JAMII: DADA ALIYEFARIKI NA KUZIKWA AIBUKIA NYUMBANI KWAO AKIWA MZIMA, WAZAZI NA NDUGU WACHANGANYIKIWA
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/jamii-dada-aliyefariki-na-kuzikwa.html
HOFU ya ushirikina imetikisa Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la
hivi karibuni ambapo mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta jiji hapa, Witness
Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12, mwaka huu na kuzikwa kwenye
makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, Kata ya Moshono wilayani
Arumeru, Arusha kuibuka akiwa hai.
Binti huyo aliibuka kwao hivi karibuni akiwa mpole na kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wazazi wake kutimua mbio kwa hofu.
Watu kutoka maeneo
mbalimbali jijini hapa wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa
wazazi wa binti huyo kwa lengo la kumshuhudia kwa vile ndugu
walishaamini kuwa, mpendwa wao huyo alishakufa na alizikwa.
UWAZI LATIA TIMU NYUMBANI
Baada ya kusikia taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari mpaka eneo
la tukio na kumshuhudia binti huyo kisha likaenda kwenye kaburi
alilozikwa.
Kwenye kaburi hilo, msalaba wenye kuonesha siku yake ya
kuzaliwa (1992) na kufa (12, Aprili, 2014) ulikuwa bado umesimama imara
huku kaburi lenyewe likionesha dalili ya kutitia kidogo.
BABA MZAZI ASIMULIA
Akisimulia mkasa huo kwa mshangao mkubwa, baba mzazi wa binti huyo, Obed Leiyo alisema:
“Ilikuwa Aprili mwanzoni, binti yangu alitoweka nyumbani baada ya kurudi kutoka chuoni majira ya saa 2 usiku akiwa amechelewa.
Mimi kama mzazi nilimfokea kwa kuchelewa kwake kurudi nyumbani.
“Yeye kwa hasira zake alizunguka nyumba akaondoka muda huohuo na hakurudi kabisa hapa nyumbani.
“Siku iliyofuata tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila
mafanikio, tukatoa matangazo kwenye vyombo vya habari lakini binti yangu
hakuonekana.”
TAARIFA ZAFIKA, KAFA
Mzazi huyo aliendelea kusema: “Siku moja tulipata taarifa kwamba
kuna mwili wa msichana umeonekana katika Kijiji cha Bwawani hapahapa
Arumeru.
“Mimi pamoja na ndugu wengine tuliamua kwenda katika kile
kijiji. Tulipofika tuliambiwa ni kweli mwili wa msichana uliokotwa
lakini wananchi wakauzika.”
WAFUKUA KABURI
Baba huyo anaendelea: “Niliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Usa
River ambako niliomba kibali kwa ajili ya kufukua kaburi na kuutoa mwili
ili kuutambua kama ni binti yangu au la!
“Nilipewa kibali, tukafukua kaburi na kutoa mwili.
Nilimtambua kuwa ni binti yangu kutokana na alama mbalimbali alizokuwa
nazo, ikiwemo rangi kwenye kucha na sehemu ya kushoto ya uso ilikuwa
nyeusi kwa sababu aliwahi kupooza.
MWILI WASAFIRISHWA, WAZIKWA
Baba huyo wa Witness alizidi kueleza kuwa waliusafirisha mwili
huo hadi nyumbani kwake Moshono na kuandaa taratibu za mazishi ambapo
Aprili 23, mwaka huu mwili ulizikwa.
AIBUKA GHAFLA
Hata hivyo, Obed anasema alishangaa siku ya tukio kumwona binti
yake huyo akiibuka nyumbani hapo akiwa hai jambo ambalo lilimshangaza na
kumfanya akimbie kwanza na baadaye kufanya mawasiliano naye.
BINTI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi, binti huyo alikiri kutoweka nyumbani kwao Aprili 15, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema hakujua kilichoendelea baada ya kuondoka nyumbani
lakini baadaye alibaini kuwa alikuwa katika Kijiji cha Olkokola wilayani
Arumeru na alikwenda kwenye nyumba ya mwanamke mmoja asiyefahamiana
naye akamuomba maji ya kunywa.
“Nilifika kwenye nyumba moja nikamkuta mama mmoja, nikamwomba
maji ya kunywa akaenda kuniletea. Nilikunywa huku amenisimamia, lakini
maji yalikuwa machungu sana, nikamrudishia, akanilazimisha ninywe kwa
kunisukumia kikombe kinywani. Nilipomaliza nilipoteza fahamu.
“Baadaye nilizinduka, nikaendelea kuishi palepale nyumbani kwa yule mama lakini sifahamu nilikuwa nafanya nini.
“Juzi ndiyo nikashangaa
kujikuta nimerudi nyumbani, mimi sijui nini kilikuwa kikiendelea,” alisema binti huyo.
MAJIRANI NAO
Majirani kadhaa waliokuwepo nyumbani kwa Obed walilielezea tukio
hilo kwamba ni la ushirikina huku wakisema ni jambo la kuogofya ambalo
halikuwahi kutokea kijijini hapo kabla.
Wengine walisema kuwa binti huyo alifufuka na wengine walisema alichukuliwa msukule.
“Hili si suala la kawaida lazima kuna ushirikina kwani huyu
binti tulishamzika na wazazi wake walimtambua kabisa kuwa ni yeye baada
ya kuambiwa alikutwa amekufa, sasa hebu fikiria tangu tumezika
mbona hakuna mtu aliyekuja na kusema na yeye alipotelewa na binti yake
halafu cha ajabu hilo kaburi mbona limebonyea? Atakuwa amefufuka,’
alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Amina Liwa.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Benedict Mpujila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.
KUMBUKUMBU
Mapema mwaka jana tukio la kishirikina liliibuka katika wilayani
Arumeru eneo la Kwa Mrefu ambapo mtu mmoja alidaiwa kudondoka na ungo,
muda mfupi baadaye alitoweka na kwenye ungo kubaki mayai na kuku mweupe.
Chanzo:GlobalPublishers