https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/afya-kashfa-nzito-yaikabili-sekta-ya.html
Maisha ya baadhi ya watu wanaotumia dawa za kufubaza makali ya
ugonjwa wa Ukimwi (ARVs), yapo hatarini, baada ya kupungua kwa dawa hizo
nchini na hivyo kufanya wagonjwa kutumia dawa tofauti na zile
wanazotumia siku zote.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa hali hiyo
inatokana na urasimu wa baadhi ya taasisi za Serikali, ambazo
zinachelewa kuagiza dawa za ARVs kwenye viwanda vya nje ya nchi.
Tayari Mfuko wa Kimataifa unaoshughulikia Ugonjwa
wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria wa Global Fund, Shirika lisilo la
Serikali linalojihusisha na masuala ya afya (Sikika) na watumiaji wa ARV
nchini wamethibitisha kuwapo kwa upungufu huo na hatari zake kiafya kwa
wagonjwa.
Global Fund katika ripoti yake ya robo ya mwaka
huu (Januari- Machi), imekiri kuwapo kwa upungufu wa dawa za ARV nchini
na athari ambazo wameanza kupata wagonjwa.
Ripoti hiyo inaonyesha upungufu huo wa dawa za ARV
unatokana na uzembe wa baadhi ya taasisi za Serikali kuchelewa kuagiza
dawa hizo pamoja na kuwapo kwa mabadiliko katika ununuaji na
ucheleweshwaji wa kupatikana fedha za kununulia ambao umesababisha
upungufu huo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa waathirika wakuu katika
upungufu huo wa dawa ni wanawake wajawazito wanaoishi na virusi vya
Ukimwi, ambao wanatakiwa kutumia ARV aina ya TLE ili kuzuia maambukizi
ya mama kwenda kwa mtoto.
Upungufu huo, umesababisha wagonjwa kubadilishiwa
dawa tofauti na zile wanazotumia hali ambayo imesababisha baadhi yao
kinga ya mwili (CD4) kushuka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi
ya mikoa nchini unaonyesha tatizo hilo la kupungua kwa ARVs nchini,
limewaumiza wagonjwa wengi na kwamba sasa wanapokwenda hospitali
wanapewa dawa za kutumia wiki mbili au vidonge 10 badala ya dawa za
mwezi mmoja au miwili.
Sikika
Shirika lisilo la Kiserikali (Sikika),
linalojihusisha na masula ya afya, wamebaini kuwapo kwa upungufu wa dawa
za ARV katika mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro, Tabora, Shinyanga,
Morogoro, na Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria alimwambia
mwandishi wa gazeti hili kuwa taarifa walizozipata kutoka kwa watu
wanaotumia ARV, upungufu mkubwa wa dawa hizo kwa Mkoa wa Dar es Salaam
upo katika katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Mwananyamala, Amana na
Temeke.
Katika hospitali hizo wagonjwa wanabadilishiwa dawa za ARV na kupewa tofauti na zile ambazo wamezoea kuzitumia.
“Taarifa tulizopata Machi mwaka huu, ni kwamba tatizo hilo bado
lipo na wagonjwa wanaendelea kupewa dawa pungufu, mfano badala ya kupewa
za mwezi mara nyingine walikuwa wanapewa za wiki au kubadilishiwa dawa
bila kupewa maelezo ya mabadiliko hayo,” anasema Kiria.
Kiria aliiomba Wizara ya Afya itoe tamko rasmi
kuwaeleza wananchi hali halisi ya dawa za ARV, ili kuepusha hali ya
wasiwasi na madhara ya kisaikolojia wanayoyapata wagonjwa hivi sasa.
“Ni haki ya kila mwananchi kupata taarifa sahihi
ambazo zinahusu afya yake, ili naye aweze kutimiza wajibu wake wa
kuilinda afya yake na za wenzake,” anasema Kiria.
Kiria anaishauri Serikali kutenga bajeti kwa ajili
ya shughuli za dharura pale ambapo itatokea, huku akiitaka kupunguza
utegemezi.
Anasema taarifa ya matumizi ya Serikali ya ugonjwa
wa Ukimwi mwaka 2011 na Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukimwi
(NMSF III) wa mwaka 2013/14 – 2017/18 unaonyesha kuwa bajeti hiyo
imekuwa ikipungua na kwamba utegemezi wa wafadhili ni zaidi ya asilimia
97.
Naibu Waziri
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Kebwe Steven, anasema kuwa licha ya kutegemea ufadhili, lakini Serikali
ina fedha kwa ajili ya kununua dawa ndani na nje ya nchi kama itatokea
kutakuwa na dharura.
Anasema kuwa hafahamu kuhusu kuwapo kwa upungufu,
anachofahamu ni kuchelewa kufika kwa dawa kutokana na taratibu za
uagizaji, kwani Global Fund ambayo ndiyo inayoagiza dawa hizo husambaza
kwa nchi nyingi.
Anasema kuwa anadhani hilo ndilo tatizo lililosababisha kupungua kwa dawa hizo nchini.
Naibu waziri huyo anasema pamoja na Global Fund
kutoa dawa hizo nchini, lakini Serikali wamekuwa wakichangia kiasi
katika kuziingiza dawa hizo.
“Siyo kwamba hatuchangii kabisa, kuna vitu ambavyo
tunafanya ikiwamo gharama za kutoa dawa hizo bandarini, hatuwezi
kumwachia jirani atujengee nyumba,” anasema Kebwe.