SINGIDA: Mgonjwa alazwa wodini miaka 45
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/singida-mgonjwa-alazwa-wodini-miaka-45.html
Mzee Lnajui akiwa hospitalini |
Sio utani, sijui ni kwa muda gani umewahi kukaa hospitalini lakini usiombe yakupate. Abdi Lanjui (75),
ametimiza mwaka wa 45 akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Singida
alikolazwa tangu mwaka 1971 baada ya kupata ajali ya lori.
Lanjui aliyekuwa dereva wa taasisi aliyoiita
“Mamlaka ya Pamba,” alipata ajali hiyo mkoani Mwanza baada ya lori
alilokuwa akiendesha kuchomoka gurudumu la mbele na kupinduka.
“Sababu ya mimi kugeuza wodi kuwa makazi yangu ya
kudumu ni ajali iliyosababisha kupooza kuanzia kiunoni hadi kwenye
nyayo. Kwa kuwa sinyanyuki kitandani, nimepata vidonda kuanzia makalioni
hadi miguuni. Kwa sasa naishi maisha magumu mno,” alisema.
Aomba msaada
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali na jamii
kwa jumla kumsaidia chakula kwa kuwa hana ndugu wa kumsaidia. Lanjui
ambaye hawezi kunyanyuka kitandani, alisema kwa miaka mingi uongozi wa
hospitali ya mkoa ulikuwa ukimhudumia kwa kumpa chakula lakini baadaye
huduma hiyo ilisitishwa, hivyo kumfanya awe ombaomba na maisha yake kuwa
ya mlo mmoja kwa siku.
“Kwa vile siwezi kunyanyuka kitandani na sina
ndugu yeyote, nimekuwa nikiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa
hapa hospitali. Nashukuru sana wamekuwa wakinisaidia bila kuchoka na
kuniwezesha kupata walau mlo wa siku moja,” alisema. Lanjui ambaye
anazungumza vizuri pia aliomba msaada wa fedha za kwenda Hospitali ya
KCMC, Moshi ili apatiwe huduma zaidi ya matibabu.
Mwanza hadi Singida
Lanjui aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika
hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali
ya Sekou Toure, Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali.
Alisema akiwa Sekou Toure mwishoni mwa mwaka 1970,
hali yake ilibadilika na kuwa mbaya ndipo alipomwomba mwajiri wake
amrudishe nyumbani katika Kijiji cha Mhintiri katika Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida ili ‘akasubiri kifo chake.’
Hata hivyo, alisema uongozi wa Mamlaka ya Pamba
ulikataa kumpeleka kijijini kwake, badala yake ulimkabidhi katika
Hospitali ya Mkoa wa Singida mwaka 1971.
Alisema wakati anapata ajali na kulazwa hospitalini, wazazi na ndugu yake wa pekee, walikuwa wamekwishafariki dunia.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Mussa Kamala
alisema hivi sasa mgonjwa huyo anahudumiwa na hospitali kama watu
wengine wenye ulemavu ambao hawatozwi gharama yoyote.
Alisema uongozi wa hospitali uliwahi kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mipango ya kumrudisha nyumbani, lakini haikuwezekana. Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Zuhura Kalya alisema walishindwa kumrejesha kwao kwani walipofuatilia ilibainika kuwa hana ndugu na hakukuwa na mtu anayemfahamu kwa sababu aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya uhuru.
CHANZO : MWANANCHI
Alisema uongozi wa hospitali uliwahi kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mipango ya kumrudisha nyumbani, lakini haikuwezekana. Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Zuhura Kalya alisema walishindwa kumrejesha kwao kwani walipofuatilia ilibainika kuwa hana ndugu na hakukuwa na mtu anayemfahamu kwa sababu aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya uhuru.
CHANZO : MWANANCHI