jaridahuru

Mitandao

KITAIFA: DR. BILAL AWAAGIZA UKAWA KURUDI KWENYE MSTARI, WAACHE KUKAIDI NA KUFUATA MISINGI YA JAZBA




MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal amewatoa hofu Watanzania wanaoishi nchini hapa kuhusu mvutano uliojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba na kuwahakikishia kuwa ana imani litakapokutana Agosti mwaka huu mambo yatakwenda vizuri.


Dk Bilal amewaeleza hayo Watanzania hao baada ya risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo (Tanzanite Society), David Semiono kueleza masikitiko yao kuhusu kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.

Akizungumza na Watanzania hao mjini hapa jana, Dk Bilal alisema kilichojitokeza katika Bunge hilo ni kurekebishana ili nchi ipate Katiba mpya yenye maslahi kwa wananchi na itakayomudu kwa miaka mingi ijayo.

Dk Bilal alisema kazi ya kuandika Katiba si rahisi kama inavyofikiriwa kwani katika nchi nyingine, uamuzi hufikiwa baada ya kutokea kutoelewana na hata kupigana jambo alilosema Tanzania si rahisi kwa kuwa inaheshimu maoni ya wananchi wake.

Aliutaka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuacha jazba na kurudi bungeni ifikapo Agosti mwaka huu ili waweze kushirikiana na wenzao katika kukamilisha kazi hiyo muhimu waliotumwa na wananchi.

“Tunachoomba waliotoka nje ya mstari, tusiwe wa kwanza kukaidi na kufuata misingi ya jazba. Tutangulize Utanzania wetu, naomba wote waliotoka bungeni, warudi, tukimaliza kwa amani mchakato huu, tutaijengea sifa kubwa nchi yetu, sote tuheshimu mchakato hadi mwisho wa amani,” alisema Dk Bilal.

Akizungumzia Muungano, Dk Bilal aliwataka Watanzania hao kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla, huku akiwakumbusha kuwa Muungano huu umekuwa wa mfano Afrika na duniani kwa ujumla.

Akijibu malalamiko ya Watanzania hao kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haiwatendei haki wafanyabiashara wanaoingiza magari nchini kwa kutoza kodi zenye utata, Dk Bilal alisema amelipokea tatizo hilo, na kueleza kuwa Serikali inazifanyia kazi kero mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo.

Aliwataka Watanzania hao kuwa wavumilivu kwani jambo huanza kwa hatua moja na kuwahakikishia kwamba anaamini kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kero hizo zitapatiwa ufumbuzi haraka.

Kuhusu ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, Dk Bilal aliiasa jamii na viongozi wa dini mbalimbali nchini kushirikiana na serikali kwa kuwapa miongozo ya maadili mema vijana ili kuepukana na janga hilo.

“Tusifanye mzaha katika malezi ya watoto wetu, viongozi wa dini zote nchini wana wajibu wa kuwafundisha vijana wetu maadili mema na sisi wazazi tusichoke kuwakanya vijana wetu kwa ukali kuhusu matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Dk Bilal.

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo pia kuhimiza Watanzania kutumia nafasi yao ughaibuni kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nyumbani kwani Tanzania haiwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji wa kutosha.

Chanzo:Habarileo

Related

Kitaifa 1377922403461445462

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item