MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana Ijumaa Juni 6, 2014 imetupilia
mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS) dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG).
Katika kesi hiyo ambayo walalamikaji walidai ya kuwa Pinda alivunja
Katiba kwa kauli aliyoitoa bungeni, Juni 20, 2013, wakidai kauli yake
ilikua ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa Sheria kuwapiga wananchi,
wakati wa vurugu.
Kauli hiyo ya Pinda ni ile aliyoitoa bungeni alipovitaka Vyombo vya
Dola kuwapiga wale wote wanaokaidi amri za vyombo hivyo, kwa madai kuwa
serikali imeshachoshwa na vitendo vya baadhi ya wananchi wanaokaidi kwa
makusudi amri za vyombo vya dola (hususan Jeshi la Polisi).
Uamuzi huo ulitolewa jana Ijumaa Juni 6, 2014 mahakamani hapo na jopo la
Majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Kiongozi
Fakihi Jundu akisaidiana na Dk Fauz Twaib na Augustine Mwarija wakati
wakitoa uamuzi wa Pingamizi la awali lililowasilishwa na AG.
Uamuzi Mahakama hiyo umetokana na pingamizi lililowekwa na Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu, aliyewasilisha hoja tano.
Akisoma uamuzi wa pingamizi hilo, Jaji Jundu alisema kwamba Mahakama
hiyo imekubaliana na hoja ya AG kwamba walalamikaji katika kesi hiyo
hawakuwa na mamlaka kisheria ya kufungua kesi hiyo kulingana na ibara ya
100 (1) ya katiba ya nchi.
Ibara hiyo inasema "Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na
utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali
penginepo nje ya Bunge".
Hata hivyo Jaji Jundu alisema ibara ya 100 (2) ya Katiba hiyo
inayosema: "Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine
yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la
madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani
ya Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au
vinginevyo."
Katika hatua nyingine, Jaji Jundu alisema kwamba LHRC na TLS hawakuwa
na mamlaka ya kufungua shauri hilo kulingana na Kanuni ya 71 (1) ya
Bunge ambayo inamtaka mtu binafsi aliyeathirika na kauli yoyote
iliyotolewa bungeni kuwasilisha malalamiko yake Kwa Spika na si taasisi
kufungua kesi kama walivyofanya wao.
Alisema kwamba kama kauli aliyoitioa Pinda ingeathiri taasisi hizo
moja kwa moja, basi wangeweza kuwasilisha malalamiko yao kama taasisi na
si kwa niaba ya kundi fulani.
Kanuni hiyo inasema: 'Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 na 101
ya Katiba, mtu yeyote asiye Mbunge ambaye atajisikia kuwa amepata athari
hasi kutokana na kauli au maneno au shutuma zilizotolewa bungeni
kumhusu yeye binafsi, anaweza kupeleka malalamiko pamoja na maelezo yake
ya kujitetea kwa Spika.”
Jaji Jundu alisema kwamba Mahakama hiyo inaitupa kesi hiyo bila gharama kutokana na uhalisia wa kesi yenyewe.
Baada ya hukumu hiyo, nje ya Mahakama, wadai katika kesi hiyo, akiwemo
Frugecy Masawe, Harold Sungusia, Peter Kibatala na wegine, walisema
kwamba wiki ijayo jopo la mawakili katika kesi hiyo watakutana kujadili
hatua za kuchukua baada ya kupata nakala ya uamuzi huo.
Katika kesi hiyo Namba 24 ya mwaka 2013, pamoja na mambo mengine,
walalamikajikatika kesi hiyo (LHRC na TLS) waliiomba Mahakama itamke
kuwa kauli ya Pinda ilikwenda kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda
aifute hadharani.
Hata hivyo, walalamikiwa kupitia jopo la mawakili wanne wa Serikali,
likiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG), George Masaju,
waliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo.
Katika pingamizi hilo walalamikiwa wanadai kuwa kesi hiyo ni batili na
iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge ya
mwaka 1988
Mawakili hao wanadai kuwa Pinda analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na
(2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au kufunguliwa shauri la madai
mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, alilolitenda au
aliloliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada au hoja.
Upande wa walalamikaji ukiwakilishwa na mawakili Harold Sungusia na
Fulgence Massawe (LHRC), Mpale Mpoki, Peter Kibatala na Jeremiah
Mtobesya (TLS), katika majibu yao walidai kwamba walalamikaji wana haki
ya kushtaki. Aidha, walidai kwamba kinga ya mbunge ina mpaka na
inalindwa kwa shughuli za Bunge pekee, huku wakidai kuwa hati hiyo haina
dosari na kwamba hata kama zipo dosari za kisheria, zinaweza
kurekebishwa.