https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/jamii-siri-nzito-bidhaa-za-machinga.html
Katika eneo la mnada wa kuuza vitu vya machinga
vilivyokamatwa lililopo katika Soko la Kibasila Gerezani, kulikuwa na
makundi ya watu wa aina mbili; waliokwenda kununua vitu vingi kwa bei
ndogo na wengine ni wale ambao bidhaa zao ndizo zilikuwa zinapigwa mnada
na hawakuwa na uwezo wa kushinikiza wauziwe wao.
Wafanyabiashara waliokuwapo katika eneo hilo jana,
walisikika wakisema wamekwenda kununua vitu vya dhuluma na kwamba
walilazimika kununua kwa kuwa hakukuwa na njia nyingine ya kufanya.
Leonard Mwagike alisema baada ya bidhaa zake
kukamatwa alijaribu kwenda kuzikomboa lakini alishindwa baada ya
Mahakama ya Jiji kumwamuru alipe faini ya Sh400,000.
“Kinachoendelea hapa ni dhuluma tu, haiwezekani
mzigo wangu wa Sh50,000 uniambie nilipe faini ya Sh400, 000, bora kuja
hapa kuununua tena kama nitaweza,” alisema kwa huzuni.
Mfanyakazi wa kampuni moja ya udalali jijini,
iliyopewa mamlaka ya kuuza bidhaa hizo, alikuwa akifungua mzigo mmoja
baada ya mwingine na kuwataka wafanyabiashara hao wapange bei.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida,
alionekana kutaka kuchukua kila bidhaa aliyoiona ni nzuri, huku
akiwaambia wanunuzi kuwa alikwishaichunguza mizigo hiyo kwa hiyo anajua
upi ni mzuri.
Mzigo wa kwanza kufunguliwa ulikuwa una vyombo vya
plastiki vya kuwekea chakula, ambavyo vyote viliuzwa kwa Sh10, 000.
Zilifuata nguo za watoto na chupa za chai, kisha ukafika wakati ulioleta
msuguano kiasi cha kutishia mnada kuvunjika.
“Sasa kwenye mzigo huu kuna mali nzuri wengine
wameshaiona si ndiyo? Eeh! Ni madera (magauni), mfuko mzima shilingi
ngapi?” Anauliza dalali, lakini kabla hajapata jibu anasema:
“Jamani yupo shemeji yenu (mke wake) lazima naye
apate hizi nguo (huku minong’ono ikianza kusikika anachukua magauni
matatu na kuyaweka pembeni).”
Kitendo hicho kiliwakasirisha baadhi ya machinga
waliokuwapo katika eneo hilo, huku wakisema iwapo angeuona mapema mzigo
huo angeuchukua wote.
“Mali mmetunyanganya sisi na hata tunazonunua hapa
mtazichukua tena, halafu bado mnachukua hata mnazouza, hili
halikubaliki,” alisema mfanyabiashara mmoja.
Baada ya kuuzwa kwa bidhaa mbalimbali zikiwamo feni, viatu na
suruali, linapatikana tena furushi lenye madera na hali ikawa kama
ilivyokuwa awali.
Dalali: “Ule mzigo huu hapa tena, lakini saa hizi
tuuweke pembeni kwanza, mimi ninaweza kuuchukua wote.” Kauli hiyo
inapingwa huku kila mtu akitaka magauni yote yahesabiwe.
Wakati uuzaji ukiendelea, Mmachinga mmojawapo
anabaini kuwa mzigo wake uliokuwa umekamatwa umeuzwa kwa mtu mwingine
hivyo anaamua kumfuata na kuongea naye.
“Haiwezekani mzigo wangu mkubwa vile wa mikoba anunue mtu kwa Sh8,000 tu,” anasema huku akiondoka.
Hamisi Kiwanuka anasema alikamatwa kwa kosa la
kupanga na kuuza feni barabarani, lakini alipojaribu kuzitafuta baadaye
hakuzipata, badala yake aliziona nyingine zimevunjika, ambazo hazikuwa
zake.
“Hawa jamaa wanauza hapa vitu vilivyobaki baada ya kuchambuliwa sana, vizuri vyote wamechukua,” alisema.
Pia, mama mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Mama Kuluthumu, ambaye alifanikiwa kununua sufuria 17 kwa sh10, 000, alisema:
“Baadhi ya sufuria ziliondoka na wali na nyama sijui ziko wapi?”
Viongozi wanena
Mwenyekiti wa Operesheni ya kuwaondoa Wamachinga
barabarani jijini hapa, Msongoro Songoro, alisema wapo wafanyabiashara
wa aina mbili ambao wanalengwa katika zoezi hilo la safisha jiji;
wanaotoa bidhaa ndani ya maduka na kuzipanga nje na wale wanaoweka
barabarani.
Wafanyabiashara wanaopatikana na kosa la kupanga
bidhaa nje hutozwa faini ya papo kwa papo ya Sh50, 000 na kupewa onyo,
ambapo fedha inayopatikana hupelekwa katika halmashauri husika na zile
zinazopatikana kwenye mnada hupelekwa ofisi ya jiji.
“Lakini anayepanga bidhaa barabarani, akikamatwa
anafikishwa mahakamani na mali yake inataifishwa kwa sababu hana leseni
ya kufanya biashara hiyo,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema hadi kufikia Juni 12 mwaka huu jumla ya
wafanyabiashara 711 walifikishwa mahakamani, huku baadhi yao
wakihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au faini kati ya Sh100,000 na
Sh400, 000.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za askari wa Jiji kula
chakula cha wafanyabiashara, Songoro alisema kuwa taarifa hizo siyo za
kweli kwa sababu kutokana na vurugu zinazokuwapo wakati wa ukamataji
siyo rahisi chakula hicho kufaa kuliwa tena.