BUNGENI: KIBARUA CHA MAKINDA KUOTA NYASI, ATISHIWA KUNG'OLEWA USPIKA
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-kibarua-cha-makinda-kuota-nyasi.html
BUNGE la Muungano jana lilitibuka baada ya wabunge kurushiana vijembe
kuhusu madai kwamba baadhi ya mawaziri na wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wanakomba mamilioni ya fedha kutoka mifuko ya hifadhi ya
jamii zinazochangwa na wafanyakazi nchini.
Mjadala huo uliibuka jana baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Wa kwanza kuibua hoja hiyo alikuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi,
Kapteni John Komba (CCM), ambaye alimlalamikia Mbunge wa Singida
Vijijini, Tundu Lissu (CHADEMA), kwamba amelidang’anya na kulipotosha
Bunge.
Komba ambaye alikuwa akizungumza kwa jazba, alisema Lissu amekaririwa
na baadhi ya vyombo vya habari jana akitaja majina ya wabunge na
mawaziri waliopata mamilioni kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa
Serikali za Mitaa (LAPF).
Mbunge huyo wa CCM ambaye alikuwa akitumia lugha zisizo za staha
kumshambulia Lissu, alisema fedha za LAPF sh milioni 1.5 zilizotolewa
kwa kikundi kimoja cha kuweka na kukopa jimboni kwake zilitumika kwa
kununua injini ya boti kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
“Mheshimiwa Spika, sijui hizi ni akili za namna gani, sijawahi kufika
ofisi za LAPF, wala simjui meneja wake na wala sijapata fedha zozote
tangu taasisi hiyo ianze, naomba mwongozo wako kuhusu madai haya,”
alisema Komba.
Kabla ya kutoa mwongozo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema yeye ni mmoja wa mawaziri
waliowahi kupata msaada wa LAPF.
Lukuvi alisema taasisi hiyo pamoja na nyingine zote, zina fungu maalumu kwa ajili ya kusaidia huduma za jamii.
“Mheshimiwa Spika, LAPF, NSSF, PPF na mifuko mingine ha hata mabenki
yana fungu la kuhudumia jamii ambapo wabunge wanaweza kwenda kuomba
msaada wa masuala ya elimu, afya na huduma nyingine. Mimi mwenyewe
nilishapata msaada wa LAPF mara tatu, kwa hiyo kuomba hakuna
tatizo,” alisema Lukuvi.
Waziri mwingine aliyeibuka kujibu hoja hiyo ni Waziri wa Kazi na
Ajira, Gaudensia Kabaka, aliyesema LAPF ilitoa fedha hizo kihalali na
kwa mujibu wa sheria.
Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Serikali za Mitaa,
Tawala za Mikoa (Tamisemi), alipinga hoja ya mawaziri na wabunge kuchota
mamilioni hayo bali walipata misaada kwa ajili ya majimbo yao na
wamefanya kihalali na LAPF imetoa misaada hiyo kisheria.
Ghasia, alisema wakati Lissu anahoji fedha kidogo walizopata mawaziri
na wabunge aliowataja, kiongozi wake wa kambi rasmi ya upinzani,
Freeman Mbowe, anadaiwa na NSSF zaidi ya bilioni moja na kuna hati yake
ya kukamatwa kwa ajili ya madai hayo.
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, ambaye ni mmoja wa
mawaziri waliotajwa kunufaika na fedha hizo, kwanza aliomba mwongozo wa
spika kuhusu Lissu.
Alisema Lissu ameibua hoja hiyo bila kutangaza maslahi binafsi
aliyonayo kwani kuna mtumishi aliyefukuzwa LAPF kwa ubadhilifu wa fedha,
anamtetea mahakamani.
“Mheshimiwa Spika, Lissu hajatangaza maslahi binafsi katika suala
hilo. Yeye anamtetea mtumishi anayetuhumiwa kufilisi mabilioni LAPF
wakati yeye anahoji wanaosaidiwa sh milioni mbili kuleta maendeleo
kwenye majimbo yao. Naomba mwongozo wako katika hili,” alisema.
Nchemba, alisema kazi ya kutafuta misaada majimboni ni ya maana sana
na kama wabunge wa CCM wameomba na kupata fedha LAPF, wanapaswa
kupongezwa kwani ndio uwajibikaji wa mbunge.
Baada ya maelezo kutoka kwa mawaziri hao, Naibu Spika Job Ndugai,
alimtaka Lissu kusimama na kutoa maelezo ya ziada juu ya madai
aliyoyatoa.
Akitoa maelezo ya ziada kuhusu madai hayo, Lissu alisisitiza kuwa
mawaziri na wabunge aliowataja, wamekuwa ombaomba na wamekomba fedha za
LAPF zinazochangwa na wafanyakazi.
