jaridahuru

Mitandao

SIASA: LOWASSA AANIKA 'MABILIONI' YAKE, ASEMA ANA MAMIA YA NG'OMBE HUKO MONDULI, AUWEKA WAZI UTAJIRI WAKE



Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema madai kwamba yeye ni tajiri hayana ukweli wowote. Amesema yeye ni mfugaji na anamiliki ng’ombe zaidi ya 800 katika Jimbo la Monduli, mkoani Arusha.


Lowassa alisema hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake wiki iliyopita mjini Dodoma.


 “Haya madai hayana hata chembe ya ukweli hata kidogo, isipokuwa mimi nadhani wananitakia mema kwa sababu ukiona jumba zuri wanasema la Lowassa, gari nzuri la Lowassa, kitu chochote kizuri wanasema cha Lowassa,” alisema na kuongeza:


“Wamesema uongo mwingi sana, mimi nasema tu nilichopata nimepata na sina utajiri kiasi hicho, lakini si mbadhirifu wa haki zangu ninazopata kama mshahara na haki nyingine.”

Alipotakiwa kutaja mali anazomiliki, Lowassa alisema: “Mimi ni mfugaji, nina ng’ombe zaidi ya 800 jimboni kwangu Monduli.”


Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alisema madai kwamba anamiliki utajiri uliopindukia yalianza kabla hajajiuzulu uwaziri mkuu na ilielezwa kuwa “maduka fulani” ni yake.

Alibainisha kuwa hata kampuni ya Alphatel ambayo wanamiliki kwenye familia yake iliwahi kuhusishwa na jengo kubwa lililojengwa na mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia wilayani Kinondoni, Dar es Salaam likiitwa Alpha.


“Ikaonekana ni jengo langu, kule Mbezi kuna rafiki yangu mmoja walienda watu wakasema hii nyumba ya Lowassa. Yule bwana alitoka na bastola akawakimbiza. Mimi sina nyumba maeneo hayo,” alisema Lowassa.


Bomu la ajira

Akitaja njia za kutegua ‘bomu la ajira’ kwa vijana ambalo amekuwa akisema liko mbioni kupasuka, Lowassa alitaja maeneo mawili ambayo yanapaswa kutazamwa ili kuzalisha ajira nyingi mpya.


Alitaja kilimo akisema kinachukua watu wengi nchini. Alisema kinapaswa kutengenezewa mazingira ili vijana wanaomaliza chuo kikuu wawe tayari kuishi kwenye mazingira ya kilimo.

Alitoa  mfano wa Misri kuwa mwanafunzi anapomaliza chuo kikuu hupelekwa Mto Nile na hupewa ekari tatu za kulima mizabibu, trekta na vyombo vingine na mkopo ambao huanza kuulipa baada ya miaka mitatu.

“Tangu akiwa chuo (mwanafunzi) anajua ajira yake ni kilimo na kwamba atapewa mazingira ya kufanya kilimo, si cha jembe la mkono ila kilimo cha kisasa, anakopeshwa na anawezeshwa,” alisema.

Kwa hapa nchini, alisema Serikali ingefanya uamuzi mgumu wa kutenga maeneo kama Kigoma, ichukue eneo la ekari milioni 10 ipandwe michikikichi (mawese) na kuwakabidhi vijana na baada ya miaka minne watakuwa wamepata mawese kwa ajili ya chakula na kuuza nje.

Alitaja eneo jingine ni Serikali kuanzisha viwanda ili ajira ziendelee.
“Tunaweza na sisi tukajenga kwa makusudi viwanda vya nguo ambavyo vinachukua ajira ya watu wengi au viwanda vingine tutakavyoona vinafaa vinavyochukua ajira ya watu wengi. Naliweka suala hili hadharani tulijadili,” alisema.

Lowassa, ambaye amekuwa akitajwa miongoni mwa wanasiasa wanaotaka kuwania urais, alisema: “Kama mabepari wanaendeleza sera za kijamaa kuokoa ajira zao na sisi tuendeleze sera hizo hizo kuokoa ajira za watu wetu. Utaniambia Serikali itatoa wapi fedha, jibu langu rahisi sana, tuna gesi. Mungu ametubariki.

“Tuna uhakika wa kupata trilioni 50 cubic metre. Unaweza kukopa kutokana na gesi uliyonayo ardhini na tukifanya hivyo tutakuwa tumetengeneza ajira nyingi za vijana.”

Alisema duniani kote vyama vya siasa vinapotaka kuingia madarakani huangalia masilahi ya watu wake, jambo gani la msingi ambalo chama kikiingia madarakani kitayafanya, likiwamo hili la ajira ambalo lipo karibu katika kila nchi na kila chama kinachoingia madarakani hulizungumzia.

“Labda niseme mfano mmoja, Mwalimu (Julius) Nyerere alipokuwa anaanzisha elimu ya kujitegemea mwaka 1967 alikuwa anaangalia ajira,” alisema.

Kwa nini analiita bomu? “Mimi sisemi tu ni bomu ila nasema ni bomu linalotarajia kulipuka wakati wowote, lakini ni bomu ambalo tunahitaji kulishughulikia. Lengo langu la kupiga kelele ni kuitaka jamii ishughulikie jambo hili.”
Alieleza kufurahishwa na matokeo ya kelele zake za ajira, kuwa ziliamsha wizara hadi kutoa takwimu na kila wizara ikatakiwa kuangalia kwenye eneo lake inatengeneza ajira kiasi gani.

Afya yake je?
Yamekuwapo madai kuwa afya yake inatetereka na kuwa alilazimika kwenda Ujerumani kutibiwa. Alipoulizwa alisema... “Hili ni kama lile la utajiri.”


“Watu wanapenda kunitakia afya mbaya. Kwani wewe unaionaje? Wanatunga tu naumwa, nikifanya mazoezi nikapungua kidogo wanasema huyu amepata stroke (kiharusi) amepelekwa Ujerumani. Lakini nataka nikuhakikishie kuwa afya yangu ni nzuri sana, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananipigania afya njema.

Lakini kwa nini amekuwa akionekana kwa TB Joshua Nigeria?... “Kila mtu ana uhuru wa kuamini na kushirikiana na imani anayofikiri inafaa. Namuona TB Joshua kama muumini na mwombaji mzuri ninayekubaliana naye katika vitu vingi, kwa hiyo nasikia faraja kwenda kwa TB Joshua na ninataka kuwahimiza watu wanaotaka kwenda, waende, ni mwombaji mzuri sana.”

Source:Mwananchi

Related

Siasa 9214932768997531393

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item