SIASA: KAFULILA, WEREMA WINGIA VITA KALI, WEREMA AMKOSAKOSA NGUMI KAFULILA, ASEMA ATAMKATA KICHWA KAFULILA

https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/siasa-kafulila-werema-wingia-vita-kali.html
Dodoma. Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo.
Ugomvi baina yao uliendelea jana asubuhi nje ya
Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha
kikao cha Bunge hadi leo.
Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu
kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama ishara ya
kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge huyo.
Juzi asubuhi baada ya Zungu kuahirisha kikao cha
Bunge, muda mfupi baada ya Jaji Werema na Kafulila kurushiana maneno
bungeni, mwanasheria huyo alitaka kumtia adabu Kafulila kwa kumwita
mwizi.
Kafulila alimwita Jaji Werema mwizi akijibu mapigo baada ya awali kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Ilivyokuwa jana
Wakati akizungumza na gazeti hili mara baada ya
Bunge kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila
katika Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo
chake cha kumwita mwizi.
“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita mimi mwizi.
Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa kabisa na
kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata Kafulila ambaye
alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.
Jaji Werema alisema juzi alishikwa na jazba baada
ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya Ukumbi
wa Bunge.
Wakati Jaji Werema akiendelea kumlalamikia
Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe mbunge
huyo... “Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya kusameheana,
yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”
Lakini badala ya kukubaliana na ombi la Zungu,
Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi
nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba
msamaha.”
Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi.”
Wakati wakiendelea kurushiana maneno, Zungu alikuwa katikati
yao, huku akiwasihi wapeane mkono na kusameheana bila mafanikio... “Haya
mambo yamekwisha jamani, malizeni tofauti hizi.”
Kama vile alijua kuwa kauli ya kuua ilimchanganya
Kafulila, Jaji Werema huku akitembea kuelekea katika Jengo la Utawala la
Bunge alisema: “Siwezi kukuua kwa maana hiyo unayodhani, maana kufa
utakufa kwa mapenzi ya Mungu, ila tutapambana tu, nitakuonyesha.”
Kauli ya Kafulila
Akizungumza baadaye, Kafulila alisema: “Kutokana
na hali ilivyo sasa, nimeandika barua Ofisi ya Spika juu ya vitisho
nilivyopewa na Jaji Werema, kwanza jana (juzi) alitaka kunivamia pale
bungeni na kunipiga, leo (jana) asubuhi amenitishia kuwa atanikata
kichwa.”
Kafulila alisema barua hiyo pia ataipeleka Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelezo kuwa siku za hivi karibuni
yamekuwa yakitokea matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kutupwa porini...
“Kwa nafasi yake, Werema anaweza kufanya lolote, hivyo barua hizo
zinalenga kueleza alichokusudia kunifanyia.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
alipoulizwa kuhusu mvutano uliotokea juzi bungeni na barua za Kafulila
alisema Ofisi ya Bunge haijapata malalamiko yoyote.
“Jana sikuwapo bungeni lakini mpaka sasa hakuna
malalamiko yoyote yaliyoletwa katika Ofisi ya Bunge. Kama wangeshikana
mashati ndani ya Bunge hilo lingekuwa kosa la kufanya fujo bungeni na
adhabu zake zipo wazi,” alisema Joel.
Juzi, baada ya kurushiana maneno, Jaji Werema
alinyanyuka alipokuwa amekaa na kuanza kumfuata Kafulila kabla ya
kuzuiwa na kundi la mawaziri.
Mbali na kumzuia, mawaziri hao walimsindikiza hadi nje ya Ukumbi wa Bunge ambako alipanda gari lake na kuondoka.