ELIMU: MFAHAMU PIUS MSEKWA, MTANZANIA MWENYE ELIMU NA UJUZI USIOTIA MASHAKA
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/elimu-mfahamu-pius-msekwa-mtanzania.html
Wakati Tanzania inapata uhuru wake mwaka 1961, haikuwa na wasomi wengi ila wa kuhesabu, hasa wa ngazi ya chuo kikuu.
Mmoja wao, ni spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Chipanda Msekwa.
Kama ilivyokuwa kwa wasomi wenzake wengi wakiwa wamepitia Chuo Kikuu cha Makerere, hakuwa kando katika uongozi wa nchi.
Akiwa mwanafunzi mtiifu wa Mwalimu Julius Nyerere
tangu wakiwa Pugu, alijikuta akikabidhiwa majukumu ya kuwa mmoja wa
watendaji muhimu wa serikali ya Tanganyika huru na chama cha TANU.
Ukiondoa kazi ya Ukatibu wa Bunge aliyoanza mwaka
1960 akiwa na miaka 25, mwaka 1967 akiwa na umri wa miaka 32 aliteuliwa
kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU.
Kwa umri na elimu yake huo ulikuwa muda wa kuifaidi dunia, achilia mbali kufanya kazi za kuutumikia umma.
Kwa vijana wa sasa, hicho ndicho kipindi cha kupupia maisha badala ya utumishi uliotukuka kwa umma.
Miaka zaidi 50 ya utumishi wa umma na kama
mwanasiasa, Msekwa ambaye ni msomi mwenye weledi mkubwa katika
historia, sayansi ya siasa, uongozi wa umma na sheria ya katiba na
utawala, anasema hakufikiria kutumia madaraka yake kwa maslahi binafsi,
seuze kutapanya mali ya umma.
Mfano mzuri wa urithi ambao vijana wa sasa hawana
budi kujifunza kwake ni namna alivyokubali nyumba yake binafsi iliyopo
kisiwani Ukerewe kutumiwa na viongozi wa juu nchini bila kudai chochote
kwa serikali.
“ Ni nyumba nzuri...wakubwa wote wakienda
wanafikia kwangu, maDC ma RC wote wanajua hivyo, wanalala bure tu ni
wageni wangu, sitaki kujilimbikizia mali, ‘’ anaeleza.
Msekwa anajua kulipa fadhila kwa jamii hasa
akikumbuka kuwa mafanikio yake kielimu yalitokana na msaada wa wasamaria
wema waliomsaidia baada ya baba yake kufariki dunia.
Tarikhi yake inaonyesha baada ya baba yake
kufariki akiwa darasa la tano, alipata udhamini na mfanyabiashara mmoja
mwenye asili ya bara la Asia mpaka alipomaliza shahada ya kwanza katika
Chuo Kikuu cha Makerere.
“Niliguswa sana na wema huo, niliendelea kukumbuka na kuenzi
kitendo chake hicho wakati wote…. Kwa ajili hiyo baadaye sana katika
maisha yangu nilipokuwa nimepata uwezo wa kufanya hivyo, nilihamasika
kuwatendea watu wengine wema kama huo, anasema katika kitabu chake
kiitwacho ‘Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Nyerere’.
Anaongeza kusema kuwa fadhila zaidi kwa jamii
alitoa alipokuwa Spika wa Bunge alipoamua kujenga shule ya sekondari
katika kijiji alichozaliwa, Bugombe kisiwani Ukerewe na baadaye
kuikabidhi kwa serikali. Shule hiyo inajulikana kwa jina la Pius Msekwa
Secondary School.
Maisha ya shule
Tangu akiwa ngazi za chini za elimu hadi chuo
kikuu, alidhihirisha uwezo mkubwa wa kuyakabili masomo ikiwamo lugha ya
Kiingereza aliyoimudu barabara.
