa simu na mwajiri wa binti yangu kuwa,
angekuja kuwatembelea lakini kesho yake alinitaarifu kuwa ni mgonjwa na
Jumapili nikaletewa maiti ya binti yangu.”
Alisema yeye na mumewe walianza kujawa na wasiwasi
juu ya binti yao na jeneza lilipowasili walitaka kulifungua lakini
walikatazwa na aliyefika na maiti hiyo kwa madai kuwa mwili ulikuwa
umeharibika.
“Tulipokuwa tunalazimisha kuona mwili tuliambiwa
ugonjwa uliosababisha kifo chake unaambukiza, hivyo ungeweza kuwaathiri
wananchi waliokuwapo.”
Hata hivyo, baba wa marehemu Triphone Basheka
alisema mwili huo ulikuwa umeunguzwa sehemu mbalimbali na kwamba,
wananchi walitaka kujua ukweli huo baada ya kukosa ushirikiano wa
madaktari na vyombo vya dola ikiwamo Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya.
Hatua hiyo iliwakera wananchi ambao walianza
vurugu, hali iliyosababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya
huku baadhi yao wakikamatwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lambris
Kipuyo alikanusha taarifa ya kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama haikutoa
ushirikiano na kukemea tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Kipuyo alisema kwa mujibu wa uchunguzi, viungo
vinavyodaiwa kunyofolewa vilikuwapo na kilichosababisha utata ni
kukosekana kwa meno manne na mwili kuwa na makovu mbalimbali.