ELIMU: CWT YAIPA SERIKALI SIKU 14 KUPANDISHA MSHAHARA, LA SIVYO WALIMU WAPANGA KUANDAMANA NCHI NZIMA
![](https://resources.blogblog.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/09/elimu-cwt-yaipa-serikali-siku-14.html
BARAZA la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT), limetoa siku 14
kwa wakurugenzi wa halmshauri nchini kuwapa barua za kuwapandisha vyeo
walimu wanaostahili la sivyo watafanya maandamano nchi nzima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa
CWT, Gratian Mukoba, alisema maazimio ya baraza hilo yalifikiwa tarehe
28 mwezi uliyopita mkoani Morogoro.
Mukoba, alisema ifikapo Septemba 15 mwaka huu kama wakurugenzi
watakuwa hawajawapatia walimu wanaostahili barua za kuwapandisha vyeo,
basi watarajie maandamano ya walimu kwenye ofisi zao.
“Baraza limetoa siku 14 kuanzia siku ya kikao na ifikapo siku ya
tarehe 15 kama walimu wanaostahili kupandishwa vyeo watakuwa hawajapewa
barua zao, kutafanyika maandano ya nchi nzima kuelekea kwa wakurugenzi
wa halmashauri kudai barua hizo, hatupendi hali hii itokee lakini
hatufurahishwi na hali ya kutojali haki zetu,” alisema Mukoba.
Aidha, Mukoba alisema Baraza limekemea tabia ya serikali ya
kuwanyang’anya walimu madaraja ambayo tayari wamekwishayapokea kwa
kisingizio cha kutokuwapo fedha za kulipa.
Alisema hata nyongeza ya mishahara iliyotolewa Julai mwaka huu
imepingwa na walimu nchi nzima, kwani mbali ya kuwa ndogo sana imetolewa
kwa upendeleo na walimu wanataka kujua ni kwanini watumishi wengine
waongezwe kwa asilimia kumi na walimu asilimia 6.35.