BUNGENI: WABUNGE WA CHADEMA WAUMBUANA BUNGENI, MDEE AIGONGEA PASI CCM

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-wabunge-wa-chadema-waumbuana.html
Dodoma. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amemshukia Leticia Nyerere (Viti Maalumu-Chadema) kwa kumtaka aende CCM kwa sababu bado Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ana nafasi za kuteuwa wabunge. Hadi sasa Rais Kikwete ameshateua wabunge wanane kati ya nafasi 10 alizopewa kikatiba.
Mdee aliyasema hayo jana alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/2015.
Alisema Kambi ya Upinzani Bungeni haiko kwa ajili
ya kuisifia Serikali bali ni kuikosoa na kutoa mawazo mbadala. Mdee
alisema wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka minne na mawazo mengine
yalishachukuliwa na kufanyiwa kazi na Serikali likiwamo la kupunguza
kodi ya mishahara.
“Jambo la Serikali kutoa huduma kwa wananchi ni la
lazima na siyo hiyari, fedha hazitoki mifukoni mwenu (wabunge wa CCM),
zinatoka kwenye kodi ya wananchi,” alisema Mdee.
Alisema kama Leticia anataka kwenda CCM badala ya
kudhalilisha upinzani ambao unafanya kazi usiku na mchana, aachie ubunge
ili Rais Kikwete amteue.
“Atuulize sisi, watu waliokuwa wanajipendekeza CCM walifikia wapi, wamepigika huko,” alisema Mdee.
Akichangia katika mjadala huo juzi, Leticia
aliisifia Serikali kwa kupeleka maendeleo katika Jimbo la Kwimba.
“Naishukuru Serikali yangu kwa kupeleka maji katika jimbo langu la
Kwimba,” alisema Leticia.