BUNGENI: LISSU AWASILISHA NYARAKA NYETI NA KUIBUA SIRI YA MUUNGANO
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-lissu-awasilisha-nyaraka-nyeti.html
Kambi ya Upinzani imedai kuwa na ushahidi wa nyaraka ambazo zimewasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano unaonyesha kwamba Muungano uliopo ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji ambao nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya Tanganyika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Tundu Lissu, katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2014/15.
“Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi moja kubwa ya Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa koloni lake. Kwa sababu maneno haya yanaweza kupotoshwa na wale ambao wamefaidika na uhusiano huu wa kikoloni kati ya Tanganyika na Zanzibar,” alisema Lissu.
Alisema kutokana na hali hiyo, kwa miaka mingi Zanzibar imelalamika kwamba inapunjwa katika mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotolewa na nchi wafadhili na taasisi za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano na hivyo mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu utaratibu wa mgawanyo wa mapato hayo kuangaliwa upya.
Alidai kuwa serikali ilijibu kuwa hali hiyo inashughulikiwa kwa umakini, lakini alisema majibu hayo ni ya uongo.
Lissu alimnukuu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), akitoa taarifa kwenye kamati hiyo kwamba kwa mwaka wa fedha 2013/14, hadi kufikia Machi, 2014 SMZ imepata gawio la misaada ya kibajeti ya Sh. 27,190,502,190.97 kati ya Sh. 32,627,535,000 zilizoidhinishwa na Bunge.
“Hii ndiyo kusema kwamba kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa Zanzibar, ni asilimia 83 ndizo zilizolipwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha,” alisema Lissu.
Alisema kama Zanzibar ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato hayo, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali, mwaka jana peke yake gawio halali la Zanzibar la misaada na mikopo ya kibajeti lingekuwa Sh. bilioni 52.335.
“Badala ya kupatiwa Sh. bilioni 52.335 ambazo ni fedha zake halali, Zanzibar iliidhinishiwa Sh. bilioni 32.627 au asilimia 52 ya fedha zake halali.
Fedha hizo ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za misaada na mikopo ya kibajeti kwa Jamhuri ya Muungano. Fedha zilizobaki, yaani Shilingi trilioni 1.130 au asilimia 97.2 ya fedha zote za misaada ya kibajeti zimetumika na zitatumika Tanganyika,” alisema Lissu na kuongeza:
“Kwa ushahidi huu wa nyaraka mwaka jana peke yake Zanzibar iliibiwa Shilingi bilioni 25.145 au asilimia 48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.”
Lissu alieleza kuwa mapendekezo yaliyopelekwa bungeni na Serikali, Zanzibar itaibiwa fedha nyingi zaidi kwa mwaka huu wa fedha 2014/15.
Alidai kuwa kama Serikali ingeheshimu utaratibu wake wa asilimia 4.5 ya fedha hizo kwa Zanzibar, gawio halali la Zanzibar kutokana na fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka ujao wa fedha lingekuwa Sh. bilioni 44.647.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa Wazanzibari kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na misaada na mikopo ya kibajeti inayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano hazijalipwa kwa mwaka jana wa fedha?” alihoji.
Kambi hiyo pia inaitaka Serikali kupeleka bungeni takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo ya kibajeti kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na sehemu ya fedha hizo zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho.
SHEREHE ZA MUUNGANO Kuhusu sherehe za miaka 50 ya Muungano, Lissu alisema zilipambwa na picha za baadhi ya waasisi kwa Tanzania Bara, lakini kwa Zanzibar barabara zilipambwa na picha za marais wa huko tu.
Alidai kuwa Muungano haujawahi kuungwa mkono Zanzibar na kwamba pengine ndiyo maana hata picha za kuchanganya udongo zinazoonyeshwa kila uchao zinamwonyesha Mwalimu Nyerere akichanganya udongo peke yake, wakati Sheikh Karume haonekani kabisa.
Alisema katika picha hizo za kumbukumbu ya Muungano anaonekana Hayati Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano kwa upande wa Tanganyika wapo Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa Zanzibar wanaoonekana ni Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo.
Lissu alisema katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia kilichochapishwa mwaka 2010, Harith Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, na baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26 ya mwaka huo.
“Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwa nini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake?” alihoji.
Alisema Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo wakati Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Kwa upande wa Tanganyika, alisema Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Munanka alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Akinukuu kitabu hicho, alisema mwandishi wake alionyesha jinsi akina Hanga, Twala na Saadalla na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo,” alisema.
MJADALA MKALI
Suala la Muungano wakati wa jioni liliendelea kuliteka Bunge huku baadhi ya wabunge wakidai kuwa Zanzibar haijanufaika na wengine wakitaka kuitishwa kwa kura ya maoni juu kwa wananchi kama wanautaka Muungano na uwe wa muundo gani.
Mbunge wa Mbulu (Chadema), Mustapha Akunaay, alisema ni vyema serikali ikatumia Sh. bilioni 20 za Tume ya Kabadiliko ya Katiba, kutunga muswada wa sheria ya kuwawezesha wananchi kupiga kura ya maoni ya kama wanataka kuwapo kwa Muungano na uwe wa muundo gani.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF) Mohamed Mnyaa, alisema Waziri wa Muungano ametumia asilimia 86 ya hotuba yake kuzungumzia suala la mazingira na kuacha suala la Muungano ambalo alilizungumzia kwa asilimia 14 kana kwamba ni jambo dogo.
Alisema kwa mujibu ya hotuba ya Waziri Mkuu Bungeni, asilimia 90 ya Watanzania walizaliwa baada ya Muungano na kwamba pamoja na takwimu hizo haifai kunyamaza kwa kuwa kuna dhuluma.
Waziri wa Fedha, Saada Salumu Mkuya, alisema mikopo ya nje ni tofauti na mikopo ya kibajeti. Alisema misaada na mikopo nafuu Zanzibar inaweza kupata yenyewe na kwamba bajeti ya Sh. bilioni 750 kati yake asilimia 50 inatokana na fedha za wahisani.
Alisema Zanzibar inaweza kupata misaada kwa asilimia 100 na kwamba Serikali ya Muungano jukumu lake ni ufafanuzi wa fedha hizo na Zanzibar inapelekewa mchanganuo.
Mkuya alisema kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya Zanzibar kinapelekwa na kwamba taarifa zinazotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni upotoshaji.
Chanzo:Nipashe | Na Dunstan Bahai, Salome Kitomari na Ashton Balaigwa,Dodoma.