jaridahuru

Mitandao

PENGO AMPANGIIA MAJUKUMU ASKOFU MWANDAMIZI

 Picha

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amegawa majukumu ya kazi kwa Askofu Mkuu Mwandamizi, Yuda Thadeus Ruwa’ichi aliyeripoti rasmi juzi Dar es Salaam na kulakiwa na waumini wa jimbo hilo kuu na pia Askofu Msaidizi, Eusebius Nzigilwa.

Akizungumza kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya kumkaribisha Askofu Mkuu Mwandamizi iliyofanyika juzi kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Kardinali Pengo ambaye ndiye mkuu wa jimbo hilo alisema Askofu huyo Mwandamizi hakuja Dar es Salaam kupumzika bali kufanya kazi.

Kardinali Pengo alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi amehamishiwa Dar es Salaam baada ya Baba Mtakatifu, Francis kukubali ombi lake (Pengo) la msaidizi, hivyo uwepo wake utasaidia mgawanyo wa shughuli za kichungaji kwenda vizuri kwani jimbo hilo lina parokia zaidi ya 100 na vigango vingi.

Alisema wakati anamwomba Papa hakupendekeza jina la askofu yeyote bali alimwachia Baba Mtakatifu aamue mwenyewe na ndipo alipoamua kumteua Askofu Mkuu Ruwa’ichi kuwa mwandamizi wake.

“Mtuombee sisi maaskofu wenu watatu ili tuwe na imani ya kutambua Yesu ni Mwokozi wa Ulimwengu na ni Mwokozi wa wanadamu kwani yeye ni Mungu na pia ni mwanadamu,” alisema Kardinali Pengo.

Baadaye alitangaza mgawanyo wa majukumu yao kusimamia idara mbalimbali akiwemo mwenyewe. Idara atakazoongoza yeye Kardinali Pengo ni ya Liturujia, Mahakama ya Kanisa, Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) na Utoto Mtakatifu.

Alisema Askofu Mkuu Mwandamizi, Ruwa’ichi atasimamia Idara ya Uchungaji, Utume wa Walei, Teolojia, Haki na Amani pamoja na Caritas, wakati Askofu Msaidizi, Nzigilwa atakuwa na jukumu la kusimamia Idara ya Miito, Katekesi, Mafundisho ya dini, Vijana Wakatoliki na Mawasiliano.

Kardinali Pengo pia aligawa mipaka ya maeneo ya shughuli za kichungaji kwa kila Askofu ambapo Askofu Mkuu Mwandamizi atakuwa akitoa huduma za kichungaji katika eneo lote la upande wa kushoto mwa Barabara ya Nyerere, huku Askofu Nzigilwa akipangiwa eneo lote la upande wa kulia mwa Barabara ya Morogoro na lililobaki katikati ya Barabara za Morogoro na Nyerere litakuwa chini yake.

Askofu Ruwa’ichi alimshukuru Mungu kwa kumpa majukumu mapya na kuomba waumini wote wamwombee ayatimize kwa uaminifu. Aliagiza zawadi ya Sh milioni 80 aliyopewa na Jimbo Kuu la Mwanza, Sh milioni 60 kati ya fedha hizo zirudi jimboni humo ili kufanikisha shughuli za kitume.

Waumini wa kanisa hilo, Getruda Sambalyegula wa Parokia ya Kibaha na Fabian Paulo wa Parokia ya Yombo Dovya, walisema kuwa wamefurahia kuja kwa Askofu huyo Mwandamizi kwa kuwa ataongeza nguvu katika kazi za kichungaji kwa kuwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam ni kubwa na lina parokia nyingi.

Viongozi wa serikali wastaafu waliohudhuria ibada ya hiyo ya misa ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Spika mstaafu, Anne Makinda na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi alipata daraja la upadre mwaka 1981 na mwaka 1999 aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu.

Mwaka 2005 alihamishwa na kuwa Askofu wa Dodoma hadi Januari mwaka 2011 alipoteuliwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza na mwezi Juni mwaka huu akateuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Related

Kitaifa 1426578852057153401

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item