BUNGENI: "WIZARA YA MALIASILI IMEJAA USANII MTUPU" Msigwa.
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-wizara-ya-maliasili-imejaa.html
Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema
Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa ubabaishaji na ‘mvutano wa
kimasilahi’ baina ya waziri na katibu mkuu, hivyo kukwamisha shughuli
za kuendeleza utalii.
Msemaji wa kambi hiyo (Maliasili na Utalii),
Mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akisoma maoni
kuhusu hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa
mwaka 2014/15.
Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na mvutano
baina ya Waziri Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi
ambao unaonyesha udhaifu wa Serikali.
“Hii inathibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa
kuwa, waziri na katibu mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila
kushirikiana na kila mmoja anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala
ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.
Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha
kazi wakurugenzi wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema
taratibu za kuwafukuza hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye
(Nyalandu) siyo msafi kwa kuwa anashindwa hata kujua mipaka yake ya
kazi.
Mbali na mvutano huo, Msigwa alisema maazimio ya
Bunge kuhusu matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili yanaendelea
kupuuzwa na watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo.
“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote
hamfichi mnafiki na debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali
ya wahenga). Siyo mara ya kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi
wa Lazaro Nyalandu,” alisema.
Alisema Waziri Nyalandu alipozungumza katika kikao
cha wadau wa ulinzi wa maliasili Juni mwaka jana mkoani Iringa,
aliahidi kuwa majina ya majangili yakiwamo ya vigogo yangetangazwa
hadharani, lakini hadi sasa hakuna majina yoyote yaliyotangazwa
hadharani.
Uteuzi wa Sarakikya
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema) alizungumzia kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Paul
Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo alilosema
ni kinyume na haki za binadamu.
Msemaji huyo alibainisha kuwa, wakati wote
Watanzania wanajiuliza maswali ambayo hayajapata majibu kuhusu vigezo
vilivyotumika kumteua Sarakikya.
“Katika Operesheni Tokomeza, mtu huyu alikuwa
kiongozi wa utekelezaji wa moja kwa moja na kinachodaiwa ni uvunjifu wa
haki za binadamu, inashangaza kuona mtu huyu tena ndiye ana nafasi ya
kukaimu ukurugenzi, lini kawa msafi?” alihoji Msigwa.
Msigwa pia alizungumzia shehena ya meno ya tembo ambayo alisema
Serikali inatafuta soko lake badala ya kuyateketeza kwa kuwa kuuza ni
kuchochea ujangili nchini.
Kudharau Mahakama
Msigwa alisema Mkurugenzi wa Wanyamapori alipuuza
uamuzi wa Mahakama ulioizuia Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris
Limited kuwinda baada ya kubainika inavunja sheria.
Msigwa alisema kuna taarifa kuwa kampuni hiyo
ilishapewa zuio na mahakama la kufanya uwindaji kutokana na kutozingatia
sheria, lakini ilipitia mlango wa nyuma na kuomba kibali cha uwindaji
na kupewa.
Ajibu hoja
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge jana jioni,
Nyalandu alisema Serikali itachukua vielelezo vyote vya Msigwa kuhusu
Kampuni ya Green Miles Safaris Limited kufanya shughuli zake kinyume cha
sheria na kuvifanyia kazi.
Kwa upande wa wakurugenzi wizarani, alisema kuna
upotoshaji wa baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwa hakuna mfanyakazi
aliyefukuzwa kazi. .. “Siyo Mkurugenzi Bwana Songorwa (Alexander) wala
mtumishi mwingine.”
Alisema hatua aliyochukua ni kuwahamisha vituo vya
kazi, Profesa Songorwa alipelekwa Chuo cha Mwika kuwa mwalimu wakati
Profesa Jaffar Kidegesho alihamishiwa Hifadhi ya Selous.
“Sheria ya utumishi wa umma haikuvunjwa wala
kanuni zake, naomba nilithibitishie Bunge lako kuwa habari hizi nyingi
za kwenye magazeti hazikuwa na usahihi wowote,” alisema.
Akizungumzia shutuma za Kambi Rasmi ya Upinzani
juu ya kuteuliwa kwa Sarakikya kuwa Kaimu Mkurugenzi Wanyamapori,
Nyalandu alisema hakuna anayeweza kuyaelewa yote yaliyotokea katika
Operesheni Tokomeza ila hadi hapo Tume ya Kimahakama itakapokamilisha
kazi yake.
“Ndugu Sarakikya ni mmoja watumishi waandamizi na
waliobobea katika kazi walizofanya… Kwa hali yoyote ile Serikali
haitamwonea mtu haya endapo atabainika na tume hii kwamba alivunja
maadili yake,” alisema.
Ingawa Nyalandu hakujibu kuhusu uhusiano wake
kikazi na Katibu Mkuu Tarishi, baada ya bajeti yake kupitishwa Spika wa
Bunge, Anne Makinda alisema yamezungumzwa mambo mengi kuhusu suala hilo,
hivyo inaonyesha kuna tatizo.
Makinda alishauri waziri kuyo na katibu mkuu wake washirikiane ili kutimiza malengo ya Serikali.
Makinda alishauri waziri kuyo na katibu mkuu wake washirikiane ili kutimiza malengo ya Serikali.
Chanzo:Mwananchi