Alisema wakati viongozi hao wakichotewa fedha kutoka mfuko huo, wapo
wafanyakazi wanahaha kupata malipo yao bila sababu za msingi.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi wanaopata fedha hizo ni wabunge
wa CCM tu, kama kuna mpango huo, kwanini wengine hawapati msaada? Jambo
la tatu Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za LAPF zinatumika kununulia jezi
na mipira. Waziri Magufuli kanunulia jezi na mipira kwa ajili ya vijana
wa jimbo lake. Fedha za LAPF zimetumika kununulia kompyuta Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati Bunge kila mwaka
linatenga fedha kwa ajili ya wizara zote,” alisema Lissu na kuibua zogo
kutoka kwa baadhi ya wabunge wa CCM kumpinga.
Baada ya kuibuka kwa mzozo ndani ya Bunge hilo jana, Naibu Spika
Ndugai aliamua kuifunga hoja hiyo, huku akisema unaponyoosha kidole
kimoja kwa mwenzio, jiangalie wewe mwenyewe ni msafi kiasi gani.
Alichosema Tundu Lissu
Lissu, juzi aliwataja kwa majina mawaziri na wabunge aliosema bungeni kuwa wamekuwa ombaomba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni
Naibu Spika, Job Ndugai na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na
Uratibu wa Bunge), William Lukuvi.
Wengine ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na wabunge
Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba
(Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye
(Arumeru Magharibi).
Mbali na kuwataja kwa majina, Lissu pia ametoa vielelezo
vinavyoonyesha jinsi walivyokuwa wakiidhinishiwa malipo kwa nyakati
tofauti na LAPF, kwa sababu mbalimbali.
Lissu aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kiwango cha fedha kutokuwa
kikubwa, lakini kinaweza kusababisha mgongano wa kimasilahi kati ya
wajibu wa wabunge kwa umma na masilahi yao binafsi.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha Bunge kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia serikali na taasisi zake.
Mchanganuo wa malipo
LAPF ilitoa sh milioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa madarasa Jimbo la
Kongwa linaloongozwa na Ndugai, ilitoa Sh milioni 1.6 kwa ajili ya
kuisaidia Shule ya Isimani iliyopo katika Jimbo la Waziri Lukuvi, sh
milioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maabara wa Jimbo la Arumeru Magharibi.
Waziri Kairuki aliidhinishiwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta
mpakato (Laptop) mbili kwa ajili ya vyama vya wafanyakazi, sh milioni
2.5 kwa Waziri Chana ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kwa ajili ya
taasisi ya Iringa Constituency Development Account.
Aprili 5 mwaka jana, LAPF iliidhinisha sh 500,000 kwa ajili ya
taasisi ya Ukonga Constituency Development Trust Fund inayoongozwa na
Mwaiposa katika Jimbo la Ukonga.
Februari 2013, LAPF iliidhinisha sh milioni 2.8 kwa Machangu kwa
ajili ya taasisi inayoitwa Iyana Education Trust, aliyodai kuwa ni mali
ya Machangu na Agosti, 2013 LAPF iliidhinisha fedha za kununulia
pikipiki mbili kwa ajili ya vituo vya afya vya Jimbo la Mtera
linaloongozwa na Lusinde.
LAPF pia ililipa sh milioni 1.5 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za
maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Nyasa Foundation, uliopo katika eneo la
jimbo linaloongozwa na Komba ambaye pia ni mlezi wa mfuko huo.
LAPF iliidhinisha sh milioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maabara wa Jimbo la Arumeru Magharibi la Medeye.
Lugola atishia kumng’oa Spika
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM),
ametishia kuendesha harakati za kumng’oa Spika Anne Makinda kama muswada
wa VAT hautapelekwa bungeni.
Muswada huo utalenga kuondoa misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara
wakubwa ambapo kwa mwaka 2012/2013, serikali ilipoteza sh trilioni 1.6.
Akiomba mwongozo wa spika, Lugola alisema kuna taarifa kwamba Bunge halina mpango wa kupeleka muswada huo.
“Kama Spika Makinda ataendelea kuilinda serikali na isiulete muswada
huo kipindi hiki, nitaongoza harakati za kumng’oa,” alisema.
Lugola alisema Bunge haliwezi kukubali serikali iendelee kupoteza fedha kwa ajili ya misamaha ya kodi.
Akijibu mwongozo huo, Waziri Lukuvi alisema muswada huo utaletwa katika Bunge hili na hilo halimhusu Spika Makinda.
Chanzo:TanzaniaDaima