MAKALA : Wiki ya Elimu? Je Wadau wa Elimu wanasikilizwa?
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/makala-wiki-ya-elimu-je-wadau-wa-elimu.html
Hii ni Wiki ya Elimu Tanzania. Tanzania inaadhimisha Wiki ya Elimu kwa mara ya kwanza.
Lengo
la Wiki ya Elimu tunaambiwa kwamba ni kusherehekea mafanikio na
kujituma, pia kuwapatia motisha watu mbalimbali waliosaidia juhudi za
kuboresha elimu nchini wakiwamo wanafunzi, walimu na shule.
Kaulimbiu ya Wiki ya Elimu ni, “Elimu bora kwa wote inawezekana. Timiza wajibu wako.”
Kwa
jumla, uamuzi wa kuwa na Wiki ya Elimu Tanzania ni mzuri. Lakini
tukitaka kusema kweli (na lazima tuseme kweli), Wizara imekurupuka
kuanzisha Wiki ya Elimu.
Kwa
upande mmoja, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haikutoa taarifa
yoyote mapema kwa walimu na wanafunzi wao kwamba watakuwa na siku yao.
Wiki ya Elimu ni wiki ya walimu na wanafunzi wa shule. Kwa hivyo,
ushiriki wao katika wiki yao hii umekuwa mdogo sana!
Ajabu
ni kwamba Waziri wa Elimu alikuwa na maofisa wote wa elimu mjini
Morogoro miezi michache iliyopita. Mbona hakuwashirikisha jambo hili
zito? Ushirikishwaji unakosekana!
Lakini
kwa upande mwingine, Wizara haina chochote cha kusherehekea kipindi
hiki. Hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana katika sekta ya elimu
kiasi cha kufanya sherehe. Juu ya yote, Wizara haikujituma.
Kwa upande wa kaulimbiu ya Wiki ya Elimu, “Elimu bora kwa wote inawezekana. Timiza wajibu wako.”
Hapa
haijulikani nani anatakiwa atimize wajibu wake. Maana wanafunzi, walimu
na wazazi wanatimiza wajibu wao. Tatizo ni wizara yenyewe. Haitimizi
wajibu wake, wala haijitumi!
Kwa
kuwa matatizo ya elimu (ambayo yanaitwa changamoto) ni makubwa mno,
tulitazamia kwamba Wizara ingeshughulikia kwanza mambo mbalimbali
yanayopigiwa kelele. Baada ya hapo ingeanzisha Wiki ya Elimu kutafuta
kuungwa mkono baada ya Wizara yenyewe kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.
Katika mazingira hayo, umma wa Tanzania unashangaa Wizara inasherehekea mafanikio yapi na kujituma kupi!
Bado
watoto wetu wanamaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Sababu
iko wazi. Leo watoto wadogo, yaani wanafunzi wa darasa la kwanza na la
pili wanafundishwa masomo tisa! Wanafundishwa Hisabati, Kiswahili,
English, Sayansi, Tehama, Stadi za kazi, Haiba na Michezo, Kifaransa na
Dini!
Hawafundishwi
kusoma na kuandika. Ni kweli Kenya wanafunzi wa madarasa hayo
wanafundishwa masomo11, Burundi masomo 11, Rwanda masomo 10 na Uganda
masomo tisa.
Lakini
hatuwezi kulinganisha maendeleo ya elimu katika nchi hizo na yetu. Kule
kwa wenzetu Wizara ya Elimu inasimamia elimu kwa ufanisi na umakini.
Haisambazi vitabu vibovu shuleni, lakini pia kule wana vifaa bora vya
kufundishia kusoma na kuandika. Sisi huku masomo ya kusoma na kuandika
tumefuta kabisa!
Kwa
hiyo, haishangazi kusikia kuwa upimaji wa wanafunzi wa darasa la pili
uliofanyika katika halmashauri 20, umeonesha kwamba katika kila
wanafunzi 100 waliopimwa, wanafunzi 92 hawakuweza kusoma na kuelewa!
Katika
mazingira hayo, tunasherehekea nini? Wizara ifanye kazi kwanza ili
katika wanafunzi 100 watakaopimwa 92 waweze kusoma na kuandika. Ndipo
ianzishe upya Wiki ya Elimu ya kusherehekea mafanikio na kujituma.
