BUNGENI: MBUNGE APOKEA MSHAHARA WA TSH 50,000/- ALALAMIKIA MAKATO YA MKOPO

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-mbunge-apokea-mshahara-wa-tsh.html
WAKATI baadhi ya watu wakiamini wabunge hulipwa zaidi ya sh milioni
10 kwa mwezi, mmoja wa wabunge wa Bunge la Muungano, amejikuta akitoka
na mshahara wa sh 50,000 kwa mwezi,
Tanzania Daima limebaini.
Mbunge huyo ambaye jina limehifadhiwa, amejikuta akiambulia kiasi
hicho cha fedha kutokana na makato makubwa ya marejesho ya mkopo wa
Bunge wa zaidi ya sh milioni 300 aliouchukua baada ya kuingia bungeni.
Mbali ya mbunge huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni,
inaelezwa kuna wabunge wengine wengi wanakabiliwa na tatizo hilo la
kuambulia mishahara kiduchu kutokana na makato ya mikopo na kodi.
Akizungumza na gazeti hili, mbunge huyo kutoka Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ambaye alisisitiza jina lake lihifadhiwe, alisema yeye pamoja na
wabunge wengine wengi, wanakabiliwa na tatizo la makato makubwa ya
madeni waliyokopa na watakuwa wakilipwa kiasi hicho kwa muda wote wa
Bunge.
“Karatasi yangu ya mshahara kila mwezi inaonyesha napata sh 50,000 tu
na huo ndio ukweli maana nilikopa nikajengea nyumba zangu tano za
nguvu, najua hata nikikosa ubunge mwakani, maisha yangu yataenda vizuri,
lakini wapo waliokopa kwenda kutekeleza ahadi walizozitoa majimboni,
hao wasiporudi bungeni wamekwisha,” alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wapiga vijembe wakubwa dhidi ya wenzao
wa upinzani, alisema maisha yake ya ubunge kwa kiasi kikubwa
yanategemea zaidi posho za vikao, ambavyo kwa mwaka huu vimekuwa
mfululizo, vikiwemo vikao vya Bunge la Katiba.
Alisema anaomba ratiba ya vikao vya Bunge la Muungano linarotarajia
kuanza tena Julai baada ya Bunge la Bajeti linaloendelea kumalizika,
isibadilike ili aendelee kupata posho ya sh 300,000 kila siku.
Bunge la Julai
Hata hivyo, matumaini ya wabunge kuunganisha vikao vya Bunge la
Bajeti linalomaliza vikao vyake Julai mosi na jingine lililotarajia
kufanyika Julai, yameanza kufifia.
Awali kulikuwa na taarifa zilisema kuwa baada ya kumalizika kwa
mkutano wa Bunge la Bajeti linaloendelea, wabunge hao wangepumzika kwa
wiki moja kisha kuanza tena vikao vya kamati na kurejea tena bungeni
Julai.
Kufifia kwa matumaini hayo kunatokana na taarifa ilizozipata gazeti
hili kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi katika kikao
walichoketi wiki iliyopita, hawakufikia muafaka juu ya pendekezo la
kuwepo kwa mkutano mwingine wa 16 wa Bunge ifikapo Julai.
Tanzania Daima, limedokezwa kuwa baadhi ya wajumbe walisema ratiba
hiyo itawafanya wachoke zaidi kwani kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti
walikuwa wakishiriki kwenye Bunge la Katiba ambalo liliahirishwa
mwishoni mwa mwezi wa nne.
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge la Katiba, wabunge walipumzika kwa
takriban wiki moja na kuanza vikao vya kamati za Bunge na baadaye
kuingia kwenye Bunge la Bajeti ambalo wakimaliza watajiandaa kushiriki
lile la katiba litakaloanza Agosti 5.
Awali baada ya taarifa za kuwepo kwa Bunge jingine Julai kabla ya
lile la katiba, baadhi ya wabunge walionekana kuzifurahia wakidai
litawasaidia kupata posho zitakazopunguza ukali wa maisha.
Baadhi ya wabunge wamekwa na kilio cha mara kwa mara kuwa fedha
wanazolipwa haziwatoshi kutokana na mikopo mingi waliyonayo na upandaji
wa gharama za maisha.
Akizungumza na Tanzania Daima, Kaimu Katibu wa Bunge John Joel,
alisema hadi sasa bado Bunge halijaamua uwepo wa Bunge la Julai kama
baadhi ya watu wanavyotoa taarifa.
Alisema kama jambo hilo litaridhiwa na vikao husika Bunge litauarifu umma.
Bunge la Julai litakuwa kwa ajili ya kujadili miswada mbalimbali ya
sheria iliyowasilishwa bungeni, ambayo haitaweza kujadiliwa katika Bunge
la Bajeti.
Itakumbukwa kuwa Bunge la Muungano lilikutana Desemba mwaka jana,
badala ya Januari kama ilivyo kawaida kupisha ratiba ya Bunge la Katiba.
Baada ya Desemba, wabunge walipumzika kwa mwezi mmoja na kurudi tena
bungeni Februari kwa ajili ya Bunge la Katiba ambalo lilikaa kwa siku 67
hadi Aprili ambapo walipumzika kwa wiki moja na kurudi kwenye Bunge la
Bajeti Mei 6, mwaka huu.