BUNGENI: MAFISIDI wa Fedha za IPTL kuona cha Mtema Kuni
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-mafisidi-wa-fedha-za-iptl-kuona.html
Dodoma. Tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh200
bilioni katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
zinaonekana kuwa kaa la moto na jana zilitikisa Bunge na kuibua mvutano
mkali.
Hata hivyo, suala hilo sasa limekabidhiwa kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini ukweli wake.
Tuhuma hizo ziliibuliwa juzi na Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye alisema kashfa hiyo ni
zaidi ya ile ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT iliyotokea mwaka
2005.
Kafulila alisema ufisadi huo unamhusisha Waziri wa
Nishati na Madini, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Gavana wa BoT na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa
Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu
Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick
Werema.
Hata hivyo, akihitimisha hotuba ya bajeti yake na
kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwagiza
CAG na Takukuru kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.
“Hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa
pesa kutoka akaunti ya Escrow na kuzipeleka IPTL. Tunajiuliza kama ni
ufisadi, ni ufisadi wa nini wakati fedha zile ni za IPTL?” alihoji
Pinda.
Pinda alifafanua suala hilo lilipoandikwa kwa
kirefu na gazeti dada la Mwananchi (The Citizen), CAG aliwasiliana na
Katibu Mkuu wa Nishati, Gavana wa BoT na Mkurugenzi wa Tanesco ili
kupata picha ya mchakato mzima.
“Wakati akiendelea hivyo, CAG akapata barua kutoka
kwa Katibu Mkuu wa Nishati akimwomba afanye uchunguzi wa kina na wakati
huo huo kamati ya PAC nayo ikamwelekeza kuchunguza jambo hilo.”
Waziri Mkuu aliongeza kusema: “Kwa tuhuma zenyewe
zilivyo, itabidi tuwahusishe Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao
ili kupata ukweli.
“Kwa maelezo na mtiririko ulivyo, kinachobaki ni
tuhuma zinazojitokeza ambazo upo uwezo mkubwa wa vyombo hivi kuweza
kuzibaini. Naliomba Bunge lako likubali CAG akubali kukamilisha kazi
hiyo.”
Waziri Mkuu alisema wako viongozi wa Serikali
ambao wametuhumiwa katika suala hilo hivyo ni vyema likachunguzwa kwa
uzito wake ili wale watakaobainika wamekula rushwa washtakiwe.
Katika ufafanuzi wake huo, Pinda alisema katika mabishano hayo
yako maswali ambayo anafikiri ni ya msingi kuhojiwa ikiwamo kama IPTL
ililipa kodi stahili zinazohusiana na pesa hizo.
Pinda alisema kisheria, fedha zile zilipokuwa
zinakwenda Escrow, akaunti zilipaswa kukatwa kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT), na wabunge wanaweza kuhoji kuanzia hapo.
Hali kadhalika, Waziri mkuu alisema wabunge
wanaweza pia kuhoji kama wakati IPTL inauzwa kwa mwekezaji mpya kampuni
ya PAP kama ililipa kodi kama sheria za nchi zinavyotaka.
Waziri mkuu alisema hata uamuzi wa mahakama ya
kimataifa ya usuluhishi, ilielekeza fedha hizo zipelekwe IPTL kwa vile
ni zao na zilitunzwa tu katika akaunti hiyo katika kipindi cha mgogoro.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza kuwa PAC
imekwishamwandikia barua ikimtaka akubali CAG achunguze suala hilo na
yeye amekubali, na taarifa yake itapelekwa bungeni kupitia PAC.
Hata hivyo, kulitokea mzozo kati ya Spika na
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika baada ya Mnyika kumtuhumu Spika kuwa
anafanya kazi ya Serikali badala ya kumwacha Waziri mkuu atoe majibu.
Mnyika alikuwa akishikilia msimamo wa kuundwa kwa
kamati teule akisema uko uzoefu wa miaka ya nyuma ambapo CAG alitumika
kuisafisha kampuni ya Richmond katika kashfa ya kufua umeme.
Mbunge huyo alisema suala la kuamua kama iundwe
kamati teule ya Bunge ama la inatakiwa kufanywa na Bunge na siyo Spika
hivyo kwa mtazamo huo, Spika anafanya kazi ya Serikali.
Hata hivyo, Spika alimtaka Mnyika akae chini kwa
sababu tayari suala hilo litashughulikiwa na CAG na haiwezekani mambo
mawili kwenda kwa wakati mmoja kwani huko ni kupoteza muda.
Mnyika alijaribu bila mafanikio kumweleza Spika
kuwa anataka kuondoa shilingi kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu
inayofikia Sh5 trilioni kwa mwaka 2014/2015 lakini aligonga mwamba.
Kwa upande wake, Werema alisema suala la akaunti
ya Escrow, Watanzania wanayo haki ya kujua kama kodi mbalimbali
zilizotakiwa kulipwa kisheria, kama zililipwa na IPTL na washirika wake.
“Ni vizuri tuelewe, unapomtaka Waziri mkuu auende
kamati teule hiyo siyo kazi yake…, kama kuna ufisadi lazima ujulikane
lakini vitu vyote viko wazi,” alisisitiza Werema.
Kabla ya Waziri mkuu kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina aliomba mwongozo
wa Spika akisisitiza Kafulila alisema uongo.
Mpina alisema maelezo ya Kafulila kuwa Gavana wa
BoT alipobanwa na kamati yake alikiri kutoa fedha hizo kwa shinikizo,
yalikuwa siyo ya kweli na wala hayakutamkwa na Gavana mbele ya kamati.
“Maelezo ya Gavana wa BoT ninayo, haiwezekani
watendaji wa Serikali wanafika mbele ya kamati halafu wanakuja kuzushiwa
maneno ambayo hawakuyasema.
“Mimi jana baada ya tukio hili kutokea, niliwaita
wajumbe wangu kwa sababu suala hili liliwasilishwa kwa mfumo wa semina,
hatukuwa na hansard, tuliwauliza wote wakasema halikusemwa.
Hata hivyo, alisema kwa vile suala hilo lina
harufu ya rushwa ni vyema CAG akashirikiana na Takukuru kuchunguza kwa
vile taasisi hiyo inayo mamlaka kisheria kuzifikia kampuni binafsi.
Baada ya maelezo hayo, Kafulila alisimama na
kuomba mwongozo wa Spika akisema jambo hilo ni kubwa na limekuwapo
tangu mwaka 2005 mpaka leo na kutaka apewe nafasi ya kuthibitisha.
“Kwa sababu ya unyeti wa jambo lenyewe kuwagusa
vigogo ambao ushahidi wa kila mmoja alivyohusika ninao, niruhusiwe ili
nithibitishe kila mmoja alivyohusika kwenye ufisadi huu,” alisema.
“Mheshimiwa Spika, tuache mizunguko na porojo
nyingine, twende kwenye uhalisia. Kuna kodi zimekwepwa, kuna ufisadi
umefanyika, wananchi wanataka kujua ukweli wa jambo hili,” alisema.
CHANZO : MWANANCHI
CHANZO : MWANANCHI