BUNGENI: MAWAZIRI SABA WANAOPUMULIA MIRIJA HAWA HAPA, BAJETI ZA WIZARA ZAO ZAPITA KWA MBINDE

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-mawaziri-saba-wanaopumulia.html
Msuguano mkali umekuwa wakati Bunge linapokaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti za wizara husika. Hata hivyo, bajeti hizo zimepitishwa baada ya maelezo marefu na wakati mwingine msaada wa kiti cha Spika au pale Waziri Mkuu au Kaimu wake ndani ya Bunge anaposimama ‘kuokoa jahazi’.
Mawaziri ambao hadi sasa wameingia katika orodha
ya bajeti zao kupita kwa mbinde na wizara zao kwenye mabano ni Profesa
Jumanne Maghembe (Maji), Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi), Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Dk
John Magufuli (Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Sophia Simba
(Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Dk Seif Rashid
(Afya na Ustawi wa Jamii).
Sababu za kasheshe
Kwa sehemu kubwa, bajeti nyingi zilipata upinzani
kutokana na Hazina kutoa fedha kidogo za maendeleo kati ya asilimia 19
na 30 tu, wakati wizara nyingine zilitikiswa na tuhuma za ufisadi wa
watendaji wake.
Sophia Simba
Miongoni mwa mivutano ni ule uliohusu taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (Wama) ambayo Mwenyekiti wake ni mke wa Rais
Jakaya Kikwete, Mama Salma, hoja iliyoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti
ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed alitaka
taasisi hiyo ifutwe, kwa maelezo kwamba inajihusisha na masuala ya
kisiasa na kwamba mwaka 2010, Mama Salma aliitumia kumfanyia kampeni
mumewe.
Katika hoja hiyo alisema mmoja wa wajumbe wa bodi
ya taasisi hiyo ni Waziri wa wizara hiyo, Sophia Simba kinyume na sheria
na taratibu.
Waziri Simba akajibu: “Nipo Wama lakini kazi
ninayoifanya pale ni ya kujitolea na silipwi kitu. Kanuni na sheria
zinakataza mtu kujihusisha na taasisi nyingine kama tu anakuwa analipwa
mshahara”.
Profesa Maghembe
Juzi, Profesa Maghembe alipata wakati mgumu baada
ya hoja iliyoshika mshahara wake iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika kujadiliwa kwa dakika 31, hadi Kaimu Waziri Mkuu,
Profesa Mark Mwandosya alipoingilia kati.
Wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao, waliungana kutetea
hoja ya kutaka suala la upatikanaji wa maji liwe ajenda ya kwanza ya
Serikali. mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul alitaka bajeti
hiyo ifumuliwe ili kuondoa posho za vikao na safari.
Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu alisema tatizo la maji ni zito na akapendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa maji.
Profesa Mwandosya alisimama na kutoa uthibitisho
kwa niaba ya Serikali kwamba muswada huo wa fedha utapelekwa bungeni
kabla ya kuvunjwa kwa Bunge 2015 na alikubaliana na wabunge kwamba suala
la maji litakuwa ni nambari moja katika vipaumbele vya Serikali.
Dk Magufuli
Kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli kwamba
ujenzi wa barabara si sawa na chapati, ilisababisha baadhi ya wabunge
kumjia juu wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara yake.
Baadhi ya wabunge wa mikoa ya kusini mwa nchi,
walichachamaa kutokana kile walichodai kuwa ni kutotengwa kwa fedha za
ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
Suala jingine lililotawala mjadala huo ni sakata
la malori kuruhusiwa kuzidisha uzito barabarani, hoja ambayo iliibuliwa
na Machali ambaye alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwaomba radhi
Watanzania kutokana na hatua yake ya kuyaruhusu kubeba mizigo mizito na
kusababisha barabara zinazojengwa kwa mamilioni ya fedha za kodi za
wananchi kuharibika. Pinda alitoa ufafanuzi mzuri.
Dk Mwakyembe
Wabunge walitaka maelezo ya kina juu ya
uendeleshaji Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), Shirika la Ndege
(ATCL), ukarabati wa meli ya MV Victoria na upanuzi uwanja wa ndege
Mwanza.
Wabunge waliokuwa vinara wa kupinga bajeti hiyo
wakitaka mambo hayo manne kupatiwa ufumbuzi ni wabunge wa CCM, Dk Hamisi
Kigwangalla (Nzega), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Charles Mwijage
(Muleba Kaskazini), Richard Ndassa(Sumve) na mbunge wa Ilemela
(Chadema), Ezekiah Wenje.
Profesa Muhongo
Ni kati ya bajeti ambazo zilipita kwa mbinde huku wabunge wakiibua hoja na ufisadi mbalimbali uliofanywa ndani ya wizara hiyo.
Sakata la IPTL ni moja kati ya mambo yaliyotikisa mjadala wa
bajeti hiyo huku Mnyika na mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole
Sendeka wakiwasilisha ushahidi kuhusu tuhuma kadhaa za wizara hiyo.
Mashambulizi hayo yaliibua tuhuma mpya dhidi ya
wabunge, Profesa Muhongo alipodai kwamba baadhi ya wabunge wakiwamo wa
upinzani wamehongwa na IPTL.
Katika maelezo yake, Profesa Muhongo alisema ana
ushahidi wa kamera za CCTV zinazowaonyesha vigogo hao wa upinzani
wakisaini nyaraka na kuchukua fedha hizo.
Sakata jingine lililoibuka ni kukosekana kwa umeme
katika maeneo ya vijijini na kulazimika Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kutoa ufafanuzi akisema kuwa fedha zitakazotengwa kwa ajili ya Mfuko wa
Nishati Vijijini (Rea) hazitaguswa.
Profesa Tibaijuka
Waziri Tibaijuka alijikuta katika wakati mgumu
baada ya wabunge, wengi wa Dar es Salaam kumbana kuhusu ujenzi wa mji
mpya wa Kigamboni.
Suala hilo lililohusishwa na ufisadi lilionekana
kumchanganya waziri huyo na wakati mwingine alishindwa kujibu maswali na
badala yake kuwashambulia wabunge wa upinzani hasa Halima Mdee wa
Chadema.
Alisema wapo wabunge ambao walikuwa na hoja na
wengine walikuwa wakipiga kelele, akitoa mfano tuhuma dhidi yake kuwa
anamiliki kiwanja katika Mji wa Kigamboni kwamba hazina ukweli wowote.
Dk Seif Rashid
Nayo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikumbwa
na dhoruba jana kabla ya kuokolewa na Profesa Mwandosya baada ya wabunge
wengi hususan wanawake, kutaka kuikwamisha.
Chanzo:Mwananchi