Bado
wakaguzi wa shule hawatimizi wajibu wao wa kuendesha semina za masomo
wanayoyakagua. Badala yake wanakwenda shuleni kukaripia na kukemea
walimu kwa kufundisha vibaya masomo ambayo hawakuelekezwa namna ya
kufundisha vizuri!
Ni
jukumu la wakaguzi wote kuendesha semina za masomo yote. Lakini kuna
walimu wanakiri kuwa hawajahudhuria semina yoyote katika miaka kumi
iliyopita. Wanaletewa masomo mapya shuleni bila kufanyiwa semina.
Na
sasa umezuka mtindo mbovu sana. Walimu wanatakiwa wajiitishie semina
kwenye kata waziendeshe na waelekezane wenyewe! Hii haijatokea katika
nchi yoyote isipokuwa Tanzania. Tuseme wakaguzi wa shule hawana uwezo na
ujuzi wa kuendeshea semina za masomo wanayokagua? Kwa kweli sijaona
tunachosherehekea.
Bado silabasi zinazotumika kufundishia masomo mbalimbali hazikutungwa kwa ufanisi na zinavuruga walimu.
Chukua
kwa mfano, silabasi ya Historia darasa la tano. Mwalimu anatakiwa
afundishe utawala wa Wajerumani Tanganyika, Tanganyika chini ya utawala
wa Waingereza, utawala wa kisultani Zanzibar, mapambano ya Watanganyika
dhidi ya Wajerumani, na kadhalika. Silabasi hazikutungwa kwa mfululizo
unaomsaidia mwanafunzi kuelewa somo.
Huwezi
kufundisha utawala wa Waingereza Tanganyika kabla hujafundisha
mapambano ya Watanganyika dhidi ya Wajerumani. Pia huwezi kufundisha
ukoloni wa Wajerumani na Waingereza kabla ya utawala wa kisultani
Zanzibar.
Kana
kwamba ubovu huo haujatosha, bado kuna tatizo kubwa la vitabu
wanavyotumia walimu kufundishia masomo mbalimbali. Pamoja na Wizara
kutahadharishwa isisambaze vitabu shuleni bila kuanza kutafuta maoni ya
walimu walivyovitumia, Wizara imetumia vibaya fedha ya rada kwa
kusambaza vitabu vibovu shuleni.
Tatizo jingine ni hili: Walimu wanatumia vitabu vitatu au vinne katika darasa moja kwa somo moja, vyenye maelezo tofauti.
Chukua,
kwa mfano, mazao ya biashara yaliyomo katika Nembo ya Taifa. Oxford
University Press wanasema ni pamba na karafuu. Educational Books
Publishers wanasema ni pamba na kahawa.
Halafu
bado kuna tatizo la madawati. Inaonekana fedha ya rada iliyotengwa kwa
ajili ya kununua madawati imeyeyuka. Hatusikii madawati hayo
yamesambazwa wapi.
Kisha
bado kuna masomo ya Stadi za Kazi na Tehama ambayo yanawapotezea wakati
walimu na wanafunzi wao. Hakuna walimu waliopewa mafunzo ya
kufundisha masomo hayo na hayana vifaa vya kufundishia! Kwa hivyo,
lengo la masomo hayo kuwasaidia wanafunzi wanaorudi nyumbani kujiajiri
limepotea kabisa!
Vile
vile, bado masomo ya Historia na Uraia yaliyokusudiwa kuwajengea
wanafunzi uzalendo yameendelea kupuuzwa na Wizara! Kwanza, masomo hayo
yalifutwa kabisa! Yaliporejeshwa masomo hayo si tu yana vipindi vichache
zaidi shuleni bali katika Mtihani wa Taifa huulizwa maswali 14 wakati
masomo mengine huulizwa maswali 50.
Juu
ya yote, bado walimu wana madai yasiyo na idadi ambayo
hayashughulikiwi! Ni katika mazingira hayo tunaulizana Wizara
inasherehekea mafanikio yapi na kujituma kupi?
Sasa
basi, kwa kuwa katika Wiki hii ya Elimu, Wizara ya Elimu inasherehekea
kujituma tunaitazamia kwamba itaendelea kujituma kwa kuboresha
maandalizi ya Wiki ya Elimu ya mwaka 2015.
CHANZO: JAMHURI MEDIA