https://jaridahuru.blogspot.com/2014/06/bungeni-lowassa-mbowe-waunganisha-nguvu.html
KIONGOZI Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, wameikosoa Serikali ya Rais Jakaya
Kikwete, wakisema kuwa ajira kwa vijana ni bomu linalofanyiwa mzaha.
Hii si mara ya kwanza kwa Lowassa kuinyooshea kidole Serikali ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), japo mara zote amekuwa akibezwa kuwa anatumia
turufu hiyo kujijenga kisiasa wakati suala hilo si kubwa kiasi hicho.
Katika kampeni za kuingia madarakani mwaka 2005, Rais Kikwete
aliahidi kutengeneza ajira milioni mbili kwa vijana, ahadi ambayo hadi
sasa utekelezaji wake unatia shaka, kutokana na muda wake kufikia
ukingoni.
Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa
mwaka wa fedha 2014/15 bungeni juzi, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai
na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alisema suala la ajira linapaswa liwe
hoja maalumu bungeni kwa kuwa serikali imeshindwa kulipa kipaumbele.
Alisema ukosefu ajira ni janga la kitaifa, serikali haionekani
kushitushwa nalo na badala yake imekuwa ikifanya mikatati inayoishia
ngazi za juu.
Mbowe alifafanua kuwa jambo hilo linatakiwa liwekewe mikakati kuanzia ngazi za halmashauri, mikoa na serikali kuu.
Alibainisha kuwa kuongeza ajira si suala la kufumania bali ni mkakati maalumu unaoandaliwa na serikali.
Alisema tukio lililotokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa
vijana 11,000 waliokwenda kufanya udahili wa kupata nafasi 70 za ajira
za Idara ya Uhamiaji, ni ishara mbaya kwa mwelekeo wa taifa.
“Serikali haipo makini na ukosefu wa ajira, na sisi wabunge
hatulichukulii jambo hilo kwa ukubwa wake, vijana 11,000 wanawania
nafasi 70! Hii ni hatari,” alisema.
Aliongeza kuwa suala hilo limezungumzwa na watu wengi, akiwemo
kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM, lakini akaelezwa si kubwa kama
anavyolizua.
Mbowe alisema tatizo la ukosefu wa ajira limechangiwa na mfumo uliopo sasa wa kila kitu kurundikwa kwenye Serikali Kuu.
Alisema tatizo hilo lingepungua kama halmashauri zingekuwa na mkakati wa kuzitengeneza kwenye mazingira wanayofanyia kazi.
“Sioni haja ya kuwa na wataalamu wa uchumi na wakurugenzi katika
halmashauri kama hawawezi kutengeneza ajira…. Tutengeneze mfumo wa ajira
kuanzia ngazi za chini, serikali itoe agizo kwa halmashauri kutengeneza
ajira,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, miradi ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na
sekta ya umma (PPP) inaweza kulifanya taifa litengeneze kati ya sh
bilioni 500 hadi 800.
Madeni ya serikali
Kuhusu madeni, Mbowe alisema baadhi ya madeni ya taifa yanatokana na uzembe wa mawaziri na watendaji serikalini.
Kauli hiyo ameitoa juzi jioni bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mbowe alisema serikali imeliingiza taifa hasara ya sh bilioni tano
kutokana na kushindwa kuilipa kwa wakati kampuni inayojenga bomba la
gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Alisema ana barua za kutoka katika kampuni ya kujenga bomba la gesi
ambayo inakwenda katika Shirika la Umeme na Wizara ya Fedha inayodai sh
bilioni 5 kama riba na mkopo.
Kwa mujibu wa Mbowe, serikali haijailipa kampuni hiyo tangu Januari
mwaka huu, kama mkataba unavyosema, hivyo kuzua hofu ya kukamilika kwa
wakati kwa mradi huo.
“Jamani madeni mengi ni ya kujitakia tu… ni uzembe tu hapa,
tumeingizwa kwenye deni la sh bilioni tano kwa sababu ya wizara
imeshindwa kuilipa kampuni hii.
“Tuna kila sababu kuangalia deni hili la taifa linasababishwa na nini
ili tuangalie namna bora ya kulishughulikia na kuwashughulikia wale
wote wazembe,” alisema.
Lowassa aibuka
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM, katika mchango
wake alisema mara kwa mara alikuwa akitahadharisha kuwa ajira ni bomu,
lakini watu hawakumuelewa.
Alisema sasa bomu hilo linaanza kupasuka taratibu na kuwa serikali inatakiwa kutengeneza ajira kwa vijana.
Kwa mujibu wa Lowassa, idadi ya Watanzania ni milioni 48 na kila
mwaka wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya 40,000, lakini hakuna
ajira.
Alisema ni lazima taifa liwe na mkakati wa kitaifa wa kuwasaidia vijana kwa kutengeneza ajira.
Lowassa aliongeza kuwa ujenzi wa kiwanda chochote ni vema ukaangalia utazalisha ajira kwa kiwango gani.
Alibainisha kuwa Rais Barak Obama wa Marekani, ni miongoni mwa
viongozi walioingia madarakani kwa awamu ya pili baada ya kutengeneza
ajira.