jaridahuru

Mitandao

KITAIFA: MBOWE ADAIWA KUTAPELI ZAIDI YA TSH MILIONI 1,200 NSSF, KIBALI CHA KUMKAMATA CHATOLEWA


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, anakalia kiasi kikubwa cha fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa kukataa kulipa deni alilokopa.

Mbowe anadaiwa wastani wa sh milioni 1200 (sh bilioni 1.2), kutokana na deni alilochukua mwaka 1990 kwa nia ya kufanya upanuzi wa Mbowe Hotel ya jijini Dar es Salaam, maarufu kama Bilcanas.
Kwa kutumia mamilioni aliyokopa kutoka NSSF Machi 10, mwaka 1990, Mbowe aliweza kupanua Mbowe Hotel kwa kujenga mgahawa wa Hard Rock, kumbi za Bilcanas, Much More na Sugar Mama, ambazo amekuwa azitumia kwa ajili ya biashara tangu wakati huo.

Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa deni la mkopo huo aliouchukua kwa kutiliana saini kati yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NPF), ambalo baadaye lilibadilishwa jina na kuwa NSSF, sasa limekua na kufikia zaidi ya sh milioni 1200. Deni hili linatokana na mkopo aliouchukua na riba inayotokana na deni hilo.
Wakati wa kuchukua mkopo huo NPF (wakati huo) iliwakilishwa na Mustafa Mkulo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, huku Mbowe Hotel ikiwakilishwa Mbowe mwenyewe aliyetia saini. Pande zote mbili zilikuwa na mwakilishi mmoja. Mkulo aliwai kuwa Waziri wa Fedha.

Kwa mujibu wa mkataba wa mkopo kati ya Mbowe na NSSF, ambayo ilichukua majukumu ya NPF, Mbowe Hotel ilikopeshwa sh milioni 15, mwaka 1990. Ibara ya 5, ya Mkataba wa Mkopo kati ya Mbowe Hotel na NSSF yenye vifungu 5.01, 5.02 na 5.03, iliweka bayana kuwa riba ya mkopo huo ilikuwa asilimia 31, na kwamba kila mwaka iwapo riba isingelipwa kwa wakati nayo ingetozwa riba ya asilimia 31.

Kifungu cha 6.01 na 6.02 cha mkataba wa mkopo huo kati ya Mbowe na NSSF vinaeleza kuwa Mbowe Hotel ilitakiwa kulipa deni hilo kwa mikupuo sawa mitano katika kipindi cha miaka sita. Mwaka wa kwanza wa mkopo Mbowe Hotel haikutakiwa kulipa kitu kwa nia ya kuipa fursa ya kujiimarisha katika biashara kwa mwaka wa kwanza.
Malipo hayo yalipaswa kufanyika kila ifikapo Desemba 31, kuanzia mwaka 1991, ambapo kila mwezi alistahili kulipa sh 3,000,000 kama deni la msingi na riba ya asilimia 31 kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba.

Wakurugenzi wa Mbowe Hotel, Manase A. Mbowe, Freeman Aikaeli Mbowe na Dk. Lilian Mtei Mbowe, kwa sababu wanazozijua wao waliamua kuacha kulipa deni hilo bila mawasiliano ya aina yoyote na NSSF wala juhudi za wazi za kuonyesha nia ya kulipa hadi mwaka 1993, walipoamua kulipa sh 3,000,000 kati ya deni lote.

Kwa mujibu wa mkataba wa mkopo, hadi mwaka 1993, wakurugenzi hao walistahili kuwa wamelipa wastani wa sh milioni 9,000,000 katika deni la msingi, lakini walikaa kimya hali iliyolitia wasiwasi shirika la NSSF.

Baada ya kutoa malipo ya sh 3,000,000, wakurugenzi hao walikaa kimya na ilipofika Septemba 1996, NSSF iliamua kufungua kesi Mahakama Kuu. Kesi hiyo ya madai No. 277 ya mwaka 1996, ilikuwa ikidai Mkopaji alipe deni la msingi sh milioni 12 zilizokuwa zimesalia pamoja na riba.

Hatua hii iliwafanya wakurugenzi wa Mbowe Hotel kuomba suala hilo walimalize nje ya Mahakama. Hata hivyo, hawakuendelea kulipa hadi mwaka 1998, walipopewa tishio la kufungwa jela ndipo waliamua kulipa kwa mkupuo sh milioni 12.

Hadi wanatoa malipo hayo, deni lilikwishakuwa na kufikia wastani wa sh milioni 145.38, na kimsingi makubaliano ilikuwa ni kwamba deni hilo lingelipwa katika muda wa miezi 24 tangua tarehe ya makubaliano.

Hata hivyo, Mbowe na wakurugenzi wenzake waliamua kutoendelea kulipa deni hilo badala yake wakaamua nao kuchukua mkondo wa kisheria kwa kutumia wahasibu kukokotoa tena hesabu za riba, bila mawasilianao na NSSF, na kisha wakachagua kiasi wanachotaka kulipa wao.

Mbowe Hotel ikitumia kampuni ya uwakili ya Nyange, Ringia & Co., walifanya kazi ya kuwasiliana na wahasibu mbalimbali kisha kuwasiliana moja kwa moja na wakili wa NSSF, Ademba Gomba, kutaka deni la riba lipunguzwe.
Mgogoro na mvutano kati ya Mbowe Hotel uliendelea, huku riba ya deni nayo ikizidi kuongezeka na ilipofika Oktoba 11, 2002 Meneja wa Fedha wa Bilcanas Group Inc, Godbless Naftal, kupitia barua yake yenye Kumb. No. BGI/NSSF/MHL02/02/01, alikokotoa hesabu na kutaka wakurugenzi wa Mbowe Hotel walipe wastani wa sh 31,959,369.86, kwa maelezo kuwa kanuni iliyotumiwa kukokotoa riba ilikosewa.

Januari 16, 2003 NSSF kupitia kwa Mussa S. A. kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alimjibu Naftal kwa barua yenye Kumb. No. NSSF/LA/F.131/10/89/135, akimweleza kuwa NSSF imekataa mapendekezo yake (Naftal) na hivyo wanapaswa kulipa deni lote kwa mujibu wa hukumu ya za Mahakama Kuu za mwaka 1999 na 2001.

NSSF na Mbowe Hotel waliendelea kupigana ngwala mahakamani na kwenye bodi za usuluhishi hadi ilipofika Oktoba, 2006 ambapo Jaji Manento alihukumu wakurugenzi wa Mbowe Hotel watiwe mbaroni na kufungwa jela kwa kushindwa kutekeleza amri ya mahakama ya kulipa deni lao.

Wakili wa Mbowe Hotel, Herbert Nyange, aliwasilisha katika Mahakama ya Rufaa hati ya kiapo ambayo muhuri wake umegonjwa Oktoba 30, 2006 akipinga wakurugenzi wa Mbowe Hotel kukamatwa kwa maelezo kuwa Mahakama Kuu ilikwenda nje ya mipaka kisheria kwa kutaka wakurugenzi wakamatwe.

“Uamuzi wa amri ya kukamatwa kwa walalamikaji (wakurugenzi wa Mbowe Hotel) ulifikiwa kwa misingi ya wazi ya uvunjaji wa kanuni juu ya wajibu wa wakurugenzi dhidi ya deni au uamuzi dhidi ya shirika, hivyo ni kinyume na sheria,” alisema Nyange katika barua hiyo ya kupingwa kukamatwa kwa akina Mbowe.

Hata hivyo, kutokana na Mbowe kuona mambo yanaendelea kuchacha, Desemba 14, mwaka 2006, mmoja wa wakurugenzi wa Mbowe Hotel, Dk. Lilian Mtei Mbowe, aliamua kutoa malipo ya wastani wa sh milioni 50 kwa NSSF kwa hundi mba 298492, iliyoambatana na barua yenye Kumb. No. BGI/NSSF/MHL06/01, huku akitaka warejee kwenye meza ya majadiliano badala ya kufungwa jela.

Barua hiyo pia iliomba NSSF irejee barua ya Kampuni ya Ushauri wa Fedha ya Morgan cKlien Associates iliyoteuliwa na Mbowe mwaka 2004 kushiriki majadiliano na usuluhishi juu ya jinsi ya kulipa deni hilo.

Kampuni hiyo iliyokuwa chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Hubert Mengi, ilitoa maelezo mengi yenye kuonyesha kwa nini Mbowe Hotel ilishindwa kulipa deni lake kwa wakati. Anasema katika moja ya vielelezo kuwa fedha zilipotolewa na NSSF mwaka 1990, nchini Tanzania hakukuwapo vifaa vya ujenzi.Mengi anaeleza kuwa Mbowe Hotel walilazimika kuagiza vifaa vya ujenzi kutoka nje ya nchi, na lilijitokeza tatizo lingine kwamba benki nchini hazikuwa na fedha za kigeni, hivyo Mbowe Hotel ililazimika kusubiri kwa muda mrefu kupatiwa fedha hizo za kigeni.

Kwa maelezo hayo, anasema Mbowe Hotel walichelewa kupata vifaa na mradi ukashindwa kukamilika kwa wakati hali iliyosababisha wakurugenzi wake washindwe kulipa deni hilo kwani walikuwa hawafanyi biashara.
Baada ya mivutano yote hiyo, Mbowe Hotel wamealikwa kwenye NSSF kujadili jinsi ya kulipa deni hilo linaloendelea kukua lakini hadi jana vyanzo vyetu kutoka NSSF vilionyesha kuwa wakurugenzi wa Mbowe Hotel wameamua kukaa kimya.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi NSSF inaendelea kupoteza mapato yake yanayokaliwa na wakopaji wa aina hiyo, ambapo mwenendo usipodhibitiwa shirika linaweza kufilisika sawa na ilivyotokea kwa mashirika mengi nchini

CHANZO:GEMBE

Related

Kitaifa 3667850742869073289

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item