jaridahuru

Mitandao

ELIMU: WAALIMU WAIKIMBIA SHULE KUTOKANA NA IMANI ZA KISHIRIKINA



Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nfunzi iliyoko katika kijiji cha Nyakasaa kisiwani Kome Wilaya ya Sengerema mkoani  Mwanza, Jaqueline Massawe, pamoja na walimu kadhaa, wameikimbia shule hiyo kutokana na imani za kishikirina.
Kutokana na imani hiyo, Idara ya Elimu wilayani Sengerema, imepanga kuwapeleka walimu ambao ni wazawa wa kisiwa hicho kuchukua nafasi ya walimu waliondoka kama njia ya kutatua tatizo hilo katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 500.

Walimu hao wanaofikia saba, walianza kuikimbia shule hiyo tangu Novemba, mwaka jana  baada ya baadhi ya walimu wenzao kudai kunyolewa nywele usiku zikiwamo sehemu zao  za siri.

Hali kadhalika, wengine walidai kucharazwa viboko wakiwa wamelala usiku, hali iliyoibua hofu miongoni mwao.

Shule hiyo inayomilikiwa na serikali, ina majengo bora ukilinganisha na shule zote 183 za msingi za wilayani Sengerema.

Aidha, majengo ya shule hiyo yalikabidhiwa kwa jamii ya wanakijiji hicho Juni, mwaka jana baada ya kujengwa na wafadhili wa kutoka nchini Korea kupitia shirika la Good Neighbour (GNT) kwa gharama ya Sh. milioni 340.

Kwa sasa shule hiyo imebakiwa na mwalimu mmoja tu, Justine Katwale, na ndiye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo akisaidiwa na walimu wasio waajiriwa wanaolipwa posho na wazazi.

Kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo, wakati fulani ililazimika kwa wanafunzi kupewa mitihani na kwenda kuifanyia nyumbani na ikasahihishwa na wazazi wao kutokana na kukosa walimu.

Hali hiyo imeichukiza jamii ambayo katika mkutano mkuu wa kijiji, ulipitisha azimio la kukemea vitendo vinavyodaiwa kuwa ni vya kishirikina huku wanakijiji hao wakiteketeza kwa moto nyumba 10 za familia zinazotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo.

Mbali ya kuchoma moto nyumba za wanakijiji wenzao, pia waliwamtimua kijijini hapo.

''Ni jambo la kusikitisha kwa watuhumiwa kuchomewa nyumba zao moto, lakini pia ililazimu kuchukua hatua hiyo kutokana na ukweli kuwa athari yake ya kuwapoteza walimu ilikuwa ni kubwa zaidi kuliko kuwa na uvumilivu,'' alisema mmoja wa wanakijiji hao huku akitaka asitajwe jina lake.

Shule hiyo ilifunguliwa mwaka jana na wanafunzi waliopo walichukuliwa kutoka shule za jirani.

Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Katwale alidai kuwa alichukua jukumu la kujenga ujasiri wa kutoondoka kutokana na kutoamini imani za kishirikina.

Hata hivyo, Katwale alidai kuwa anatimiza majukumu yake licha ya kwamba yuko katika mazangira magumu.

Kwa mujibu wa Katwale, kwa sasa anasaidiwa na wahitimu wa kidato cha nne waliojiriwa na wazazi kupitia kijiji ambao wamekuwa wakilipwa posho kwa makubaliano.

Ofisa Elimu Wilaya ya Sengerema, Juma Mwajombe, akizungumzia hali ya shule hiyo kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, alisema suala hilo linapaswa kutatuliwa kwa jamii kushirikiana na serikali badala ya kuiachia serikali kwani jamii ina jukumu kubwa katika  kulipatia ufumbuzi.

''Ni kweli hali hiyo baada ya kutokea walimu waliikimbia shule hiyo na kubakiwa na mwalimu mmoja, lakini tayari walimu wamehamishiwa hapo na mizigo yao itapelekwa baadaye.

Kilichofanyika ni kupeleka walimu wazawa wa kisiwani humo hatua ninayoamini italipatia ufumbuzi tatizo hilo," alisema Mwajombe.

Aliongeza kuwa shule hiyo awali ilikuwa na walimu  saba na baada ya kutokea mtafaruku huo, waliikimbia na kubakiwa na mwalimu mmoja.


Chanzo: Nipashe

Related

Habari Mpya 235082139106091684

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item