TEKNOLOJIA: JE UNAFAHAMU KAMA TAARIFA ZAKO ZA MATUMIZI YA SIMU ZIKO SALAMA? JE MITANDAO YA SIMU INA USIRI?
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/teknolojia-je-unafahamu-kama-taarifa.html
Ukikutana na Watanzania 10 angalau nusu yao watakuwa na kifaa au vifaa vya mawasiliano kama simu na kompyuta.
Vifaa hivi vimesajiliwa kwa majina yao na taarifa zao nyingine ambazo zinaweza kuwa ni taarifa sahihi au la.
Kwa kawaida wakati wa usajili wa laini za simu au
vifaa vingine vya mawasiliano, kuna jambo ambalo mara nyingi
linasahaulika kati ya mteja wa huduma za mawasiliano na mtoa huduma
yaani kampuni husika.
Wateja wengi wa kampuni za mawasiliano hawajui
taarifa zao zinatumikaje na hata pale wanapohitaji baadhi ya taarifa,
ni vigumu kupata labda kutokee tatizo na kuhusishwa vyombo vya dola kama
jeshi la Polisi.
Mimi binafsi niliwahi kuuliza maswali kadhaa kwa
watoa huduma wa mawasiliano yangu. Niliwauliza: Taarifa zangu
zinahifadhiwa wapi na kwa njia gani na nani mwenye uwezo wa kuangalia
taarifa zangu?
Maswali mengine ni; kwanini sina haki ya moja
kwa moja kujua taarifa hizo mpaka polisi ihusishwe na kwanini nikitaka
kujiondoa kwenye huduma, kampuni zina uwezo wa moja kwa moja kuniruhusu?
Ukweli ni kuwa mawasiliano ya watu wengi
yanaangaliwa na wanapewa watu wengine bila ya sisi kujua au kujulishwa.
Tena utashangaa muda mwingine mtu unakamatwa kumbe aliyetoa taarifa ni
mtoa huduma wako.
Kuna watu wanatumiwa ujumbe mfupi wa maneno na
kampuni mbalimbali kupitia mtoa huduma wako, bila mwenye namba ya simu
kujulishwa. Na ikitokea anataka kujiondoa basi atakatwa fedha kidogo,
hajitoi bure .
Wengine husafiri kwa kipindi kirefu, wanaporudi
wanashangaa namba zao za simu zinatumiwa na watu wengine. Hili
linafanyika ikiwa tayari walishazisajili namba zao.
Natambua nchi yetu iko kwenye mchakato wa kuandaa
sheria ya mawasiliano. Sheria hii itakuwa kioo cha masuala yote ya
mawasiliano nchini, hivyo ni muda mwafaka wa kuangalia suala hili kwa
maslahi ya wateja wa huduma za mawasiliano .
Kwa nchi nyingine zilizoendelea masuala haya
walishayafanyia kazi, kwa sababu kuna wateja waliwahi kuzipeleka
mahakamani baadhi ya kampuni za mawasiliano na kushinda mashauri yao.
Nchi kama Marekani kampuni ya mawasiliano
inatakiwa kutoa taarifa kwa mteja wake endapo inataka taarifa yoyote
inayohusu kifaa chake cha mawasiliano.
Aidha, mteja anapohitaji kujiondoa kwenye huduma fulani,
anapewa utaratibu wa kufuata na mara nyingi ni kwa njia ya mtandao.
Kampuni kama Yahoo kwa kawaida inakupa siku 90 ili wakamilishe ombi lako
la kujiondoa.
Siku 90 hizi ni kuangalia kama kila kitu ni
salama kuhusu akaunti ya mteja. Ikiwa watajiridhisha kuwa kila kitu
kitakuwa shwari, utaondolewa katika huduma zao.
Kwa kuwa huduma za mawasiliano ni haki ya raia
wote, suala la taarifa zake anazotoa kwa kampuni za mawasiliano bila
shuruti nazo ziwe haki yake.
Kimsingi nihitimishe kwa kusema mteja lazima awe
na uwezo wa kuhoji na kupata ufafanuzi wa taarifa zake. Lakini muhimu
zaidi awe na uwezo wa kujiondoa kwenye huduma au kampuni fulani bila
usumbufu.
Mwandishi ni mtaalamu wa mifumo ya udhibiti wa uhalifu wa kwenye mitandao.