MAHUSIANO: UPO WAKATI HISIA ZA MSISIMKO, KUPENDA HUPOTEA KABISA KATIKA MAHUSIANO
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/mahusiano-upo-wakati-hisia-za-msisimko.html
NI somo gumu kidogo lakini ni vizuri kulijadili
maana linajenga na kustawisha uhusiano. Wengi huogopa kujifunza kuhusu
hili. Ndugu zangu huu ni ugonjwa, tena hatari sana kwenye uhusiano.
Kuna
watu wapo kwenye uhusiano na wenzi ambao wamepoteza msisimko wa
mapenzi. Yaani wanashindwa kuwa na uwezo wa kupenda. Upo uwezekano
kwamba, hukumwelewa vizuri mpenzi wako mwanzoni, lakini sasa unagundua
kwamba amepoteza uwezo wa kupenda.
\Suala la kushindwa au kupunguza msisimko wa kupenda ni ugonjwa!
Lakini baadhi ya wahusika hufahamu tatizo hili na wengine hawafahamu.
Wanaofahamu ni vigumu sana kueleza moja kwa moja kwamba wanakabiliwa na
tatizo hili.
Ni vigumu sana kugundua hili mapema, lakini ukimchunguza na kuwa
mkweli kwake, ni rahisi kukueleza ukweli huu uliojificha moyoni mwake.
Pengine wakati unakutana naye, alikukatalia akisema muda wa kuwa na
mpenzi bado, lakini ukaendelea kumsumbua na kukukubalia, mwisho
ukagundua hafurahii uhusiano wenu.
Hili huwa tatizo kubwa sana kwa walio wengi. Wakati mwingine yawezekana ukawa unafanya bidii ya kumshawishi mpenzi mpya lakini akawa katika tatizo hili.
Kila siku anakuzungusha, lakini siku moja akaamua kukueleza ukweli,
kwamba anashidwa kukupenda! Huyu ni mzuri zaidi kwako, maana angalau
sasa anakuwa amefahamu tatizo lake na amekupa nafasi ya kulijua, sasa
wajibu wako unakuwa kumpa tiba timilifu.
IKOJE HII?
Tatizo la kutokuwa na uwezo wa kupenda, limekuwa likiwasumbua wengi
sana siku hizi (hasa wanawake). Sababu kubwa zaidi ni kuwa na uhusiano
wenye historia mbaya katika kipindi kilichopita!
Mwanamke aliyeachwa na wanaume watatu kwa kipindi cha miezi miwili, hawezi kuwa na uwezo wa kupenda kwa moyo zaidi kama yule ambaye ndiyo kwanza anaanza uhusiano.
Mwanamke aliyeachwa na mwanaume wake aliyedumu naye kwa miaka minne,
anaweza kuwa bora zaidi katika uhusiano mpya akitaka kuokoa maisha yake
ya kimapenzi kuliko yule ambaye ametoswa mara nyingi zaidi.
Kisaikolojia,
zipo sababu nyingi zinazoelezwa kuchangia kumfanya mtu apoteze uwezo wa
kupenda. Lakini sababu kubwa zaidi zilizotajwa ni hizi hapa chini;
MOSI: Anahisi havutii sana. Mara nyingi wasichana wakiachwa,
huchukulia kwamba huenda hawana mvuto sana. Kwa hiyo anahisi hata kama
atakupenda, akitokea mwenye mvuto zaidi yake, utamtosa kama alivyofanya
aliyepita!
PILI: Huogopa ugonjwa wa moyo. Inawezekana ameshaumizwa sana huko
nyuma na kila anapokuangalia anahisi kuteswa tena na hivyo anaogopa tena
kupata ugonjwa wa moyo! Ana mashaka, hana amani na mapenzi tena, sababu
kubwa ni historia iliyopita.
TATU: Anakuwa na mawazo kwamba, yawezekana na wewe ni sawa na mpenzi
wake aliyepita. Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mtu akiwa katika athari,
akili yake yote inamwambia kwamba wote wanaweza kuwa sawa na waliopita!
Kikubwa ni kumtambua tu, baada ya hapo nitakufundisha cha kufanya.
Wiki ijayo tutaangalia namna ya kumtambua kabla ya kuingia kwenye somo
lenyewe na namna ya kutafuta tiba, USIKOSE!