JAMII: MENEJA EWURA AJIUA KWA KUHOFIA MKONO WA SHERIA, NI BAADA YA KUHOJIWA NA KAMATI YA BAJETI
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/jamii-meneja-ewura-ajiua-kwa-kuhofia.html
Dar/Dodoma. Meneja Biashara wa Petroli wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) amekutwa amekufa hotelini
katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar
es Salaam akitoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na
jukumu la kupanga bei za mafuta za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho
mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo
mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa
fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha
za mfuko wa barabara.
Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha
tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia
tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na
waombolezaji waliokuwa kwenye vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi
kilifanyika ndani ya nyumba ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye
kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura,
akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kugundua
kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili
kutozwa kodi.
Gashaza alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura
kwenye kamati hiyo ya Bunge akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura,
Felix Ngamlagosi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo,
takwimu za Ewura ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi
ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe
takwimu za mamlaka ya mapato.
Habari hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es
Salaam juzi majira ya saa tatu usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na
badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako
mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi
kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa kuwa marehemu aliomba akalale hotelini
kwa sababu hakuona kama ana amani kulala nyumbani kwake na ilipofika
asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani kwa marehemu waombolezaji walikusanyika
katika makundi, lakini baada ya kukaa katika kikao cha familia walitoka
na kauli moja kuwa hawatasema chochote na kwamba jukumu hilo libaki
mikononi kwa polisi.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Seleiman Kova
hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akidai kuwa anayetakiwa
kulizungumzia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo.
Alipotafutwa, Kamanda Kiondo alisema kulingana na
taarifa zilizopo Gashaza aliitwa bungeni Mei 14 na akarejea Dar es
Salaam Mei 17. Alisema aliporejea, Gashaza aliaga nyumbani kwake kuwa
hajisikii vizuri na kuelekea Hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo ambako
alichukua chumba Namba 113.
Kamanda Kiondo alisema akiwa hotelini, Gashaza
alimpigia simu rafiki yake mmoja anayejulikana kwa moja la Silipwango
akimweleza kuwa yupo hotelini hapo kujipumzisha kwa sababu bungeni
aliulizwa mambo ambayo hayakumpendeza na kwamba alihitaji kupumzika.
Rafiki huyo, kwa mujibu wa Kiondo, alimpigia simu
mkewe anayeitwa Judith akamweleza alivyoelezwa na mumewe na baadaye kwa
pamoja wakamfuata hotelini ambako baada ya kuzungumza nao kwa muda
mfupi, aliwaomba wamuache apumzike na ndipo walipoondoka.
Asubuhi, Silipwango alipigiwa simu na mkewe
kumueleza kuwa Gashaza hakurudi nyumbani na akaamua kupitia kwenye
hoteli waliyomuacha na alipofika akakuta watu wamejaa. Alipouliza
akaelezwa kuwa kuna mtu amejinyonga chumbani.
Kamanda Kiondo alisema Gashaza alijinyonga kwa
kutumia tai aliyoifunga kwenye bomba la maji ambalo pia lilikatika na
hivyo kuukuta mwili wake ukiwa sakafuni.
Kilichojiri kamati ya bajeti
“Kisheria kodi ya mafuta ni Sh263 kwa lita
inakwenda mfuko mkuu Hazina na Sh50 inakwenda kwa Wakala wa Umeme
Vijijini (Rea), lakini takwimu za mafuta yaliyouzwa inayostahili kutozwa
kodi kati ya TRA na Ewura zinatofautiana,” alisema mmoja wa wajumbe.
“Kwa hiyo Kamati ya Bajeti iliwaita wote (Ewura na
TRA) na kwa kweli wajumbe wa kamati tulikuwa wakali sana, hatutaki
mchezo tulitaka kujua nani anasema ukweli,” alidokeza mjumbe huyo.
“Uko ugomvi mkubwa tu kati ya TRA na Ewura kuhusu
nani hasa mwenye takwimu halisi,” alisema mjumbe huyo na kudokeza kuwa
meneja huyo alisema kila kitu kwa uwazi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa
baada ya vuta nikuvute ndani ya kamati hiyo, iliamuliwa watendaji wa
vyombo hivyo viwili wakafanye ulinganisho na kupeleka jibu kwa kamati
hiyo. Ewura waliwasilisha takwimu zao Jumamosi.
“Tension (mvutano) ni kubwa kwa sababu kuna watu
wizarani hawazitaki takwimu za Ewura na wanataka za TRA ambazo sisi kama
wajumbe tunaziona hazina uhalisia kunaweza kukawa na ufisadi,”
alisisitiza mjumbe mwingine.
Chenge azungumza
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew
Chenge alipoulizwa jana, alikiri kufanyika kwa kikao kilichomuhusisha
meneja huyo na kwamba taarifa alizotoa zilionekana tofauti na zile za
TRA.
“TRA ni chombo cha Serikali na Ewura ni chombo cha
Serikali, kwanini wawe na takwimu zinazotofautiana? Hilo tu ndio
tumewaagiza wakae pamoja watuambie zipi ni takwimu halisi,” alisema
Chenge.
Alipoelezwa kuwa mmoja kati ya maofisa wa Ewura
waliofika mbele ya kamati yake amejinyonga, Chenge alionyesha kushtushwa
na kuhoji kama taarifa hizo zina ukweli.
“Una uhakika kwamba amejinyonga? lini? Kama ni
kweli basi ni jambo la kusikitisha sana, lakini hiyo sasa ni kazi ya
polisi. Mimi nisingependa sana kuzungumza, tuwaachie wao wachunguze
sababu za kifo chake,” alisema Chenge.
Serikali inaelezwa kuwa katika hali mbaya kifedha
na kamati hiyo ya Bajeti imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuinusuru
kwa kukutana karibu kila siku na Hazina na wadau wengine wanaochangia
fedha katika mfuko wake.
Kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 iliyopitishwa na
Bunge, Serikali imejikuta ikiwa na upungufu wa Sh1.8 trilioni hali
ambayo kamati ya bajeti inatafuta kila njia ikiwamo kushauri vyanzo
vipya vya mapato ili kunusuru bajeti ya mwaka huu wa 2014/2015.
Bajeti ambazo zinaelezwa kuiumiza kichwa Serikali
ni ya Maji, Miundombinu na Nishati na Madini ambazo zinaelezwa kupata
mgawo kidogo mwaka jana na kuzifanya zishindwe kutekeleza miradi
mbalimbali.
Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alisema alipata taarifa jana saa 3:00 asubuhi.
Alithibitisha kuwa marehemu alikuwa Dodoma kikazi kwenye vikao na kamati ya Bunge tangu Alhamisi iliyopita.
Baada ya kumaliza kazi ndiyo ndiyo jana (juzi)
alichelewa sana kurudi ndipo alipoamua kujipumzisha kwenye nyumba ya
wageni (iliyopo karibu na nyumbani kwake) ambako alikutwa amefariki,”
alisema Samwel.
Alisema marehemu alikuwa mwadilifu, mchapa kazi na asiye na tatizo lolote kazini na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa.
Chanzo:Mwananchu