MAKALA: NANI KASEMA UZALENDO UNAPIMWA KWA MATAMASHA YA MUZIKI?

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/makala-nani-kasema-uzalendo-unapimwa.html
Mgeni rasmi wa tamasha hilo alikuwa ni Rais Jakaya
Kikwete, akiwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri
na viongozi wengine wa Serikali.
Rais Kikwete aliyezindua video ya wasanii
mbalimbali alisema amependezwa na wimbo wa uzalendo huku akiwataka
Watanzania kutimiza wajibu wao wa kuilinda nchi yao kwani inafitiniwa na
kuchukiwa na wengi.
Inawezekana ni kutokana na mwaliko huo, ndipo Rais
Kikwete akalazimika kutoa maoni kama hayo. Lakini ijulikane kuwa suala
la uzalendo linakwenda mbali zaidi ya matamasha kama hayo. Uzalendo ni
hali ya mtu kuipenda nchi yake. Neno hili lilitumika sana miaka ya 1950
na kuendelea wakati nchi za Afrika na kwingineko duniani zikipigania
uhuru kutoka kwa wakoloni hasa miaka ya ‘60.
Watu waliungana kwa moyo wote kwa sababu walijua
adui yao ni mkoloni. Lakini baada ya uhuru kupatikana, tunaona neno
lenyewe likaanza kupoteza uhalisia wake, kwa sababu wale viongozi
walioingia madarakani wakajivisha tena madaraka ya ukoloni.
Leo, miaka 52 baada ya uhuru, ukiuliza Watanzania
wanaungana ili kupambana na adui gani, haieleweki. Hakuna anayejali tena
nchi, kila mtu anajitafutia mtaji wake aondoke.
Kwa hali ilivyo sasa ni nadra kuona Mtanzania
mzalendo. Maadili yameshuka tangu uongozi wa juu wa Serikali hadi ngazi
za chini. Kila kukicha utasikia kashfa ya wizi wa fedha za Serikali na
wezi hawachukuliwi hatua. Leo utasikia kashfa ya EPA, mara wezi
wamesamehewa, kesho utasikia kashfa ya IPTL, kila mtu anaruka kimanga na
nyinginezo nyingi.
Rais Kikwete ameshakiri mara kadhaa kuwa na orodha
ya wala rushwa, majangili 40 wa meno ya tembo, lakini hatuoni
wakikamatwa wala kuwajibishwa.
Halafu akitoka hapo, anawataka Watanzania waipende
nchi yao! Tutaipendaje nchi wakati wachache wanafaidi matunda ya uhuru
na wengi wanalala njaa?
Matokeo yake sasa karibu kila Mtanzania anatafuta
upenyo naye aibe siku ziende. Kama ni mfanya usafi ofisini, anaiba
sabuni walau akauze mtaani, dereva naye anaiba mafuta akauze, ofisa
anabuni miradi na safari hewa ili apate cha juu, waziri anaingia
mikataba bandia na wawekezaji ili apate asilimia 10. Mwisho wa yote Rais
amekaa kimya!
Rushwa imekithiri, siyo hospitali, shuleni,
mahakamani na popote zinapotolewa huduma. Uzalendo haupo tena, kila mtu
anachukua chake mapema.
Tatizo hili halitatibika kwa kufanya matamasha ya muziki na kuleta wasanii wa muziki wa Marekani kuja kutumbuiza.