JAMII: BAAADA YA KISA CHA MTOTO WA BOKSI, KICHANGA CHAFANYIWA UNYAMA WA KUTISHA NA MAMA YAKE MZAZI
https://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/jamii-baaada-ya-kisa-cha-mtoto-wa-boksi.html
WAKATI tukio la kusikitisha la kifo cha ‘Mtoto wa Boksi’ likiendelea
kutanda kwenye vichwa vya Watanzania, mwanamke mwingine, Fadhila
Bakari, mkazi wa Keko Machungwa, Mtaa wa Championi, amefanya unyama wa
kutisha kwa kutaka kumuua mwanaye muda mfupi baada ya kujifungua.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa Fadhila anayefanya kazi ya
mama lishe, alijifungia chumbani kwake na kujifungua mtoto huyo juzi na
kuanza harakati za kutaka kumuua.
Walisema kuwa walisikia sauti ya mtoto mchanga kutoka chumbani kwa
mwanamke huyo, lakini walipomfuata na kumuuliza kulikoni, Fadhila
ambaye alikuwa anaficha kama ni mjamzito, aliwajibu kwamba hakuna
tatizo.
“Mimi ndiye nilikuwa wa kwanza kusikia sauti ya mtoto ikitoka
chumbani kwa Fadhila. Ingawa mwenyewe alikuwa anaficha kama mjamzito,
lakini tulihisi kama mjamzito, kwa hiyo nilidhani uchungu umempanda,
niende nikamsaidie,” alisema mwanamke huyo na kuongeza.
Lakini nilipofika mlangoni, nilimuita na kumuuliza vipi, akanijibu
hakuna tatizo. Jibu lake halikuniridhisha, nikamuita mpangaji mwenzangu
na tukaanza kufanya utafiti. Tulimuita ndugu yake anayeishi nyumba ya
jirani, alipokuja tulimueleza, lakini alipomgongea afungue alikataa.
“Ndugu yake huyo aliondoka na kwenda kumuita dada yake na walipokuja
walimkuta kafungua mlango, lakini alipowaona, akataka kuufunga, lakini
walimzidi nguvu na kuingia ndani,” alisema.
Jirani huyo alisema kuwa walipoingia ndani waliona michirizi ya damu
kutoka mlangoni ambako wanahisi ndiko alikojifungulia, ikielekea kwenye
kona ya chumba hicho ambako kulikuwa na malundo ya nguo na mifuko ya
rambo.
“Dada yake alijaribu kutafuta lakini hakuona, ndipo mpangaji mwenzetu
alipoingia ndani na kwenda kwenye lile rundo la nguo na alipotoa,
tukamkuta mtoto amelazwa kifudifudi, tulipomgeuza, akawa anapumua kwa
tabu.
“Kitu cha kwanza tulichofanya ni kumpa huduma ya kwanza, kwa kumkata
kitovu, kisha tukamchukua yeye na mama yake na kumpeleka Kituo cha
Polisi Kilwa Road, ambako mama huyo ameshikiliwa na mtoto anapatiwa
huduma kwenye hospitali ya Polisi Barracks,” alisema.
Jirani mwingine, Andrew Kisalu, alisema kuwa kabla ya kumpeleka
hospitali, walimfanyia uchunguzi mtoto huyo na kugundua amevunjwa mguu
mmoja, huku akiwa na michubuko usoni kutokana na kuburuzwa na mama yake
kutoka mlangoni hadi kwenye kona aliyokwenda kumficha.
“Yule mwanamke alijifungulia mlangoni, sasa inaonekana alimburuza
kutoka mlangoni hadi kwenye kona kabla ya kumvunja mguu mmoja,” alisema
Kisalu.
Wakizungumzia tukio hilo, wakazi wa eneo hilo walisema kuwa
wameshangazwa na ujasiri wa mwanamke huyo wa kujifungua bila ya kuomba
msaada kwa mtu, lakini wamesikitishwa na ukatili alioufanya wa kutaka
kumuua mwanaye.
“Inaonekana alidhamiria kufanya tukio hili, ndiyo maana alikuwa
anaficha kama ni mjamzito. Alitaka kujifungua kimya kimya na kumuua,”
alisema.
Kituo cha Polisi Kilwa Road, kimethibitisha kutokea kwa tukio hilo,
lakini wamekataa kuzungumzia lolote kwa kuwa wao si wasemaji wa Jeshi la
Polisi.