jaridahuru

Mitandao

SIASA: UKAWA YAZIDI KUITETEMESHA SERIKALI, SASA WAHOJI MAMLAKA YA BUNGE MAALAMU NAUWEZO WAKE




MATUMAINI ya kupatikana kwa katiba mpya na uwepo wa Bunge Maalum Agosti 5, yatajulikana wiki hii katika vikao vya maridhiano vitakavyofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta.

Hata hivyo, maajaliwa hayo yatategemea zaidi kulainika kwa misimamo baina ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pande hizi mbili kila moja ina msimamo wake. UKAWA wanataka pendekezo la serikali tatu lililopo kwenye rasimu ya katiba ndilo liwe msingi wa majadiliano bungeni, CCM wanataka serikali mbili ambazo hazikupendekezwa na tume.

Msuguano wa pande hizo mbili hivi sasa umeligawa taifa na kutishia upatikanaji wa katiba mpya ambayo mchakato wake utaligharimu taifa zaidi ya sh bilioni 80.

Katiba hiyo haitoweza kupatikana bila uwepo wa UKAWA kwakuwa sheria ya mabadiliko ya katiba inaweka wazi kuwa ili vifungu vya katiba vipitishwe bungeni ni lazima vipitishwe kwa theluthi mbili ya kura za wajumbe kutoka Zanzibar na Tanzania bara.

Kipengele hicho ndiyo kikwazo kwa CCM kwa kuwa kwa bara wana uhakika wa kupata idadi hiyo, lakini Zanzibar hawawezi kuipata bila kushirikisha wajumbe wa CUF ambao wamo ndani ya UKAWA, wenye msimamo wa serikali tatu.

Kukwama au kuendelea kwa mchakato huo kutaanza kujulikana kesho katika kikao kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi na pande zinazopingana.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa Mutungi, amelazimika kuingilia jambo hilo baada ya Ikulu kumtaka afanye hivyo ili kunusuru mchakato huo. Hata hivyo, katika hatua ya awali ofisi yake iliingilia kwa vitisho dhidi ya CHADEMA, chama chenye nguvu na kinachoongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Hata hivyo, taarifa za Ikulu kukutana na kiongozi mmoja wa UKAWA kuzungumzia sakata hilo zilikanushwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ingawa ilikiri kuwa Rais Kikwete anaunga mkono jitihada za kutafuta ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Sitta, naye amejitosa kutafuta suluhu hiyo kwa kuitisha kikao cha watu 30 kitakachofanyika Julai 24.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa licha ya kuwapo kwa jitihada hizo, mchakato huo uko shakani kwakuwa kila upande hauonekani kuwa tayari kuachia msimamo walionao.
Moja ya kikwazo kinachoelezwa na wadau mbalimbali, ni kuwa viongozi wanaoitisha majadiliano hayo hawana ubavu wa kutatua mgogoro huo isipokuwa Rais Kikwete ambaye naye anashikilia msimamo wa serikali mbili.

Hoja hiyo ilipata mashiko kwenye mkutano wa kwanza ulioitishwa na Jaji Mutungi, uliomalizika huku UKAWA ikionyesha wazi kutilia shaka mamlaka iliyompatia haki ya kuitisha kikao hicho.
UKAWA pia wamekuwa wakisimamia kutaka kujua uhalali wa Bunge la Katiba kuwa na mamlaka ya kuifumua na kuibadili rasimu ya katiba iliyoandikwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ikiwa na muundo wa serikali tatu.

Hata katika mazungumzo yaliyopita na Jaji Mutungi suala ambalo lilionekana kusababisha msuguano utakaosababisha kushindikana kupatikana katiba mpya ni la UKAWA kusimamia sheria inayozuia Bunge Maalum kutokuwa na mamlaka ya kuifumua rasimu na kuibadilisha isipokuwa kazi yao ni kuiboresha.

Suala hilo limekuwa likipingwa na wajumbe wa CCM wanaotetea kwa kusema kuwa sheria inawaruhusu wajumbe wa Bunge hilo kufanya chochote katika rasimu.
Tayari UKAWA wameonyesha hofu kuwa vikao hivyo havitazaa matunda yanayotarajiwa bali suluhu ya jambo hilo lipo kwa muasisi wake Rais Kikwete.

Ili kuonyesha kwamba suala la kurejea bungeni kwa UKAWA litakuwa gumu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema kuwa hawatakuwa tayari kurejea bungeni kwa kupitia hila za CCM.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa UKAWA, katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA alipigia msumari kwa kusema kuwa UKAWA wanaona ni uendawazimu kurudi bungeni wakati CCM na viongozi wake hawako tayari kufuata rasimu iliyopelekwa bungeni.

Aliongeza kuwa hawatakuwa tayari kurejea bungeni ili baadaye wajumbe wa CCM, waendelee kuwakejeli hivyo ni bora wasirejee katika vikao hivyo.

Mwanasheria TLS
Naye SHEHE SEMTAWA anaripoti kuwa Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, amesema kutokana na tofauti zilizojitokeza kwenye Bunge Maalum la Katiba katika kutafsiri sheria kuhusu muundo wa serikali, ni vema suala hilo likafikishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Alisema kuwa kutokana na pande hizo mbili kukwaruzana kuhusu serikali moja au mbili, ni vema suala hilo likafikishwa Mahakama Kuu itakapopatikana tafsri kuhusu sheria ya mwenendo mzima wa sheria na kanuni zinazoendesha Bunge.

Stolla, alibainisha kuwa baada ya mahakama kutumia mamlaka yake ya kutafsiri sheria, chochote kitakachoamuliwa na mahakama hiyo itabidi Bunge la Katiba likubali kufuata uamuzi huo.

Related

Siasa 3095785023423174433

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item