SIASA: BAADA YA KUDAIWA FIDIA BILIONI 310, KAFULILA SASA ATOA MPYA, AIBUKIA TAKUKURU NA KUTOA NYARAKA NYETI

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-baada-ya-kudaiwa-fidia-bilioni.html
HATIMAYE Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulia (NCCR-Mageuzi),
amewasilisha ushahidi wake kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) kuhusu tuhuma za wizi katika akaunti ya Tegeta Escrow
alizozitoa bungeni akiwahusisha vigogo sita wa serikali.
Katika ushahidi huo, Kafulila anaeleza sababu zake ni kwanini anataka
Bunge lichunguze tuhuma hizo badala ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Takukuru.
Kwa mujibu wa barua yake kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na
nakala kwa Spika wa Bunge na CAG, Kafulila ametoa maelezo yenye kurasa
saba akiambatanisha na vielelezo kadhaa juu ya tuhuma hizo.
“Nikichangia hotuba ya waziri mkuu nilitaka uchunguzi ufanyike
kupitia Kamati Teule ya Bunge kuhusu tuhuma zinazohusisha kiasi cha dola
270 milioni zilizopaswa kuwa ndani ya akaunti hiyo sanjari na zile dola
122 milioni zilizokwishatolewa na kupewa Kampuni ya PAP,” inasomeka
barua hiyo.
Kafulila alisema Takukuru ni chombo chenye jukumu zito, lakini hakina
meno kukabiliana na rushwa zinazowakabili vigogo wa serikali kwani
mwamuzi wa mwisho katika masuala hayo huwa ni Ofisi ya Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DPP) ambaye amekuwa akitupilia mbali mashitaka kwa
kisingizio cha mamlaka aliyonayo kikatiba.
Sababu ya pili kwa mujibu wa barua hiyo ni malalamiko ya Ofisi ya
Takukuru yenyewe kusema kuwa Ofisi ya DPP inakwamisha ufanisi wa vita
dhidi ya rushwa, ilikuwa ni ushahidi tosha wa yeye kukataa uchunguzi
ufanywe na Takukuru.
Sababu ya tatu, Kafulila alinukuu taarifa za wikleaks kuwa rais
anakwamisha mambo mengi kuhusu vita dhidi ya ufisadi, huku sababu ya nne
ikiwa ni uzoefu kuwa ufisadi huu umekaliwa kimya na Ikulu bila
kufanyiwa kazi.
“Unakumbuka Dk. Hosea kuwa taasisi yako katika miaka ya 2000 ukiwa
mkurugenzi ulipata kuchunguza kuhusu ufisadi wa mkataba wa IPTL namna
ulivyofikiwa kifisadi, lakini pamoja na kufanya kazi hiyo nzuri, Ikulu
haikuchukua hatua dhidi ya wahusika na wewe unafahamu kuwa ripoti hiyo
ingetosha kuwa ushahidi katika Mahakama ya ISCID kuweza kubatilisha
mkataba wenyewe ulionyonya uchumi wa nchi yetu kwa muda mrefu, lakini
Ikulu imekaa kimya,” ilisomeka sehemu ya ushahidi.
Gazeti hili liliona maeneo yaliyoainishwa na Kafulila kuashiria kuwa
hukumu ya Jaji Utamwa haikuhusu fedha ndani ya Escrow kama Waziri wa
Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alivyolieleza Bunge mapema
mwaka huu.
CHADEMA waunga mkono
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya
Kikwete aitishe tenda kwa utaratibu wa kimataifa ili kuchunguza fedha
zilizokwapuliwa katika akaunti ya Escrow.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema kuwa ni
jukumu la serikali kuhakikisha hakuna wizi ili kusafisha taifa na
kuachana na tabia ya kugeuka ombaomba.
Alisema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema,
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, Gavana wa Benki Kuu, Beno
Ndullu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi
waache blabla, waeleze ukweli.
Dk. Slaa alisisitiza kuwa katika suala la fedha za Escrow hawawezi
kunyamaza na kuona nchi ikiendelea kuliwa na kuongeza kuwa ingawa Bunge
lilitoa agizo kwa CAG na Takukuru kuchunguza suala hilo, hana imani na
watu hao.
Alisema kuwa hawana imani na Mkurugenzi Takukuru, Dk. Edward Hoseah
kwani taasisi hiyo iliwahi kutumika kusafisha sakata la Richmond.
Pia aliishutumu ofisi ya CAG kuwa nayo ilihusika kumsafisha aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, katika kashfa ya kugawa
fedha kwa wabunge ili waiunge mkono na kupitisha bajeti ya wizara hiyo.
Alisema kuwa fedha hizo ni za serikali ndiyo maana gavana anaandika,
na kuongeza kuwa ni wakaguzi wa kimataifa pekee ndio watatoa majibu
sahihi ikiwemo lini PAP alinunua Kampuni ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL).