jaridahuru

Mitandao

BUNGENI: BAJETI YA YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YAPITISHWA, MAKAZI YA ASKARI NA POSHO SASA KUBORESHWA


MFUKO maalumu wa kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha makazi ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiwemo askari, umeanzishwa ukilenga kuwezesha kupata nyumba na ofisi zaidi bila kutegemea bajeti ya serikali.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ambaye bajeti ya wizara yake iliidhinishwa juzi, alitoa taarifa hiyo wakati akihitimisha mjadala kuhusu bajeti ya wizara yake.
Katika mjadala, wabunge wengi walichangia kutaka maslahi, makazi na ofisi za askari polisi, magereza na uhamiaji yaboreshwe kuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Bunge liliidhinisha bajeti ya Sh 881,740,291,800 kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Chikawe alisema, “tumeona tusitegemee bajeti ya Hazina (Serikali).” Alisema mfuko ulioanzishwa, ambao bodi yake imeshazinduliwa ikiwa chini ya mfanyabiashara maarufu Ali Mufuruki, unalenga kukusanya fedha kutoka kwa wanajamii kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi na askari wa wizara hiyo.

Waziri, ambaye alikiri nyumba za askari katika mikoa mbalimbali kuwa duni na kusema hali hiyo haipendi, alisema mpango huo uliofikiriwa na wizara ni wa uhakika kuliko mipango mingine iliyowahi kubuniwa.

Alisema chini ya mpango huo, watahakikisha nyumba chakavu zinaondolewa kwa kujenga mpya.
Aliahidi kukaa na waziri kivuli wa wizara hiyo kutoka upinzani, Godbless Lema ili hafla ya uchangiaji chini ya mfuko huo ianzie Arusha kabla ya kwenda kwenye majiji mengine ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.

Akizungumzia posho ya askari ya Sh 5,000 ambayo wabunge walilalamikia kwamba haitoshi na badala yake iongezwe hadi Sh 7,500, Chikawe alisema wako kwenye majadiliano na Hazina kuwezesha posho hiyo ifike Sh 8,000.
Aidha alisema majadiliano mengine yanayoendelea na Hazina, ni ya kuwezesha posho ya chakula ya wafungwa itoke Sh 500 kwa siku hadi Sh 3,000. Chikawe alikiri posho hizo za askari na wafungwa ni ndogo.

Alisema kwa wafungwa, wanapokuwa wengi kiasi cha posho hushuka chini ya Sh 500. Tatizo lingine linalokabili wafungwa ni ukosefu wa sare.
Alisema hawajamudu kuwezesha kila mfungwa kuingia jela akiwa na sare yake badala yake, husubiri mfungwa anayeondoka kumwachia anayeingia.

Hata hivyo, alisema bajeti ya mwaka huu itatosheleza kununua sare. Aidha kwenye maeneo ya baridi, serikali haijamudu kununua nguo nzito za kukabili hali hiyo ya hewa.

Chanzo:Habari leo

Related

Habari Kuu 7611046682962774485

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item