KITAIFA: BIBI AKAMATWA UWANJA WA NDEGE DAR ES SALAAM NA DAWA ZA KULEVYA
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/kitaifa-bibi-akamatwa-uwanja-wa-ndege.html
Dar es Salaam. Bibi mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole
(65) amevunja rekodi ya umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za
kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82
aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na
ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana katika mitambo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa
Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja
na mbinu zake na kujiamini, mwanamke huyo alikamatwa kutokana na
ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya uwanja wa ndege.
Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi
Selemani alisema mwanamke huyo alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa
alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege
la Ethiopia.
Selemani alisema raia huyo aliwasili nchini Mei
15, mwaka huu na alikaa muda wote bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo
ambalo lilitiliwa shaka na kumkamata.
“Huyu mwanamke achana naye, akisimama mbele yako
huwezi ukaamini kwa jinsi anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya
kufunga hizo kete. Kila moja ilifungwa kwa karatasi inayofanana na ganda
la sigara,” alisema Selemani.
Alisema mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake
ya ufungaji wa kete, mwanamke huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya
kwanza ya ukaguzi.
Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha
Kuthibiti Dawa za Kulevya kilibaini na kugundua kuwa alikuwa amemeza
dawa za kulevya.
“Huyu ni mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana
nguvu za kutosha na tulishangaa baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja
katika awamu ya kwanza, jambo hili si rahisi kutokana na umri wake,”
alisema Nzowa.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Nzowa alisema kikosi chake kimejipanga kukabiliana na mbinu zote zinazobuniwa na wanaosafirisha dawa za kulevya.
Takwimu za kitengo cha dawa za kulevya cha polisi
zinaonyesha kuwa kati ya Januari na Aprili mwaka huu, Cole ni mtu wa 26
kukamatwa katika uwanja huo na raia wa tano wa kigeni kukamatwa na dawa
hizo.
Raia wa kigeni wengine waliokamatwa kutoka nje ya nchi ni kutoka Marekani, Ugiriki, Kenya na Liberia na kesi zao zinaendelea.