Kwa mfano, alipokuwa sekondari alipewa tuzo ya
tabia njema na bidii katika masomo. Darasa la 12 alifaulu kwa kiwango
cha daraja la kwanza mtihani uliojulikana kwa jina la Cambridge School
Certificate na hivyo kupata fursa ya kuchaguliwa kusoma katika Chuo
Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Akiwa chuoni hapo aliendelea kudhihirisha ‘ukali’
wake katika masomo kwa kushinda zawadi ya fedha baada ya kuibuka mshindi
katika uandishi wa insha katika somo la Uchumi.
Aidha, alipokuwa Makerere ndipo alipoanza kupata
uzoefu wa uongozi kwa kuchaguliwa kuwa katibu mkuu chama cha wanafunzi
wa chuo hicho.
Akiongoza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Kuanzia mwaka 1970 hadi 1977 alikuwa Makamu Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, fursa anayosema ilimwezesha kwa kiasi
kikubwa kumtumia Mwalimu Nyerere kwa ushauri wa namna bora ya kuendesha
chuo hicho.
Anasema alikiongoza chuo hicho katika kipindi
ambacho wanafunzi walikuwa wachache na waliochaguliwa kwa malengo
maalumu ya utumishi wa umma. Ndiyo maana kila aliyemaliza alikuwa na
uhakika wa ajira.
Msekwa ameacha historia ya aina yake chuoni hapo
kwani wakati akiiongoza taasisi hiyo iliyosheheni wasomi mahiri,
hakusita kuomba nafasi ya kusomea shahada ya uzamili. Aliamua kuwa
mwanafunzi wa wale aliokuwa akiwaongoza.
Kwa mujibu wa kitabu chake hicho, uamuzi wa kusoma
katika chuo alichokuwa akikiongoza anasema ulitokana na ushauri wa
Mwalimu Nyerere aliyemwambia: ‘’ Wewe kiongozi wa wasomi na walio wengi
zaidi miongoni mwao ni wanafunzi. Kwa hiyo ukiamua kuwa mwanafunzi
utafanana nao.’’
Mwandishi wa vitabu
Msekwa ni mmoja wa viongozi wachache nchini wenye
mapenzi na sanaa ya uandishi, Ameandika vitabu zaidi ya saba baadhi
vikiwa vinatumika kama rejea katika taasisi za elimu ya juu.
Baadhi ya vitabu hivyo ni Essays on The Transition
to Multi-partism in Tanzania (1995), 50 Years of Independence: A
concise Political History of Tanzania (2013), Reflections on Tanzania’s
multi-party Parliament (2000) na Uongozi na utawala wa Mwalimu Julius
Nyerere: Miaka 25 ya utumishi wa umma chini ya uongozi wa Mwalimu Julius
Nyerere.
Vingine ni Towards Party Supremacy (1977),
Education Policy Formation Before and After the Arusha Declaration
(1979), Parliament Privilege in Tanzania (2003) na Insha za ufafanuzi wa
baadhi ya masuala ya chama (1982).
Wasifu wake
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo katika kitabu
chake, ‘Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Nyerere: Miaka 25 ya
utumishi wa umma chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Pius Msekwa
alizaliwa katika kijiji cha Bugombe wilayani Ukerewe mwaka 1935.
Elimu ya msingi alisoma katika Shule ya Msingi
Kagunguli wilayani humo na baadaye elimu ya sekondari katika shule za
Nyegezi, Mwanza na kilichokuwa Chuo cha Mtakatifu Francis (sasa
sekondari ya Pugu).
Alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu kishiriki cha Makerere alipohitimu Shahada ya Kwanza katika somo la Historia, Machi 1960.
Hadi anaamua kupumzika, Msekwa alifanya kazi
katika nafasi mbalimbali kama Katibu wa Bunge, Katibu Mtendaji Mkuu wa
TANU, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa
Chama cha Mapinduzi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Makamu Mwenyekiti wa CCM.