jaridahuru

Mitandao

KITAIFA: ASKOFU AISIFU KATIBA YA SASA, ASEMA KATIBA ILIYOPO INAWEZA KUENDELEA






WAKATI mchakato wa mabadiliko ya Katiba ukitarajiwa kuendelea katika ngazi ya Bunge Maalumu la Katiba Agosti mwaka huu, Askofu Mkuu mpya wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu, amesifu Katiba iliyopo kwa kuunganisha Watanzania kwa miaka 50.


Askofu Dallu aliyesimikwa jana kushika wadhifa huo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathias Mulumba, mjini Songea, alisema Katiba iliyopo imefanikiwa kuwaunganisha Watanzania kiroho na sio katika makaratasi, ambayo yanaweza kuchakachuliwa wakati wowote.

Akizungumza katika Ibada hiyo maalumu, Askofu Dallu alifikia hatua akasema, Katiba iliyopo ingeweza kuendelea kutumika kwa kuwa ina mambo mengi ya msingi na kwa mtazamo wake, upungufu upo lakini ni kidogo na unaweza kurekebishwa.

‘’Ndugu zangu, Tume ya Warioba ilifanya kazi nzuri ya kukusanya maoni kutoka kwa Watanzania, lakini tungeweza kutumia Katiba iliyopo sasa ambayo ina mambo mengi ya msingi na upungufu kidogo ambao unaweza kurekebishika,” alisema.

Askofu Dallu ambaye amesimikwa baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francis, alisema kuna watu wanaodhani kuwa Katiba mpya ikipatikana matatizo yao yote yatakuwa yamekwisha na kuhadharisha kwamba mawazo hayo si sahihi.
Badala yake aliwataka Watanzania wamuombe Mungu awasaidie kupata viongozi watakaoongoza Taifa kuanzia ngazi ya chini mpaka juu, kwa kufuata maadili ili nchi isije ikaingia kwenye machafuko.

Askofu Dallu amesema hayo wakati hoja kubwa katika mchakato unaoendelea wa kupata Katiba mpya, ikiwa muundo wa Muungano, uliogawa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika makundi mawili ya watetezi wa Muungano wa serikali tatu na watetezi wa Muungano wa serikali mbili.

Watetezi wa Muungano wa serikali mbili, msingi wa hoja yao ni umoja, mshikamano na amani ya Watanzania, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Watetezi hao ambao ndani ya Bunge Maalumu la Katiba wameunda umoja wao wa Tanzania Kwanza, wamekuwa wakiungwa mkono na wasomi na wakisisitiza kuwa Muungano wa serikali tatu, si tu utavunja Muungano uliodumu kwa mika 50 sasa, lakini pia utavuruga umoja na mshikamano wa Watanzania.

Mmoja wa wasomi wanaounga mkono Muungano wa serikali mbili, Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amekuwa akionya kuwa muundo wa serikali tatu, unaotaka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika, utaibua ubaguzi kati ya Wazanzibari na watakaokuwa Watanganyika.

“Sasa kwa kuwa Zanzibar tayari ina Katiba yake, inayotoa na kulinda haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Wazanzibari, huhitaji nguvu za kinabii kubashiri kuwa Katiba ya Tanganyika ikija, itatoa na kulinda haki za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa Watanganyika.

“Hii ikitokea, itasababisha wananchi kutoka Tanganyika wanaoishi Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanganyika kushindwa kudai haki zao za uraia kisheria,” alionya Profesa Rutinwa.
Katika mazingira hayo, mfumo unaopendekezwa wa serikali tatu, utafifisha mshikamano wa Watanzania na serikali za nchi washirika, na katika hali mbaya zaidi utazalisha kero mpya za Muungano zitakazokuwa na nguvu ya kuvunja Muungano.

“Kunahitajika umakini katika hili, la sivyo historia imeshaonesha kuwa ni rahisi kuvunja Taifa kuliko kulikusanya na kulijenga upya,” ameonya Profesa Rutinwa.

Katika sehemu ya ushauri wake, Profesa Rutinwa alipendekeza pamoja na mambo mengine, utatuzi wa kero za Muungano, ufanyike pamoja na kulitazama wazo la kuwa na serikali moja, ambayo kwa mujibu wa ushauri huo, serikali hiyo ndiyo lengo la siku nyingi la Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Watetezi wa Muungano wa serikali tatu, wamekuwa na hoja tofauti ambazo zimekuwa zikitolewa na kubadilishwa kulingana na mazingira, lakini kila mara wakidai wanatetea mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya, inayopendekeza serikali tatu.

Kwanza watetezi hao ambao ndani ya Bunge Maalumu la Katiba wamejiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walidai kuwa Muungano uliopo ni batili kwa madai kuwa hakukuwa na Hati ya Muungano na Sheria ya Kuridhia Muungano, sahihi zake zimechakachuliwa.

Serikali ilipotoa Hati halisi ya Muungano, Ukawa ilibadilisha hoja na kudai kuwa watahitaji ikaguliwe na wataalamu wa kimataifa na baadaye kurudi katika hoja ya kutetea maoni ya rasimu ya Katiba mpya, iliyotengenezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Baada ya kupoteza hoja kulikosababishwa na kutolewa hadharani kwa Hati ya Muungano, wajumbe hao walianza kujenga hoja kutaka Bunge Maalumu la Katiba, lisibadilishe maoni ya rasimu ya Katiba yanayotaka Muungano wa serikali tatu.

Kupungua nguvu kwa hoja ya Muungano wa serikali tatu, kulisababisha wajumbe hao mwishoni mwa Bunge Maalumu la Katiba, kutoka nje ya Bunge na ambapo sasa wameazimia kutembea nchi nzima kunadi walichoita utetezi wa rasimu ya Katiba mpya.

Akitoa salamu za Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Mkoa Said Mwambungu, alisema Serikali itatoa ushirikiano kwa Askofu huyo kwa kuwa inaunga mkono juhudi za Kanisa Katoliki katika kutoa huduma katika sekta ya afya, elimu, kilimo na maji.

Alisema mafanikio katika sekta hizo katika Mkoa wa Ruvuma, yamechangiwa na viongozi wa dini ambao walikuwa wakijituma kwa bidii kusaidia wananchi bila kujali madhehebu wanayotoka, na kuipa Serikali faraja na inaomba ushirikiano huo uendelee.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii badala ya kuitegemea Serikali au Kanisa kuwaletea maendeleo jambo ambalo linaweza kusababisha waendelee kuwa masikini.


Related

Kitaifa 8751387871873816645

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item