JAMII: MWANAUME AJINYONGA KWA AJILI YA BAJETI, ADAIWA KULIPA KODI ZAIDI YA KIPATO

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/jamii-mwanaume-ajinyonga-kwa-ajili-ya.html
Wakati Bunge likiendelea kujadili Bajeti ya serikali huko Dodoma, Geofrey Ndibalema (41), mkazi wa Tandika jijini Dar amedaiwa kujinyonga kwa kukosa kodi ya chumba.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Juni 14, mwaka huu katika nyumba
aliyopanga marehemu ambapo ilidaiwa kuwa siku moja kabla ya tukio, baba
mwenye nyumba alimpigia simu kumkumbushia akaahidi kulipa siku
iliyofuata ambayo ndiyo alikutwa amejinyonga.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa marehemu aliyeomba hifadhi ya jina
lake, alisema Geofrey aliamka asubuhi akiwa mzima wa afya na kwenda
kuchota maji ya kuoga ili aelekee kwenye shughuli zake za upambaji
ambapo ilidaiwa kuwa alipewa tenda ya kupamba katika harusi na tayari
alishachukua nusu ya malipo.
Marehemu Geofrey Ndibalema (41), mkazi wa Tandika jijini Dar aliyejinyonga kwa kukosa kodi ya chumba.
Ndugu huyo wa marehemu alidai, wakati Geofrey anarudi kuchota maji,
alimkuta mwenye nyumba akiwa anamsubiri ili alipe kodi yake jambo
lililodaiwa kumpa hofu marehemu na kuingia ndani ya chumba chake na
kujinyonga.
“Mwenye nyumba alibaki anasubiri alipwe kodi kwa kuwa alijua Geofrey
aliingia chumbani kwake kwa ajili ya kuchukua hela hiyo lakini muda
mrefu ulipita bila kutoka nje kiasi cha mwenye nyumba kuanza kupata
wasiwasi lakini aliamua kumuacha na kuondoka,” alisema ndugu huyo.
Ndugu huyo alizidi kueleza kuwa, baada ya muda rafiki wa marehemu
aitwaye Dickson aliyekuwa akiishi naye chumba kimoja ndiye aliyegundua
mwenzake alikuwa amejinyonga.
“Rafiki yake aligonga sana mlango bila mafanikio ndipo
alikwenda dirishani na kuendelea kuita bila mafanikio, lakini
alipochungulia alimuona Geofrey akiwa ananing’inia ndipo alipotutaarifu
tukaja,” alisema ndugu huyo.
Ndugu huyo alisema baada ya taratibu za kipolisi kukamilika,
walimsafirisha marehemu mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi huku
ikielezwa baba mwenye nyumba na wanakamati wa harusi waliompa tenda
marehemu wamesamehe madeni yao.
CREDIT:GPL